Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Heri wapatanishi

MENG.webp Heri wapatanishi

Thu, 30 Apr 2020 Chanzo:

WAKATI Dk. Reginald Mengi anaanza kushiriki shughuli za kijamii kwa karibu miaka ya 1990, moja ya maeneo yaliyokuwa yanaleta wasiwasi ni chokochoko za kidini.

Kulikuwa na mfumuko wa mihadhara na vyombo vya habari kuelezea kwa kina kwanini imani mojawapo kubwa siyo sahihi. Kwa miaka ya kwanza (mwisho wa miaka ya 1980 hadi kufikia 1993 hivi) waliokuwa wanashambuliwa walibaki wamepigwa na butwaa, hawana la kujibu.

Chokochoko hiyo ingefaulu zaidi endapo wazungumzaji wakuu nchini wangeelekea mwelekeo huo, lakini wengi walikataa, kutokana na jadi ya kutobaguana kidini hapa nchini.

Dk. Mengi alisaidia kujenga mwelekeo huo chanya katika kampeni za kuchangia vikundi tofauti, siyo tu vikundi vya dini kuwa anawasaidia hata wasio wa dini yake, ila kujenga hulka ya kujali kwa jumla.

Harambee za mahitaji ya mashule, zahanati ya makundi tofauti ya kiimani, na hata nyumba za ibada, zilikuwa ni jambo la kawaida kwake, kutoa picha sahihi ya mshikamano.

Wakati anafariki dunia, wasemaji wa pande zote za imani walikiri alikuwa mtu aliyejali watu bila kuangalia vianzio vya kidini, rangi, kabila au chochote kingine, nje ya kufuatilia au kuwezesha mahitaji yanayogusa kundi kubwa la watu.

Ni mwelekeo wa kipekee ambao alikuwa nao kama mtu aliyefaulu sana katika jitihada za kibiashara, kwa kuwa kwa kawaida matajiri wanakuwa na maeneo yao ya kijamii wanayohusika nayo, tena ni kama wakipenda. Matajiri wengi wanaishi tu na familia zao na hawasikiki kokote, hawaguswi na chochote, wanaogopa usumbufu.

Ina maana kuwa kujali makundi tofauti ya watu ilikuwa ni uthubutu wa aina yake, kwa kuwa mahusiano hayo yalikuwa na sura ya ndoa, kwa maana ile ya ‘ndoa, ndoana’ kuwa kuingia ni rahisi ila kutoka ni ‘kasheshe.’ Ukishajitambulisha na kundi hili au lile la wananchi na wakajenga imani kuwa utakuwa pamoja nao, jambo hilo ni budi liendelee hadi tamati yake.

Haiwezi kufika mahali ukatangaza kuwa sina tena hamu au nia ya kuangalia kundi hili au lile; jambo ambalo halitamkwi hadharani.

Hivyo kuna kanuni nyingine ya maisha iliyotawala maisha ya Dk. Mengi ambayo kwa yakini alikuwa anaifahamu, na siyo ajabu aliwaeleza baadhi ya waliokuwa karibu naye kimaisha.

Ni ile inayosema ‘atakayekuwa wa kwanza miongoni mwenu, atakuwa mtumishi wenu,’ hivyo katika kushirikiana na makundi makubwa ya watu aliweka kando hulka ya kibiashara ambako una uwezo wa kufanya ‘maamuzi magumu.’ Unapokuwa unashirikiana na makundi ya watu maamuzi magumu ni yale unayojichukulia wewe mwenyewe, kwa mfano ni fungu gani la fedha litakuwa linatosha, au kuridhisha, kwa mahitaji fulani, na si kukataa.

Unaweza kuona kiwango cha ustadi wa kisaikolojia wa Dk. Mengi, yaani huku ni ‘ruthless businessman,’ kwa maana ya kuwa na macho makavu kuona udhaifu, hujuma au chochote kingine katika shughuli zake maridhawa, halafu avae joho lingine, ‘akachunge kondoo.’

Ni hulka nyingine ya maisha ambayo hata kama hajaizungumzia ilimwingia akilini akiwa kijana, na siyo ajabu akiwa mtoto wa kipaimara, kwa lile swali kama Petro anampenda Masihi, akajibu mara mbili kwa maumivu kidogo, halafu akaambiwa kama ni hivyo, basi ‘chunga kondoo zangu.’

Kwa tafsiri ya kina ya amri hiyo, ‘kuchunga’ siyo kutoa msaada wa hapa na pale ila pale inapowezekana kuwahakikisha watu matumaini katika maisha.

Ni tofauti na dhana ya ‘kuondoa umaskini’ kwa kuwa huo ni ‘mfupa uliomshinda fisi,’ ila kutoa mwanga, na nyenzo za hapa na pale, ili watu waweze kuinua maisha yao wenyewe.

Siyo ajabu kuwa Tanzania haikubahatika kuwa na mtu aliyefikia uelewa wa dhana au masuala yote hayo ya kiimani, ambayo kimaisha ni ya kisaikolojia, lakini yana msingi katika malezi na mafundisho.

Ni dhana zinazokaa tu kichwani na kufanya kazi, na siyo ajabu ukiongea naye hata asizikumbuke kwa kuwa ni zamani sana alifikia mwelekeo huo, hivyo inakuwa tu hulka au tabia, na siyo tena ‘mtiririko wa hoja…’

Katika mtazamo wa bingwa wa saikolojia wa Uswisi aitwaye Sigmund Freud, ambaye aliandika vitabu vyake miaka ya 1900 hadi miaka ya 1930 karne iliyopita, aliweka mfumo wa kutambua ufahamu wa mtu katika ngazi tatu.

Moja imejificha kabisa katika ufahamu wa mtu na yeye mwenyewe anaweza kuwa hata hawazi usahihi wa hiki au kile kwani imeshajijenga na kutawala kwa ndani. Ila kuna maeneo mawili ambayo yako wazi, lile la ufahamu wa kawada ambako hasa ndiyo tunaishii nalo, halafu eneo la amri ya aima fulani juu ya hili eneo la kawaida.

Hii ni pamoja na woga wa kawaida wa kutii amri za nchi, au kanuni za biashara ambazo inabidi zitiliwe mkazo, kanuni za malezi zisizoweza katu kupuuziwa, na kadhalika.

Ndiyo maana watu wanakuwa na hulka tofauti katika maisha, mara nyingine baadhi ya watu wanashangaa, na kwa jumla yako maeneo ya hulka za kawaida zinazounganisha watu wengi zaidi.

Dk.Mengi hakuwa katika kundi hili la hulka za kawaida zinazotawala katika jamii, vinginevyo asingefanya yote ambayo aliyafanya, hata nusu yake au robo tu asingefika bila kuwa na msingi wa imani usiotetereka. Ila maongezi yake hayakuwa hayo, alichokuwa anajadili ni kile kilichoko mezani na nini kinahitajiwa; iweje ajali jambo hilo lilikuwa suala tofauti.

Columnist: