Ligi zimesimama kwa muda baada ya kuchezwa kwa mechi chache ili kupisha kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa.
Hapa nchini, ligi imechezwa raundi mbili huku Yanga ikiwa kileleni ikikusanya pointi sita kama ilizonazo Azam FC na Simba japokuwa zinatofautiana kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kuna baadhi ya wachezaji wameshindwa kucheza mechi hizo za awali, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuwa majeruhi. Wapo wengine walioitwa timu za taifa, lakini wakiwa na hali ya majeraha na wamepata nafuu kidogo na kuanza kuungana na wenzao mazoezi mfano Henock Inonga ambaye aliitwa Timu ya Taifa ya DR Congo.
Pia, kuna wale ambao wanaendelea kupasha mazoezi mepesi na wenzao, wakitoka katika hali ya majeraha makubwa akiwamo kipa Aishi Manula ambaye aliumia Aprili kwenye mechi ya robo fainali ya ASFC.
Mbali na wachezaji hao lakini kuna wengine ambao wamekuwa wakitumiwa na timu zao huku wakiwa na maumivu wakati mwingine kwa kuchomwa sindano au kupewa dawa za kutumiza maumivu. Ni kawaida kwa mwanasoka kwa hiyari yake akawa na majeraha yanayoleta maumivu lakini akaamua kucheza na zaidi anaweza akatumia dawa za maumivu na kucheza.
Dawa hizi huwaondolea maumivu kwa muda tu, lakini si kuponya jeraha au kupunguza ukubwa wa jeraha. Leo nitawapa ufahamu wa mambo mawili muhimu kwa wachezaji yaani madhara ya kucheza na maumivu na utumiaji wa dawa za maumivu kiholela.
USIKUBALI KUCHEZA NA MAUMIVU
Kucheza mchezo ukiwa na maumivu ni jambo ambalo sio sahihi kiafya kwani kunaongeza ukubwa wa tatizo. Jeraha linapotoneswa mara kwa mara ni chanzo cha kujijeruhi upya na hivyo kuchelewa kupona.
Maumivu kwa mwanamichezo aliye majeraha ni ishara kuwa jeraha bado halijapona vizuri.
Maumivu yanaweza kuwa ya kawaida, ya kati na makali. Yanaweza kuwa ni majeraha ya mfupa, misuli, mishipa ya fahamu na tishu nyingine za mwilini.
Panapotokea jeraha mwili hujibu mapigo kwa kutuma askari mwili kwa ajili ya kukarabati neneo hilo. Mlipuko wa kinga ya mwili ndio chanzo cha mtu kuhisi maumivu, kufa ganzi, kuvimba, kupata joto na kubadilika rangi ya ngozi. Hali hii ndio kitabibu huitwa Inflammation.
Wanamichezo ambao wako nje ya uwanja kwa kuwa majeraha hudhani kuwa maumivu yanapopungua tu wamepona na wako fiti kuanza kucheza. Pasipo kufahamu kuwa majeraha bado hayajapona vizuri.
Mara yingine misuli ya mwili ya mwanamichezo inapotumika sana huambatana na vimichubuko vya ndani kwa ndani ambavyo uwapo wa maumivu ni kama ombi la mwili kuhitaji kupumzika ili kupona kabisa.
Unapobainika na wataalamu wa tiba za michezo kuwa una majeraha ya mfupa na nyuzi ngumu za tendon na ligamenti, fahamu kuwa itachukua muda kupona kabisa na kurudi mchezoni.
Mwanamichezo anahitajika kujifahamu na kujidhibiti maumivu yake ikiwamo kujua yanachokozwa na mambo gani, je, yanaanzaje wakati wakuanza, katikati au mwishoni baada ya mazoezi/mchezo?
Vema pia kufahamu kuwa maumivu yanauma unapominywa au yanakuwepo tu yenyewe, je yanasambaa au yanaibukia sehemu nyingine. Kila tabia ya maumivu ya mwili hutoa picha ya chanzo chake na ukubwa wake.
Wataalamu wa tiba za afya za michezo huweza kugundua na kutibu maumivu, kuyatathimini madhara yake kiujumla na huku wakitambua mjongeo wa mwili ambao unaweza kuchochea tatizo hilo kuendana na majeraha yalipo katika mwili.
Baadhi ya makocha, viongozi na mashabiki ndio wana kawaida ya kushinikiza wachezaji walio na majeruhi na maumivu kuwapa dawa za maumivu.
Ikumbukwe kuchoma sindano na kunywa dawa za maumivu zinakwenda kuondoa maumivu na kukupa utulivu kwa muda tu na si kukarabati jeraha na kuliponesha kabisa.
Hata pale anapopona mfupa, msuli au tishu zilizojeruhiwa kwa mara nyingine, hatari ya kujeruhiwa mara kwa mara ni kubwa kwani tishu hizo zinapungua uimara kuweza kuhimili michezo na mazoezi.
Ni vizuri kuepuka kumchezesha mchezaji au kucheza akiwa na maumivu au majeruhi. Vizuri kuzingatia ushauri wa madaktari wa timu na wataalam wengine wa afya.
USITUMIE HOVYO DAWA
Wanamichezo wengi hupatwa na majeraha mbalimbali wakati wa kucheza ikiwamo kuchanika misuli, michubuko, kuvilia damu, kuteguka viungo na kuvunjika mifupa ya mwili. Majeraha ya michezo yanaweza kuzuilika lakini ni kawaida kutokea unapocheza.
Unaweza usipate majeraha kwa ajali au faulo wakati wa kucheza lakini ukapata majeraha mwilini kutokana na kufanyishwa mazoezi magumu kupita kiasi.
Ni kawaida majeraha kuambatana na maumivu ambayo huwa ni kama kero na yakizidi huwa ni mateso. Hali hii ndiyo huwapa uwashawishi wachezaji kutumia dawa za maumivu bila maelekezo ya madaktari.
Ni sahihi kutumia dawa hizo unapokuwa na maumivu kiasi na huku ukihitaji kucheza kama huongezi ukubwa wa jeraha, lakini huwa sio sahihi inapotekea na kujengeka kuwa ni mazoea kila wakati. Jambo la msingi kabla ya kutumia dawa zozote vizuri kumwona mtaalamu wa afya aliye jirani nawe au mjulishe daktari wa timu kuwa una maumivu yeye ndiye atakayeamua.
Dawa za maumivu ziko za aina nyingi na kila moja au kila jamii ya dawa hizo huwa na kazi tofauti. Zipo za kukabiliana na madogo mpaka ya kati na zipo za maumivu ya kati mpaka makali. Dawa hizi huwa na maeneo maalumu ya mwilini zinapokwenda kufanya kazi.
Zipo ambazo ni maalumu kwa ajili maumivu ya kichwa tu, tumbo, misuli ya pembezone mwa mwili na mishipa ya fahamu. Hutokea wachezaji kupata uraibu wa kutumia dawa za maumivu kutokana na kutumia mara kwa mara.
Hufanya hivyo wakidhani wanatibu jeraha kumbe ni kukata maumivu tu lakini tatizo haliponi kwa dawa hizo. Tabia hii huwakumba wachezaji wenye maumivu sugu. Pasipo kujua kuwa kadiri unavyosababisha uungaji wa jeraha kuchelewa na ndivyo pia huchukua siku nyingi kuwa imara kwa asilimia. Dawa nyingi za maumivu zimechanganywa changanywa kitaalamu na nyingi zinakuwa na majina ya kibiashara.