Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hii mechi ya Simba, Yanga sasa iangaliwe kivingine

Derby Kivingineeeee Hii mechi ya Simba, Yanga sasa iangaliwe kivingine

Sun, 30 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Jumapili iliyopita ilishuhudia sare ya bao 1-1 ya Yanga na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Kwa mwezi mzima, mchezo huo ulitanguliwa na mbwembwe na ubishi mtaani huku ukifunika mashindano ya kimataifa ambayo timu hizo zilikuwa zimechezwa wiki moja kabla.

Pambano la mahasimu ni mchezo baina ya timu zinazotokea katika eneo jiografia moja au nchi moja au katika mashindano yanayozishirikisha timu mbili zenye upinzani mkubwa.Neno Derby lina asili katika mashindano ya farasi wenye upinzani kwenye miaka ya 1870 katika mji wa Derby ulioko Derbyshire,Uingereza.

Katika mpira wa miguu timu huwa wapinzani kwa upinzani kukua kidogokidogo ukichochewa na mambo kadhaa zikiwemo tofauti za kidini,kisiasa,kipato na hata historian na utamaduni.

Wachezaji huja na kuondoka,walimu huja na kuondoka,viongozi huja na kuondoka na mashabiki huja na kuondoka lakini utani kati ya timu hizo ubaki pale pale.Upinzani huu huonekana dhahiri kwenye siku ya mchezo kati ya mahasimu hawa ambapo shughuli zote husimama kupisha mpambano huo. Hakuna mchezo wenye maana kwa klabu yoyote zaidi ya mchezo wa mahasimu au watani wa jadi.

Miongoni mwa mapambano ya mahasimu yenye umaarufu mkubwa duniani kwa sasa ni pamoja na Hispania, FC Barcelona v Real Madrid (El Clasico), Italia, AC Milan v Inter Milan (Derby della Maoninna),Scotland,Celtic v Rangers (The Old firm),Uingereza Manchester City v Manchester United (Manchester Derby),Manchester United V Liverpool (North West Derby),Arsenal v Totenham Hotspurs (North London Derby),Everton v Liverpool (Merseyside Derby),Misri, Al Ahly v Zamalek (Cairo Derby),Agentina,Boca Junior V River Plate (Superclasico),Ureno,Porto v S.L Benfica (O Classico). Orodha ni ndefu sana.

Tukiangalia pambano kati ya timu ya FC Barcelona na Real Madrid au El Clasico ni mpambano kati ya vilabu vilivyo vikubwa kabisa katika ligi ya nchi ya Hispania ijulikanayo kama La Liga. Upinzani huu umedumu kwa miaka zaidi ya 120. Real Madrid imeshinda mara nyingi zaidi .

Timu hizi zinatoka katika maeneo jiografia tofauti lakini upinzani wao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na ukweli kwamba vilabu hivi ndivyo vimetawala kwa kiasi kikubwa katika kuwania ubingwa wa nchi yao.

Kuna chembe za kisiasa katika upinzani huu kwani Barcelona inatokea katika jimbo la Catalonia ambalo limekuwa likitaka kujitenga na Hispania huku Madrid ikiwa upande wa mfumo unaopinga nchi kugawanywa.

Wachumi wanaliona pambano hili kama moja ya sekta ndani ya Hispania ambayo uchumi wake unakua zaidi ya uchumi wa taifa. Mpambano wa El Clasico ni chapa inayouzwa nje ya Hispania na Ulaya; ni chapa ya kimataifa.

Mtandao wa kimichezo wa Goal.com umetaja pambano la watani wa jadi wakiliita kwa kimombo Dar es Salaam Derby au Kariakoo Derby kuwa katika nafasi ya 5 kwa ukubwa barani Afrika. Mpambano huo wa watani wa jadi unawakimbiza kwa karibu mapambano mengine ya mahasimu katika nchi za Tunisia,Morocco, Afrika ya Kusini na Misri ( pambano la mahasimu la Cairo) lililo kileleni. Uwekezaji mkubwa na kuongezeka kwa timu ya Azam FC kama moja ya timu tatu zinazowania ubingwa kunaweza kuongeza ladha katika uhasimu wa kimpira huko mbeleni.

Pamoja na utani huu kuwa na miaka zaidi ya 80 lakini utani umeshamiri zaidi kuanzia miaka ya baada ya uhuru yaani miaka 60 iliyopita. Timu hizi zinatokea mitaa ya Msimbazi (Simba) na Twiga na Jangwani (Yanga) ambayo yote iko Kariakoo katika jiji la Dar Es Salaam.

