Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hii ni heshima ya nchi, tusifanye makosa

Hii Ni Heshima 65340764

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kesho ndio uzinduzi wa michuano mipya ya Ligi ya Afrika (African Football League maarufu kama CAF Super League), shughuli inayofanyika katika ardhi ya Tanzania.

Michuano hiyo inayoshirikisha timu nane itazinduliwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao kwa miezi kadhaa umekuwa kwenye matengenezo na tayari umeshakamilika na kupambwa kwa ajili ya shughuli hiyo inayowaleta nchini viongozi wa juu wa soka duniani na wale wa barani Afrika.

Nafasi iliyopewa Tanzania ya kuwa wenyeji wa uzinduzi huo sio bahati ndogo ukizingatia kuna mataifa mengine yenye ushawishi mkubwa kisoka barani Afrika.

Hivyo ni wajibu kuitumia nafasi hiyo vyema kuanzia upande wa serikali kama yenyewe imekuwa inajinasibu kwa wiki kadhaa sasa juu ya maandalizi ya ugeni unaokuja nchini, lakini kwa viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) na wadau wote kwa ujumla, kushirikiana pamoja ili kufanikisha shuhghuli hiyo ifanyike na kufana.

Ugeni ulioanza kuwasili nchini kwa ajili ya shughuli ya kesho Kwa Mkapa sio wa kitoto na ni fursa nzuri kama nchi kuanzia kwenye sekta ya utalii, kiuchumi na kimaendeleo, kwani wageni wanaokuja wanasaidia kuliingizia taifa pato, lakini wamiliki wa hoteli, vyombo vya usafiri n.k wananufaika pia.

Ndio maana Mwanaspoti tunakumbuka kwamba tukio hili sio la kuchukuliwa kiwepesi, kwani tukifanikisha itasaidia hata kuwavuta zaidi wakati wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) za mwaka 2027 tukiwa wenyeji na majirani zetu wa Kenya na Uganda.

Tunaamini upande wa serikali, TFF wamekamilisha majukumu yao kwa kiasi kikubwa na kusaliwa tukio hilo lifanyike nchini, lakini bado kuna wadau muhimu wanaoweza kutoa taswira nzima ya ustaarabu wa kuhimili shughuli kubwa kama hizo, yaani mashabiki na wapenzi.

Wadau hao wanapaswa kubeba jukumu lao kwa ufanisi kwa kujitokeza kwa wingi Kwa Mkapa, lakini wakawa na ustaarabu katika kushuhudia tukio hilo hadi litakapotamatika kwa mechi baina ya Simba na Al Ahly kwa kuepuka matukio ya aibu kuanzia nje hadi maeneo ya ndani ya uwanja huo.

Tunalisema hili kwa kurejea kwamba Kwa Mkapa unafunguliwa kwa mara ya kwanza baada ya kufungwa ili ukarabati ufanyike na kuna maeneo katika awali ya kwanza yamekamilika, hivyo isitokee tena ukafanyika uhuni wa kuharibu miundo mbinu ya uwanja huo ikiwamo vyooni ama viti, kwani zimetumika fedha kukarabati maeneo yaliyotengenezwa hadi sasa.

Ile tabia ya kurusha chupa za maji na mambo mengine kwa kinachoelezwa kuonyesha hisia za kuchukizwa na soka la wachezaji au maamuzi ya waamuzi ni vitu vinavyopaswa kuepukwa kwa kutambua kuwa soka ni mchezo wa kistaarabu na uungwana na muungwana siku zote ni vitendo.

Hili ni jambo letu kwa faida ya nchi, hivyo ni lazima lifanikishwe kwa ufanisi ili kujenga heshima ya taifa kwa upande wa michezo ili kusaidia kuruhusu matukio mengine kama hayo kuletwa nchini ukizingatia tuna uwanja bora na cha kisasa na asilimia kubwa ya Watanzania ni vichaa wa soka.

Columnist: Mwanaspoti