Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hivi Azam FC inataka nini?

Azam Bakhresaa Azam imefanya usajili wa kutisha kuelekea msimu mpya wa 2022/2023

Tue, 19 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mitaani kuna utani unaoihusu Azam FC na ubingwa wa Tanzania. Wanaoitania timu hiyo wanasema ikichukua taji hilo, basi Kampuni ya Azam Media inapata hasara na kushindwa kuuza ving’amuzi.

Inadaiwa ndio maana tangu ilipochukua ubingwa wa Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2014 haijarudia tena kufanya kitendo hicho. Wanaozusha utani huo wanasema Azam FC ikitwaa ubingwa na kupangiwa kucheza mashindano ya CAF haipati sapoti kubwa kutoka kwa watanzania.

Mfano Azam FC ikicheza na KCC ya Uganda hakuna mtu atakayejishughulisha kununua king’amuzi au kununua bando kushuhudia mechi hiyo.

Mashabiki wanaamini watapata tu matokeo katika vyombo vingine vya habari au kuulizana baada ya mchezo kuisha. Hivi Azam na KCC ngapi ngapi?

Lakini inaaminika Simba na Yanga mojawapo ya timu hizo za Kariakoo ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM au Mafunzo za Zanzibar, Azam Media inapata faida kwa sababu mashabiki watanunua ving’amuzi au bando lake kwa wingi.

Hivyo, kampuni ya Azam Media inanufaika zaidi na uwepo wa Simba na Yanga katika biashara yake kuliko uwepo wa Azam FC.

Azam inautaka ubingwa

Achana na utani huo, Azam FC kila msimu huwa inakamia kubeba taji la ubingwa wa Tanzania, isipokuwa inazidiwa ujanja na klabu hizo kongwe.

Ligi Kuu ya Tanzania Bara ya NBC imemalizika Juni 29 na Azam FC imeshika nafasi ya tatu nyuma ya vinara, Yanga na Simba SC.

Tangu msimu wa 2018- 2019 mfululizo Azam FC imejimilikisha nafasi hiyo ya tatu. Huku juu ikiziacha Simba na Yanga zikipishana katika mbio za vijiti kuwania ubingwa na nafasi ya pili. Katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu, Azam FC ilishika nafasi ya nane. Baada ya hapo ikakomaa katika nafasi ya pili. Tangu ilipopanda imeshika nafasi ya pili mara tano.

Azam kama PSG ya kina Messi

Ukitaka kuona kama klabu hiyo inautaka ubingwa wa Tanzania kwa hali na mali, hebu angalia usajili wake wa msimu ulioisha tu. Azam FC ikiwa chini ya Kocha Mzambia, George Lwandamina, imesajili wachezaji kibao wa kigeni lakini bado imeendelea kujikita kataka nafasi ya tatu.

Ilikuwa na wachezaji mahiri wa kimataifa kama vile, Kipa Mganda, Mathias Kigonya, Mcameroon, Ivana Mbala, Mkenya, Keneth Muguna Mugambi na Mzambia, Charles Zullu. Pia, ilikuwa na Raia wa DR Congo, Idris Mbombo na Mzambia, Rogders Kola.

Bado Azam ilikuwa na Wazimbabwe, Never Tigere na Bruce Kangwa, Mghana, Daniel Amoah na Mganda, Nickolas Wadada.Wachezaji chipukizi na wazawa wa Tanzania ndani ya Azam waliochomoza msimu uliopita ni Pascal Msindo, Tepsi Evance na Kipa Wilbol Maseke. Miaka ya hivi karibuni wamekuwa na wachezaji wengine kama kina Kelvin Friday na Bryson Raphael.

Azam FC imekuwa ikifuata nyayo za Simba na Yanga kwa kushindwa kuwaamini chipukizi wake wanaotoka katika kikosi cha pili. Mara kwa mara imekuwa ikiwatoa kwa mkopo katika klabu nyingine.

Maandalizi ya msimu ujao

Ikiwa inajiandaa kwa msimu ujao, Azam FC imewasajili wachezaji watatu wa kimataifa Mnaigeria, Isah Ndala na Waivaory Coast wawili, Tape Edinho na Kipre Junior.

Inadaiwa usajili huu umesimamiwa na mmoja kati ya matajiri wa timu hiyo, Yussuf Bakheresa ambaye anataka kuiona timu hiyo ikichukua taji mojawapo la Afrika. Azam inaweza kufanikiwa kufikia hatua hiyo, lakini inatakiwa kupanga programu za muda mfupi na mrefu kufanikisha malengo yake.