Pamoja na kuwa na historia iliyoanzia kwenye siasa,pambano hili limeziacha nyuma historia hizi na kuwa utani wa mpira pekee. Hii pengine ndiyo imepelekea pambano hilikuwa la watani zaidi kuliko mahasimu. Haishangazi familia moja wanatoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kushangilia timu tofauti.

Waswahili wanasema kuwa kwa kawaida mtu hupenda Yanga na Simba kwanza kisha hupenda mpira wa miguu.

Niliuangalia mpambano wa juma lililopita kupitia runinga. Hii ilinipa nafasi ya kuangalia umati uliofurika kuanzia majukwaa maalum mpaka majukwaa ya kawaida. Kwa haraka niliweza kuona sura za watu waliotoka nje ya Tanzania wakitokea sehemu mbalimbali duniani. Na hii sasa imekuwa kawaida ingawa ni jambo kubwa kwa jicho la kiuchumi.

Licha ya kurushwa ‘live’ bado hilo halizuii watu zaidi ya elfu 50 kwenda uwanjani. Siku za nyuma nilitembelea baadhi ya miji mikubwa ulaya;wao walizima runinga ikiwa timu za mji mmoja zinapambana kwa maana hawakuwa na uhakika wa kupata watu wa kuujaza uwanja ikiwa mchezo ungekuwa mubashara. Kwa pambano la watani wa jadi la Tanzania ni kinyume kabisa.Ni tukio lenye mizizi haswa mioyoni mwa watu.

Naweza kusema kwamba kwa sasa mpambano wa watani wa jadiumefikia kiwango ambacho unaweza kuingizwa kwenye kifurushi cha mtalii (tour package). Mathalani mtalii anatua Kilimanjaro kuona Mlima Kilimanjaro na mbuga za kaskazini,kisha anaelekea Dar Es Salaam kuangalia mchezo wa watani wa jadi na kutoka hapo anaenda kwenye visiwa vya Mafia,Pemba au Zanzibar. Tiketi za mashirika ya ndege hata meli zinaweza kuunganishwa na tiketi ya kuingia uwanjani na hivyo kuongeza wageni na kuitangaza derby ya Dar Es Salaam.

Utalii wa matukio kwa sasa ni utalii mkubwa kuliko utalii wa mazingira na maumbile. Rafiki yangu mmoja raia wa Argentina anayefanya kazi Doha, Qatar husafiri kila mwaka na familia yake kushuhudia pambano la Superclasico kati ya Boca Junior na River Plate za jijini Buenos Aires.ambapo yeye na mke wake wamegawanyika katika upenzi wao kwa timu hizi.Ni kiasi kikubwa cha fedha kufanya safari hiyo lakini mwenye mapenzi na kitu hajali gharama. Miji na majiji yanajitangaza na kuingiza watalii na kipato kupitia matukio hasa ya michezo na utamaduni.

Ni wakati sasa wa kuufanyia promosheni ukachezwa hata nje ya Dar Es Salaam kwani uzoefu unaonyesha ya kuwa mashabiki wa hizi timu wametapakaa kote Afrika ya Mashariki na Kati. Uzoefu wa hapa ndani umeonyesha kwamba hizi timu zimekuwa ni kivutio bila kujali zimekutana Dar ES Salaam,Zanzibar, Mwanza, Arusha hata Kigoma.

Kwa kuupeleka nje ya Dar Es Salaam,mchezo huu utakuwa unaongezewa thamani kama chapa na kupata mashabiki wapya.Pamoja na mapato yanayotokana na viingilio,haki za runinga,mauzo ya jezi na bidhaa nyingine za vilabu,mchezo huu huingiza fedha kwenye nyumba za wageni,kumbi za starehe na kadhalika. Pia siku ya mchezo huu hutoa ajira za moja kwa moja kwa wahudumu wa mchezo na hata wasafirishaji wakubwa kwa wadogo kama bodaboda. Ni muda sasa mamlaka za utalii , jiji na sekta binafsi kuliona pambano la watani wa jadi kama fursa katika tukio la kila mwaka.

Tukio ambalo wanaweza kushirikiana na mamlaka za michezo kuliuza hili lichangie zaidi pato la mtu mmoja mmoja,taasisi na taifa kwa jumla. Michezo na matukio ni sehemu muhimu ya utalii wa kisasa. Mchezo wa watani wa jadi ni tukio bidhaa ambayo imeshakamilika. Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa TFF.

Columnist: Mwanaspoti