Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hiki ndicho kilichomstaafisha Hazard kucheza soka

Eden Hazard.jpeg Eden Hazard

Thu, 12 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Juzi Jumanne aliyewahi kuwa winga staa kwa klabu ya Chelsea na Real Madrid, Eden Hazard alitangaza kutundika daluga zake akiwa na umri wa miaka 32 tu.

“Nimetambua ndoto zangu, nimecheza na nilikuwa na furaha,” alinukuliwa Hazard.

Katika taarifa iliyechapwa katika gazeti maarufu la michezo la Hispania lijulikanalo kama la Marca inasema winga huyo alitoa taarifa hiyo kupitia mitandao ya kujamii.

Alinukuliwa akisema; “‘Lazima ujisikilize na uache katika wakati sahihi’. Baada ya miaka 16 na kucheza zaidi ya mechi 700, nimeamua kuachana na soka kama mchezaji wa kulipwa.”

Mtakumbuka msimu wa majira ya joto 2023 Real Madrid ilimuaga kwa heshima winga wake hiyo aliyetua akitokea Chelsea msimu wa 2019/20 mara baada ya kufikia makubaliano binafsi kabla ya mkataba kwisha.

Bahati mbaya winga huyo aliyekuwa katika kiwango cha juu hakuweza kuonyesha cheche zake zilizomfanya kutua klabuni hapo kwa dau la Dola 100 milioni.

Kuandamwa na majeraha mfululizo ndio sababu kuu inayotajwa kumsukuma kuachana na soka akiwa na umri mdogo wa miaka 32 akiwa amecheza mechi 700 kwa kipindi cha miaka 16.

Kufuatia majeraha aliyoyapata katika msimu wa kwanza akiwa Real Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019/20 dhidi ya PSG kwenye Uwanja wa Estadio Santiago Bernabeu hakuwahi kuwa timamu zaidi ya kukabiliana na majeraha ya mara kwa mara.

Majeraha ambayo alikuwa akiyapata mara kwa mara katika maisha yake ya soka na kumfanya kuwa nje ya uwanja muda mrefu ni mchaniko wa misuli ya nyuma ya paja, majeraha ya goti na kifundo cha mguu.

Mtakumbuka hata alipokuwa katika klabu ya Chelsea alikuwa pia akipatwa na majeraha ya mara kwa mara lakini aliweza kupona na kucheza vizuri ukilinganisha na hali ilivyokuwa alipotua Madrid.

MAJERAHA v KIWANGO

Ni kawaida kwa mchezaji ambaye anapata majeraha ya mara kwa mara kushindwa kurudi katika ubora wake kama hapo awali.

Hii inaweza kusababishwa na kutokupona vizuri, kuogopa kuumia tena, kujijeruhi, matibabu dhaifu ya majeraha ya michezo, kuathirika kiakili, kutumika sana, umri kusonga na mazoezi duni ya uponaji.

Mambo mengine ni pamoja na mwili wa mchezaji kuwa mchanga kisoka, mwili kutokuwa na ustahimilivu dhidi ya majeraha yatokanayo na wa mikimiki ya soka ambayo inahusisha kugongana kimwili.

Vile vile mienendo na mitindo mibaya ya kimaisha ya mchezaji wakati akiwa majeruhi au mzima ikiwamo ulaji holela wa vyakula, ulevi, matumizi ya tumbaku na kutoshikamana na matibabu.

Mazoezi tiba anayopewa na timu ya madaktari wanaomtibu mchezaji yanaweza kuwa hayatekelezwi kwa ufanisi hivyo kumfanya mchezaji kushindwa kuwa timamu kimwili hatimaye kucheza akiwa hayuko fiti.

Ikumbukwe kuwa kuwa utimamu wa mwili unaendana na uchezaji wa kiwango. Kwa Hazard kutokuwa timamu kulichangia kushindwa kuonyesha cheche zake zilizomfanya atue Real Madrid kwa dau nono.

