Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Haya ndiyo madhara ya pombe kwa wanasoka

Pombe Wanasoka Haya ndiyo madhara ya pombe kwa wanasoka

Thu, 27 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tunapozungumzia afya ya binadamu, basi ni jambo kubwa na la kuzingatia katika utendaji kazi wake na kulilinda. Binadamu yeyote asipokuwa na afya njema basi hata ufanisi wake wa kazi unakuwa mdogo iwe nyumbani ama ofisini kwake.

Si jambo geni mchezaji kupata changamoto la kiafya awapo sehemu yake ya kazi iwe kuumia, kuumwa ama kupoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa kujikumbusha kidogo miaka ya hivi karibu hususan kwenye soka nchini yamewahi kutokea matukio makubwa kwa wachezaji yaliyosababisha vifo ukiachana na majeraha yanayonekana kwa mchezaji ama wachezaji ni kama kitu cha kawaida.

Miaka kadhaa nyuma kwenye soka lilitokea tukio la kushtua wanamichezo wengi nchini pengine hata nchi jirani baada ya kutokea kifo cha mchezaji wa timu ya vijana ya Mbao FC (U20), Khalfan Ismail timu hiyo ilipokuwa ikicheza na Mwadui FC mashindano ya vijana kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Kifo cha mchezaji huyo kilitokeo baada ya kugongana na beki wa Mwadui kwa bahati mbaya.

Aliwahishwa Hospitali ya Rufaa ya Kagera, hata hivyo alipofikishwa madaktari walisema alifari dunia pale pale uwanjani.

Mwaka huu, yametokea matukio yanayofanana na hilo mara mbili, awali ni mchezaji wa timu ya vijana U17 ya Singida Big Stars, Mohamed Banda, aliyefariki dunia wakati wanafanya mazoezi Uwanja wa Magereza mjini Singida, Januari 19. Banda alipoteza maisha alipofikishwa hospitali ya Mkoa wa Singida baada ya kugongana kichwani na mchezaji mwenzake.

Idd Mobby, alikuwa mchezaji wa Mtibwa Sugar, alifariki Machi, taarifa zake zilitolewa kuwa alianza kuumwa kichwa wakati anafanya mazoezi binafsi ya kukimbia barabarani na kukaa chini ndipo alipowahishwa hospitali kupata huduma.

Baada ya kuona hali yake inaendelea kuwa mbaya zaidi alipelekwa Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo Dodoma ambako mauti yalimpata akiwa anaendelea na matibabu, ilielezwa sababu ya kifo chake ni mshtuko wa moyo (presha).

Uwepo wa matukio hayo ambayo mengine hutokea ghafla na mengine huenda ni afya ya mchezaji husika kutokuwa imara tangu awali, lakini bila kugundua mapema.

Kutokana na changamoto hizo kutokea kwa wachezaji, Mwanaspoti katika makala haya limezungumza na wataalamu wa afya za binadamu (madaktari), kupitia Chama cha Madaktari wa michezo nchini (TASMA), wataalamu wa lishe, wataalamu wa viungo ambao wamezungumzia mambo mbalimbali yanayoweza kuchangia changamoto za kiafya kwa wachezaji na nini kifanyike kwa wachezaji wote kabla ya kusajiliwa na baada ya usajili.

HAWA HAPA TASMA

Tanzania inashirikisha michezo mbalimbali na kwa mujibu wa sheria za Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ni lazima vyama vyote ama klabu kuhakikisha wanakuwa na madaktari ambao wanatambulika na TASMA.

Hiyo ikiwa na lengo la kuhakikisha afya za wachezaji na wale wanaozunguka maeneo ya michezo kuwa salama pale wanapopata changamoto ya kiafya.

Hata hivyo, imebainika TASMA haina ushirikiano wa moja kwa moja na Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Soka Tanzania ambayo ipo chini ya Dr Limbanga.

Katika mahojiano maalumu ambayo yalifanywa na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa TASMA, Dr Sufian Juma anaeleza mambo mbalimbali juu ya afya za wachezaji wa michezo yote.

"TASMA tuna wataalamu wengi yaani kila mkoa wapo, tatizo ni namna ya kuwatumia, kwani kuna vyama vingine huwa wanajitafutia wataalamu wao ambao hawapiti kwetu kuwathibitisha kama ilivyoelekezwa na BMT.

"TASMA inasimamia michezo yote na siyo soka pekee, lakini kwenye soka inazungumzwa kwa vile ndiyo mchezo pendwa wa watu wengi ulimwenguni, huku kwenye soka tunapaswa kushirikiana kwa karibu na Kamati ya Tiba ya TFF, hata hivyo, jambo hilo halifanyiki ingawa mwaka jana kwenye mkutano mkuu tulilieleza ila hakuna mabadiliko yoyote.

“Ni jambo ambalo tunaona kabisa halizingatiwi na tunashindwa kufuatilia kwa karibu sana tatizo likitokea maana hatushirikishwi.

"Hiki chama kinamhusu daktari yeyote hata wale waliopo hospitali na huwa tufanya kozi mbalimbali kwa wataalamu wetu kutoka Bara na Visiwani, hivyo mwanachama sio lazima awe kwenye timu."

Kamati ya Tiba ya TFF ina wajumbe saba, sisi ndiyo tunapaswa kuwapelekea majina ya madaktari waliothibitishwa, yaani ni lazima watuulize sisi maana tuna vigezo vyetu vya kumfanya mtu kuwa kwenye nafasi hiyo na itasaidia, ingawa tumeona hivi karibuni wametoa waraka wa kutaka viongozi wa klabu kupeleka wasifu wa madaktari wao.

