Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Heri tungekuwa tunajadili vipindi vya urais

8f205908ce207a22e326336818857d06 Heri tungekuwa tunajadili vipindi vya urais

Wed, 16 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NILIMSIKIA kiongozi mmoja wa dini akisema kwamba tatizo letu kubwa wanadamu, ni kutothamini neema tunazopata. Akasema hatuthamini neema nyingi tunazopewa na Mungu na hata tunazofanyiwa au kupewa na wanadamu wenzetu.

Akasema wengi Mungu ametupa neema ambazo si rahisi kuzihesabu, lakini chache miongoni mwa hizo, ni uwezo wa kuona, kusikia, kunusa, kutembea, kula na kufurahia chakula, kuzungumza, kuvuta hewa… ni nyingi mno.

Akatafakarisha akisema: “Hebu fikiria, kama Mungu angekuumba huku pua zikiwa zimetazama juu halafu mara paap, mvua kubwa ikanyesha huku ukiwa mahala ambapo hakuna sehemu ya kujikinga!” Kwamba, kuna wakati Mungu ‘anaminya’ kidogo neema zake kama vile mtu kushindwa kula, kushindwa kuvuta hewa au hata kujisaidia hadi wengine wanalazimika kuwekewa mipira ili kujisaidia au vifaa vya kuvuta hewa, lakini wengi wetu hakuna tunachojifunza kwa hayo! Tunaendelea kukaidi Amri za Mungu ‘kama kawa’.

Tunafanya hayo huku maandiko yakisema kwamba Mungu ametuumba na kutumwagia hizi neema lukuki hapa duniani kwa lengo moja kubwa; kumwabudu yeye kwa maana ya kufanya aliyotuamrisha na kuacha aliyotukataza, basi! Yule kiongozi akazidi kusema kwamba, mbali na kukufuru neema za Mwenyezi Mungu, huwa tunakufuru hata za binadamu wenzetu.

Akatolea mfano kwa mwanaume aliyempenda msichana kigoli, akamstarehesha kwa kipindi kirefu baada ya kumuoa, akimpikia na kumzalia watoto.

Hata hivyo, huku mtu huyo akiwa kachangia kumzeesha, unafikia wakati mwanaume huyu anasahau kabisa neema alizopata kwa mwanamke huyo, anaamua kutafuta kigoli mwingine huku akimwona huyu kama takataka! Akasema:

“Mara nyingi wanadamu hukumbuka neema pale tu, wanapozikosa. Wanapokuwa nazo mkononi wanajisahau.” “Mtu unapokuwa na mikono yote miwili, kwa mfano, hujui kuwa hiyo ni neema kubwa, kakini siku mikono ikikatika, ndipo anagundua umuhimu wa neema hiyo ya mikono!” Wahenga walisema: Ng’ombe hajui umuhimu wa mkia wake, hadi unapokatika.” Kiongozi huyo wa kiroho akazidi kusema:

“Unapokuwa na mke au mume, unamzoea kiasi cha kudhani uwepo wake ni kawaida tu sawa na asipokuwepo, lakini siku akiondoka au kufariki dunia, ndipo unagundua kumbe alikuwa ni neema kubwa kwako!” Nilijaribu kuyapeleka maneno ya kiongozi huyo wa dini kwa ndugu zetu wa Libya waliosahau neema kubwa ya kuwa na kiongozi mwenye maono, Kanali Muammar Gaddafi aliyeifanya nchi yao kuwa ‘ya maziwa na asali.’

Wakaanza ‘kucheza ngoma ya Watu wa Magharibi’ walioamua kumpa jina baya la dikteta, king’ang’anizi wa madaraka, mvurugaji wa demokrasia na mengine mengi, kumbe mabepari hao wa Magharibi wanamwona Gaddafi kuwa ni mtu anayewaziba kupora mali za Libya! Bila shaka vizazi vingi vya Libya havitasahau ukweli kwamba, Gaddafi alikuwa neema kubwa kwao, lakini kwa kuamini kila wanalolisikia kutoka kwa watu wa Magharibi, wakaichezea.