Mfano ni Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa iliyoamini ingebeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita kwa sababu ilikuwa na Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe. Hata Yanga iliyobeba ubingwa wa msimu uliopita ilichokifanya ni kusajili wachezaji iliyowaongezea nguvu kwenye kikosi cha misimu kama minne iliyopita.

Azam FC inakwenda wapi?

Ilipoanzishwa mwaka 2004 wengi waliamini Tanzania imepata timu ya kimbilio lake. Iliaminika Timu ya Taifa ya Tanzania ingevuna wachezaji wengi kupitia Azam FC kutokana na klabu hiyo kuwa na uwekezaji mkubwa wa mzawa.

Azam FC ilipofikia hatua ya kumiliki viwanja vyake vya mechi na mazoezi, gym pamoja na hosteli na vitu vingine wengi wakaamini makubwa yanakuja.

Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ghana, Abeid Ayew ‘Pele’ alipofika Chamazi hakuamini alichokiona pale Chamazi. Alisema hata academy yake ilikuwa cha mtoto mbele ya uwekezaji ule wa Azam.

Hivyo, uwekezaji wa Azam FC ulitarajiwa kuwa funzo kwa Simba na Yanga. Haikutarajiwa kama ingepita katika nyendo za klabu hizo kongwe za kununua wachezaji kibao kutoka nje.

Laiti kama uwekezaji huu wa Azam ungekuwa chini ya viongozi wale wa zamani wa Yanga, labda Tanzania ingeshiriki Kombe la dunia kwa mara ya kwanza. Yanga ilikuwa na uwanja mdogo tu wa Kaunda pale Jangwani lakini iliweza kuwatoa wachezaji wengi waliokuja kuitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Mwaka 1974 Yanga iliwaaandaa wachezaji kutoka katika kikosi chake cha watoto ‘Kids’ hadi B na baadaye wengi wakajiunga na kikosi cha kwanza.

Kikosi kilikuwa na kina Juma Pondamali, Jaffari Abdulrahaman, Rashid Idd Chama, Kassim Manara, Godian Mapango, Mohammed Mkweche, Mohammed Rishard ‘Adolf’ na wengine wengi?

Baadhi ya wachezaji hawa waliofanikiwa kuijenga Timu ya Taifa ya Tanzania iliyoshiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza 1980 kule Lagos, Nigeria.

Yanga ilimwajiri kocha mwenye uwezo kwa ajili ya kuwanoa vijana hao, Raia wa Jamhuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (RDC), Tambwe Leya.

Mwaka 1974, Yanga ilienda Brazil ikiwa na Kocha Professa, Victor Stănculescu na kumkuta Tambwe akiwa masomoni. Timu hiyo ilimchukua kocha huyo kwa ajili ya kufundisha timu ya vijana.

Baadaye Stanculescu aliomba kufundisha timu hiyo ya vijana na kumwachia Tambwe timu kubwa. Tambwe alifanya mabadiliko ya kuwachukua vijana kwenye kikosi chake cha kwanza.

Tambwe na kocha wa Simba Nabi Camara walifukuzwa nchini kwa amri ya Serikali mwaka 1975. Lakini Tambwe alisema ameacha hazina kubwa ya soka la Tanzania na matunda yake tungeyaona. Ni kweli tuliyaona.

Simba ya kina Mkude

Mbali na miaka ya 70 kuwa na timu ya vijana, Simba imewahi kumiliki kikosi cha vijana kilichopanda Ligi Kuu kikiongozwa na Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu Migomba, Abdallah Seseme na Haruna Chanongo.

Wengine ni Said Hamis Ndemla, Alex Christopher, Hassan Isihaka, Ramadhani Singano ‘Messi’, Miraji Athuman, Willian Lucian ‘Gallas’ na Hassan Khatibu na wengine wengi.

Kwa miaka tofauti Azam imekuwa ikiajiri makocha wa timu za vijana za Under 17-20 lakini bado haijaweza kutoa wachezaji kwa mkupuo na kuja kutegemewa kama zilivyofanya Simba na Yanga. Laiti kama Azam ingewekeza zaidi kwenye soka la vijana kwa kutafuta makocha wenye ujuzi na uwezo, tangu ilipopanda Ligi Kuu msimu wa 2008, ndani ya miaka hii Tanzania ingekuwa na lundo la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa katika nchi kadhaa duniani.

Columnist: Mwanaspoti