"Lakini haitoshi kuthibitisha madaktari tu pia wataalamu wa viungo waliothibitishwa taaluma zao maana ni watu wanaotegemeana kwenye timu, cha ajabu ukichunguza sana kuna timu mchezaji anaweza kuumia lakini daktari akashindwa hata kumshona jeraha lake, ni tatizo," anasema Dk Sufian

MADAKTARI WALIOTHIBITISHWA

Kwenye Ligi Kuu Bara kuna timu 16, hivyo kuna madaktari 16 lakini timu zingine zimeajiri hadi wataalamu wa viungo kulingana na uwezo wao wa uchumi ulivyo.

Dr Sufian anasema sifa ambazo madaktari wao hawajathibishwa na chama huku akidai huenda uthibitisho wao upo kwenye Kamati ya Tiba ya TFF.

Madaktari waliothibitishwa ni Shaaban Shija (Singida Big Stars), Mwanandi Mwankemwa (Azam FC), Abdallah Ramadhan Chuma (Geita Gold), Shindika Shija (Kagera Sugar), Hilary Paul (Namungo), Julius Njugilo (Ihefu), Sisho Chuma (KMC), Jaffary Vumbi (Tanzania Prisons), Richard Yomba (Polisi Tanzania) na Edwin Kagabo wa Simba.

Ambao hawajathibitisha TASMA kwa mujibu wa Dr Sufian ni Lawlens Mushi (Mtibwa Sugar), Stanley Kayombo (Mbeya City), Francis Mganga (Coastal Union), Juma Kiswagala (Dodoma Jiji), Simon Sugule (Ruvu Shooting) na Moses Etutu (Yanga).

"Kama Simba wao wametutumia wasifu wote wa wataalamu wao wa tiba kwenye timu yao, lakini hao wengine pengine wamethibitishwa Kamati ya Tiba ya TFF huku kwetu hatujawathibitisha. Huenda kamati hiyo baadaye itaamua kutushirikisha maana TASMA inatakiwa kufuatilia hatua kwa hatua juu ya madaktari wao huko waliko kujua utendaji wao wa kazi.

"Naendelea kusisitiza juu ya TFF ili kupata wataalamu wa tiba ya binadamu wanapaswa kuwasiliana na TASMA pia Ligi ya Champioship, First League nako waweke msisitizo kuwa kila timu iajiri daktari aliyesomea tiba za binadamu, tunafahamu kuna gharama za kulipa madaktari lakini ni vyema kuingia gharama maana utaokoa maisha ya watu," anasema.

VIONGOZI WAIJIBU TASMA

Kwa upande wa klabu ambazo zimeelezwa madaktari wao hawajathibitishwa na TASMA imekuwa tofauti kwani wameliambia Mwanaspoti wamethibitishwa na chama hicho ila msisitizo wa TASMA ni bado hadi sasa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakar anasema daktari wao, Lawlens Mushi amesajiliwa rasmi na chama hicho huku akibainisha kozi yake ya mwisho aliyosoma ni ya Januari 3 hadi 7 mwaka jana, jijini Dar es Salaam, hata hivyo TASMA imeeleza mwezi ujao (Aprili), ndipo wataanza kufanya kozi za kukumbusha.

"Kwanza umenishangaza kwa sababu sisi tumefuata taratibu zote na hatuwezi kuwa na daktari ambaye hajakidhi vigezo muhimu vinavyohitajika hivyo tutalifuatilia hili ili kujua kilichosababisha wasiwepo huko ni kipi."

Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omary Ayoub anasema daktari wao, Francis Mganga ni miongoni mwa waliosajiliwa hivyo huenda wahusika hawakuliorodhesha jina hilo ingawa wana Email (Barua Pepe) ya uthibitisho waliyotuma.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe anasema wao ni waumini kwa kutii sheria na taratibu zilizowekwa hivyo daktari wao, Stanley Kayombo amesajiliwa ila huenda wahusika wamesahau kuingiza jina lake kwenye mfumo.

POMBE CHIPS MARUFUKU

Wataalamu wa lishe na chakula nao wamezungumza namna ambavyo lishe inachangia kwa kiasi kikubwa afya bora ama mbovu kwa wachezaji, nini wanapaswa kutumia na kipi hakiwafai.

Walbert Mgeni, ambaye ni Afisa Lishe na Utafiti nchini anazungumzia kwa kina lishe bora kwa wachezaji ili kulinda afya zao; "Kati ya makundi matano ya vyakula, mchezaji anapaswa kuwa makini nayo sana kwa ajili ya kuwa na afya bora kwani ni watu wanaotumia nguvu sana.

"Mwanamichezo anatakiwa kutumia vyakula vitakavyompa nguvu na stamina kwenye mwili wake kama vyakula aina ya nafaka na mizizi ambavyo ndani yake unavikuta vyakula aina ya ndizi mbichi (zipikwe), viazi mviringo, viazi vitamu, magimbi na vinginevyo.

Kwenye nafaka unavikuta vyakula kama mchele, mahindi, mtama, uwele na vingine vinavyofanana na hivyo, pia vyakula vyenye asili ya nyama haijalishia ya aina gani na vile kama kunde, maharage, njegere, njugu na vifananavyo na hivyo kwa ajili ya kumsaidia kujenga misuli," anasema na kuendelea;

"Kuna mwaka alikuja Didier Drogba, watu walimshangaa sana alipokuwa anakula kuku mzima lakini hivyo ndivyo inavyotakiwa kwa mwanamichezo maana anatumia nguvu nyingi, hivyo lazima ajenge mwili na kutengeneza stamina.

"Lakini anatakiwa kula matunda kwa wingi na mbogamboga ili mwili wake usipate maradhi, pia aepuke utumiaji wa vyakula vyenye mafuta sana na sukari (asitumie sana), hiyo ni kuepusha matatizo ya moyo, presha na sukari."

Columnist: Mwanaspoti