Mjerumani na mbobezi wa fizikia, Albert Einstein (1879-1955), anasema: ‘’Elimu si ujifunzaji wa maarifa na data, lakini ni kujifunza kufikiri’’. Hii ni busara inayoniongoza katika kuandika makala haya leo’.
Mfumo wa elimu tuliorithi kwa wakoloni ni ule wa kukariri maarifa mengi iwezekanavyo, kisha kuyatoa hayo tuliyokariri katika mitihani.
Nakumbuka nilipomaliza mkataba wangu wa kufundisha chuoni huko Marekani nilirudi nchini, kisha nikapata nafasi ya kufundisha somo la falsafa na maadili katika chuo kimoja hapa nchini.
Wanafunzi wangu walikuwa wa ngazi ya uzamili na uzamivu, hivyo hao ni wanafunzi waliopitia shule kwa muda mrefu.
Katika siku za mwanzo za somo langu hilo, nilikaribisha maswali kutoka kwao. Mimi ni mwalimu ninayeamini kwamba wanafunzi wakiuliza maswali, basi wanaanza kuelewa kitu, na wanataka kujua.
Lakini wanafunzi wasipouliza maswali kuna shida mbili: kwanza, hawajaelewa au pili, sijafundisha vizuri. Hii ni kusema kwamba mwanafunzi anayeuliza maswali ndiye mwanafunzi anayestahili kuitwa mwanafunzi.
Turudi kwa maswali ya wanafunzi wangu niliowataja hapo juu. Swali lao kuu lililojitokeza mara kwa mara ni hili: mfumo wako wa mitihani ukoje? Hebu tuambie mifano ya maswali utakayouliza katika mitihani yako? Ilinionyesha wazi kwamba wanafunzi wangu walitamani wajue mitihani yangu itakuwaje na ni hoja gani hasa watapaswa kuzijua ili wafaulu mitihani.
Lengo langu la kufundisha falsafa na maadili kwa wanafunzi hao lilikuwa kuwakuza katika maadili na uadilifu, ili waweza kuwa watu waadilifu katika maisha yao. Hilo ndilo lilikuwa lengo langu, na naamini ndilo linapaswa kuwa lengo la elimu kwa ujumla. Hata hivyo, wanafunzi wangu walikuwa na lengo tofauti; walitaka niwasaidie na niwatayarishe katika kushinda mitihani nitakayowapa baadaye. Kushinda mitihani ndio lengo lao kuu, na ukiangalia mazingira ya elimu yetu, ndivyo mambo yalivyo.
Wanafunzi wanataka wapate maarifa kutoka kwa mwalimu, wayakariri, baadaye wayanukuu katika mitihani, washinde mitihani hiyo.
Huo ndio mfumo wa elimu tuliorithi kwa wakoloni. Ijapokuwa ni haki niongeze kuwa wakati wetu wa masomo ya msingi, darasa la kwanza hadi la nane, tulifundishwa pia ufundi kama vile kilimo, uashi, kuchomea, kuranda, na kuchora.
Hiyo ilikuwa elimu nzuri ya kutufundisha kufikiri pale anapofanya mazoezi hayo. Hilo ni jambo zuri tulilojifunza katika mfumo wa elimu wa wakati huo.
Ni jambo jema sana kwamba mfumo mpya wa elimu unaotayarishwa sasa unatia mkazo katika elimu ya ufundi.
Hata hivyo, elimu yetu ya sasa, na sehemu kubwa ya elimu inayopendekezwa, bado inatilia mkazo katika kukariri mambo na kuyanukuu kama yalivyo katika mitihani.
Tufanyeje?
Tunapaswa kufanya bidii ya makusudi kuwasaidia wanafunzi kufikiri, kutafakari na kubuni njia mbadala za kujifunza na kuielewa dunia hii.
Napendekeza hapa namna mojawapo ya kuwatayarisha wanafunzi wanaofikiri na wanaotafakari mambo kwa kina.