Ukija hapa Tanzania, kila mkoa ukienda, utakutana na simulizi kama hizi za Baraka Mina ambaye ameandika kwenye mtandao wa Jamii Forum kwamba kwa namna Rais John Magufuli alivyoupaisha Mkoa wa Shinyanga, atashangaa sana kama hatazoa kura zote za mkoa huo.

Mina katika andiko lake anasema: “Waingereza wanasema kuona ni kuamini. Nimefika mkoani Shinyanga na kuona mafanikio mengi.” Kisha mtu huyo anataja mafanikio hayo yanayomfanya JPM achukue kura zote mkoani humo kuwa ni pamoja na ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Anasema ukarabati huo umepanua wigo wa utoaji wa huduma bora na za kisasa za afya katika mkoa huo. Pili, anasema ni kuweka taa za umeme jua katika barabara za halmashauri za Shinyanga, na hivyo kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara usiku.

Mengine anataja kuwa ni ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 35,000 za mazao, kuboresha makazi ya wazee Kolandoto kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuimarisha barabara katika Manispaa ya Shinyanga kwa kiwango cha lami.

Anazidi kuyataja mengine kuwa ni pamoja na kurejeshwa kwa mali za vyama vya ushirika zilizokuwa zimeuzwa kiholela na nyingine kuporwa zikiwemo nyumba za makazi, maghala, viwanda na viwanja; kuhamasisha ufugaji wa samaki katika Mkoa wa Shinyanga ambapo mabwawa 103 yamechimbwa na kujengwa kwa machinjio ya kisasa.

Mina anazidi kuorodhesha neema ambazo JPM amewafanyia wana Shinyanga katika kipindi chake cha miaka mitano kuwa ni pamoja na kutengwa kwa maeneo rasmi kwa ajili ya wajasiriamali, wakiwemo mama lishe na wauza mboga kufanyia biashara.

Mengine ni ujenzi wa mabwawa ulioanza kutekelezwa, ikiwemo bwawa la Seke Ididi ili kutatua kero ya maji na kuanzishwa kwa vituo vya huduma ya mkono kwa mkono (One stop centres) ili kulinda haki za wanawake katika Mkoa wa Shinyanga.

Simulizi kama hizo za Mina ndizo utazisikia kila mkoa ukienda; iwe Arusha, Mbeya, Mara, Tanga, Lindi na kwingineko bila kutaja miradi mkubwa ya kitaifa kama ujenzi wa reli ya kisasa, bwawa la kuzalisha umeme wa uhakika na kadhalika.

Hapa tunamzungumzia Magufuli aliyepambana vilivyo na saratani ya rushwa na ufisadi ambayo imekuwa ikizitesa nchi nyingi za Afrika kiasi cha Waafrika wenzetu wengi kutuonea wivu kuwa na rais huyu.

Mwaka 2017, nilibahatika kuwa miongoni mwa waandishi wa habari 35 kutoka Afrika waliozuru China kwa programu maalumu. Ingawa JPM alikuwa na miaka miwili tu ofisini, niliona namna waandishi wa mataifa mengine ya Afrika walivyoonekana kumkubali kiasi cha kunikera kwa maswali na kutaka kusikiliza namna kiongozi huyu anavyoongoza nchi.

Walitamani angezaliwa katika nchi zao. Sisemi kwamba Magufuli ni malaika na wala sisemi hakuna Watanzania wengine wanaoweza kufanya mambo kama yeye, lakini kwa aliyoyafanya bado anakuwa chaguo muhimu na la pekee angalau kwa sasa la Watanzania, mintarafu ukiangalia sura zilizojitokeza kupambana naye na jinsi marais wengine wa Afrika walivyo.

