Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hili la PF3 kwa majeruhi lifanyiwe kazi kwa haraka

Bb190198f393809639c028367d0f3b1f.jpeg Hili la PF3 kwa majeruhi lifanyiwe kazi kwa haraka

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KAMA kuna jambo lililokuwa kizingiti au ukuta katika kuokoa maisha ya watu wanaopata majeraha mwilini kutokana na matukio ya ajali, kuvamiwa, kipigo, kubakwa na yanayofanana na hayo, ni ulazima wa kupata fomu maalum ya polisi namba tatu (PF.3) ili kupata matibabu.

Bila fomu hiyo iliyopo kisheria, hata mtu awe majeruhi anayekata roho dakika chache akiwa eneo la tiba yaani hospitali, hawezi kupatiwa matibabu ili kuokoa maisha yake.

Ni ukweli usiopingika kuwa, sheria inawekwa ili ifuatwe na haitungwi bila kufanyika utafiti unaoleta matokeo ya uhitaji wa uwapo wake, lakini nia hiyo njema ya sheria iliyoweka PF.3, changamoto kubwa imekuwa kwa watu wanaopata majeraha kutibiwa wanapofikishwa hospitalini bila fomu hiyo.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, fomu ya PF.3 hutolewa kwa mtu baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa mlalamikaji au muathirika kwa matukio yenye madhara mwilini, ajali au matukio yenye kuleta mashaka kuhusu vyanzo vyake kama vile kipigo, kujeruhi, ubakaji, kulawiti, kunywa sumu na mengineyo.

Nakumbuka wakati Waziri wa Fedha na Mipango wa sasa, Dk Mwigulu Nchemba akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, aliandika katika ukurasa wake wa Facebook akiagiza kuwa majeruhi na mtu mahututi anapofikishwa hospitalini, atibiwe kwanza wakati mchakato wa kupata PF.3 ukiendelea ili kuokoa maisha yake.

Baada ya kauli hiyo ambayo sina uhakika ilifanyiwa kazi kwa kiasi gani, aliyekuwa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema katika mazingira ambayo hali ya muathirika ni mbaya, huduma za kwanza za kuokoa maisha yake huendelea kutolewa wakati watoa huduma wakiijulisha Polisi ili kuharakisha upatikanaji wa PF.3.

Hata hivyo, utekelezaji wa hili umekuwa njia panda kwa maeneo mengi hasa kutokana na kwamba PF.3 ipo kisheria hivyo ni lazima mabadiliko yafanyike ili kutoa nafasi ya tiba kwa walio mahututi bila fomu hiyo.

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha Ushonaji cha Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam katika Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Polisi, Kurasini, es Salaam, pamoja na maagizo mengine, alilitaka Jeshi la Polisi kuangalia upya sheria kuhusu PF.3.

Rais Samia alisema watu wanaopata ajali wanaumia kwa viwango tofauti, wengine wakihitaji kupatiwa tiba ya haraka wanapofikishwa hospitalini lakini sheria imeweka ulazima kwamba hawezi kuhudumiwa mpaka awe na fomu ya PF.3 hatua inayochangia vifo ambavyo pengine vingezuilika.

“Mtu anapopata ajali wanaomuokota ni ku-panic, mbio hospitali, hawakumbuki kurudi kwanza polisi. Kwa hiyo niombe sana hii sheria muiangalie, mtu anapofikishwa hospitali apate huduma, mambo mengine ya kipolisi yaendelee. Tunapoteza uhai wa mtu sababu ya kipengele kidogo cha PF.3,” alisema Samia alipozungumza katika hafla hiyo.

Nalishauri Jeshi la Polisi kulichukua kwa uzito na kulifanyia kazi kwa haraka suala hili ili kuokoa maisha ya watu yanayopotea kwasababu ya kipengele cha ulazima wa PF.3 ili majeruhi atibiwe.

Napendekeza maboresho ya sheria yafanyike kwa haraka na wakati yakiendelea, kuwe na dawati au dirisha dogo katika vituo vya afya, zahanati na hospitali kubwa ya polisi ili kurahisisha kupatikana kwa fomu hizo wakati majeruhi akiendelea kutibiwa.

Columnist: www.habarileo.co.tz