Mtakumbuka enzi za Ronaldo de Lima alikuwa katika kiwango cha juu na kuweza kufanya makubwa katika medani ya soka lakini bahati mbaya katika umri mkubwa akiwa katika kiwango cha juu aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara.

Hali hii ilichangia kushindwa kutimiza majukumu yake kwa kiwango katika dakika 90 akiwa katika klabu ya Real Madrid hivyo alipigwa bei akatua AC Milan.

Hata kiungo wa zamani wa Arsenal, Abou Diaby naye aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara hatimaye alimua kukatisha maisha yake ya soka kutokana na hali hiyo.

Mtakumbuka hata Sergio Kun Aguero aliyewahi kuwa mshambuliaji wa Man City na Barcelona aliamua kutundika daluga 2022 mara baada ya kushauriwa na watalaam wa afya hii ni baada ya kupata tatizo la moyo.

Hivyo inawezekana kwa Eden Hazard ameshauriwa na wataalam wa afya kuachana na soka kutokana na kuandamwa mara kwa mara na majeraha yatokanayo na michezo.

Ni kawaida mwili wa mwanasoka anayeandamwa na majeraha mara kwa mara kushindwa kucheza kama hapo awali hii ni kutokana na kuwa nje muda mrefu akijiuguza.

Hata mara baada ya kuachana na Madrid ilielezwa kuwa huenda angelikwenda kucheza katika ligi ya Marekani ambayo ni nyepesi isiyo na majukumu mengi ukilinganisha na EPL na La liga.

Lakini inaonyesha, hakuna klabu ambayo ilionyesha nia ya kumnunua mpaka kufikia majuzi alipotangaza kustaafu soka. Hii ni dhahiri kabisa pengine angeliweza kufeli vipimo vya afya.

Nimewahi kueleza kuwa utimamu wa afya wa mchezaji ndio hutoa mustakabali wa mchezaji kununuliwa au kupewa mkataba katika klabu kubwa za soka la kulipwa.

Pengine baada ya kujitathimini kupitia wataalam wake wa afya imeonyesha kuwa asingeliweza kupimwa na kuonekana kuwa yuko timamu katika klabu ambayo ingemhitaji.

Inawezekana pia historia ya kuwa majeruhi mara kwa mara imefifisha nia ya klabu hizo za Marekani ikiwamo Inter Miami iliyoonyesha nia ya kutaka kumnunua.

Kuwa majeraha mara kwa mara kunaathiri moja kwa moja kiwango cha mwanasoka hatimaye kuonekana kuwa kiwango chake kimeporomoka.

OKOCHA KWA HAZARD

Hapa nchini kuna ugeni wa aliyewahi kuwa staa wa soka duniani katika Ligi Kuu ya EPL na Kombe la Dunia, Augustine Azuka ‘Jayjay’ Okocha akizungumzia afya ya akili ya wanamichezo baada ya kustaafu.

Ujumbe huu unamhusu Hazard hasa ikizingatiwa naye ni binadamu ana mapokeo ya kihisia hata kama ana mamilioni ya dola lakini anahitaji sana kuwa na utulivu wa kiakili ili asiingie katika matatizo ya kiafya ikiwamo msongo wa mawazo, sonona na shinikizo la akili.

Ikumbukwe kuwa kustaafu soka kwa umri wa miaka 32 na soka la kulipwa lililokuwa linamwingizia maelfu ya dola kwa wiki linaweza kumuumiza kihisia hatimaye kupata matatizo ya akili.

Anachotakiwa ni kuwa na ukaribu na wataalam wa afya ya akili, wanasaikolojia na washauri nasaha hasa pale atakapoona anapata dalili za matatizo ya akili ikiwamo kuwa na huzuni, kukosa usingizi, kujitenga, hofu au kutamani kujiua.

Columnist: www.tanzaniaweb.live