Niseme tu kwamba kwa sura zinazowania urais na kwa kuzingatia kazi aliyoifanya Magufuli ambayo kwa Watanzania si ya kusimuliwa, kuendelea kujadili kama kuna mtu mwingine wa kumpa urais zaidi ya Magufuli ni kupotezeana muda! Ninaungana na Profesa PLO Lumumba wa Kenya ambaye amekuwa akisema kuna haja sasa ya kuangalia upya hii demokrasia ya kuiga nje kwa sababu wakati mwingine haiendani na hali zetu Afrika.

Profesa anasema hata tunapokuwa na waangalizi wa ndani kwenye uchaguzi wetu, mara nyingi hatuaminiani badala yake tunasubiri kusikia waangalizi wa Ulaya watasema nini na ndicho tutakachoamini zaidi wakati hata sisi tuna macho, tunaona kila kitu, tena na katika mazingira yetu! Ni katika mtazamo huo, sina hakika kama nchi kama Libya kwa jinsi Gaddafi alivyokuwa akiineemesha ilikuwa na sababu yoyote ya kufanya uchaguzi au kuwasikiliza vibaraka.

Wakati nikishangaa kuona namna mwaka huu walivyojitokeza watu wengi kutaka urais kwa maana ya kupambana na kiongozi ‘anayetisha kwa viwango vikubwa kwa ubora,’ binafsi nimekuwa ninawashangaa wanaoonesha hofu yoyote dhidi ya hawa waliojitokeza kupambana na ‘chuma cha pua.

’ Ninaamini wataishia tu kupiga kelele kwa sababu hata ndege angani wanaona Tanzania inavyopaa kwa kila nyanja. Nadhani wengine wamejitokeza kutengeneza tu CV kwamba ‘na mimi niligombea urais nikipambana na Rais bora Afrika kwa sasa!’

Kutokana na kazi nzuri ya JPM, nilishafikiria kuacha hata kuzungumzia wapinzani ambao hawana hoja makini kabisa baada ya Magufuli kufilisi hoja zao zote kutokana na utendaji uliotukuka.

Hofu yangu imekuwa ni mustakabali wa nchi yetu dhidi ya mabeberu. Hata katika uchaguzi huu, hofu yangu ni kama mabeberu watawatumia baadhi ya wagombea kutuletea chokochoko na vurugu ili tupoteze amani, utulivu na umoja wetu.

Mabeberu siku zote hukerwa na amani ya nchi yenye rasilimali nyingi kama ilivyo Tanzania. Hukerwa zaidi kunapokuwa na kiongozi anayejitambua kama JPM kwa sababu ubeberu ukikosa mahala pa kunyonya na kupora rasilimali, utatoweka.

Hiyo ndiyo hofu yangu kubwa lakini siyo kwamba kuna mgombea mwenye ubavu hata wa bawa la nzi kupambana na chuma cha pua, JPM. Tumwache Magufuli aendelee kutumia muda huu wa kampeni kukutana na Watanzania na kugusia mafanikio yaliyofikiwa na kisha kueleza yale aliyopanga kutufanyia katika miaka mingine mitano kupitia ilani ya uchaguzi ya chama chake.

Sisi wengine badala ya kutumia muda huu adhimu eti kujadili nani anafaa kuwa rais wetu wakati anajulikana, heri tujadili namna tutakavyopambana na ubeberu kwa sababu ndilo tishio letu kubwa kwa au tujadili suala la kumwongezea JPM uongozi baada ya miaka mingine mitano.

Umuhimu wa kujadili kama kuna haja ya kubadili katiba ili tuendelee kuvuna neema anazoleta Magufuli umenijia baada ya kuangalia sura zilizosimamishwa kupambana naye. Kimsingi hali ndiyo hii, bado tunamhitaji Magufuli hata baada ya miaka mitano ijayo.

Columnist: habarileo.co.tz