Kwanza tupate busara ya mjerumani mwanafalsafa mwingine, Martin Heidegger (1889-1976) aliyeandika hivi:
‘’Kuna elimu au mtazamo wa kuona kila kitu katika mstari ulionyooka, kwa mfano mtu anasoma kitabu au sura ya kitabu kuanzia mwanzo hadi mwisho, kisha kuendelea na sura nyingine, au kuishi kuanzia asubuhi hadi jioni bila kurudi nyuma kuona mtu umefanya nini.’’ Huu ni mtindo unaongalia mbele tu, mtindo wa kuamka asubuhi, unakunywa chai, unakwenda kazini, unarudi nyumbani, unakula, unalala. Hakuna kurudi nyuma kuangalia ulichokifanya.
Lakini ipo namna nyingine ya kuishi na kujifunza, ambayo Heidegger anasema na kufanya jambo na kisha kurudi nyuma kiakili kutathmini ulichokifanya, na kutafakari kuhusu ulichokifanya.
Mfano ni kusoma makala hii, ukaitafakari, ukaioanisha na maisha yako, hata ukarudi kuisoma mara ya pili.
Heidegger anasema huu mtindo wa maisha ya aina ya pili ndio uliotamalaki duniani na huo wa kwanza ni nadra.
Tafsiri rahisi ya hili ni kwamba watu wengi hatufikiri kwa kina, hatufikiri juu ya maisha yetu, tunasonga mbele kwa mbele bila kutazama nyuma.
Mtindo huu wa maisha haulei busara na hekima, ndio maana tunaona matatizo mengi katika siasa, uongozi, malezi ya watoto na hata katika elimu.
Hivyo pendekezo hapa ni kwamba elimu yetu ithamini mazoezi kama mijadala, ufundishaji kwa kutumia hadithi na kadhalika.
Mwalimu asiyeweza kufundisha mada fulani kama hadithi au asiyeweza kuoanisha mada fulani na maisha ya kila siku, hastahili kuwa darasani.
Nilipokuwa shule ya msingi na sekondari, tulikuwa na mijadala kila wiki. Tuliwaalika wanafunzi wa shule nyingine tukashindana katika mijadala mbalimbali. Kwa nini tusifanye hivyo sasa? Kwa nini tumejikita sana katika mitihani ya mtahiniwa kuchagua mojawapo ya jibu sahihi kati ya majibu manne? Ni lini mwanafunzi huyu atajifunza kufikiri? Uzoefu wangu huku mitaani ni kwamba wanafunzi wetu wa msingi na sekondari na hata wa chuo kikuu, si wepesi wa kufikiri, kutafakari, kubuni na kadhalika.
Nilimuuliza mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu: unaonaje juu ya madai ya Katiba mpya? Hakuwa na mawazo. Alisema hawafanyi siasa shuleni.
Nilisikitika sana. Hivi mwanafunzi huyu atashindanaje na mwanafunzi wa nchi jirani katika usaili wa kupata ajira ofisi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mfano?
Hebu ona hili lingine. Nilipokuwa nafundisha chuo hicho cha Tanzania nilichokitaja hapo juu, niliwaambia wanafunzi wangu (wa uzamili na uzamivu) kwamba katika mtihani unaofuata, wanarusiwa kuingia katika chumba cha mtihani wakiwa na vitabu na madaftari.
Wanafunzi walishtuka. Niliwaambia kwamba kama wasipotafakari juu ya yale tuliyojijunza darasani, kama hawawezi kuoanisha ya darasani na maisha ya kila siku, vitabu na madaftari hayo yasingefaa lolote.
Ni kama niliwaamsha usingizini. Nikaona macho na masikio yao yapo tayari kujifunza. Zaidi niliona kwamba wameanza kushirikisha mioyo yao na roho zao katika yale tuliyojifunza.
Hapa ndipo elimu inaibuka. Ni pale mwanafunzi anapoweza kufikiri na kutafakari kwa kina kuhusu kile anachojifunza, anapoanza kuoanisha maarifa ya shuleni na maisha ya kila siku.
Hii ndiyo elimu inayofaa kwa watoto wetu na taifa letu. Tujenge taifa la watu wanaofaidi moja kwa moja kutoka kile wajifunzacho darasani, taifa la watu wanaofikiri na kutafakari kwa kina. Hiyo ndiyo elimu anayoisema mwanafalsafa Einstein.