Kwa miaka ya hivi karibuni timu za Simba na Yanga ndizo ambazo zilikuwa zikilalamikiwa kwa kuongoza kupewa penalti ingawa kwa msimu huu mambo yamebadilika tofauti na ilivyokuwa mwanzoni.
Mwanaspoti linakuletea timu vinara wa kupata penalti nyingi msimu huu ikiwa imebakia michezo saba tu.
DODOMA JIJI (6)
Hii ndiyo timu pekee hadi sasa inayoongoza kwa kupata penalti nyingi (6) ingawa ni moja tu kati ya hizo iliyofungwa ya mshambuliaji, Collins Opare kwenye mchezo na Polisi Tanzania Novemba 1, mwaka jana.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Ushirika Moshi, Opare alipata bao hilo dakika ya mwishoni mwa mchezo huo baada ya kutanguliwa na Idd Kipagwile dakika ya 52 aliyefunga pia kwa penalti.
Mbali na Opare kupata ila alikosa katika mchezo na Namungo ambapo Dodoma Jiji ilipoteza kwa bao 1-0, Novemba 26, mwaka jana katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida.
Wengine ni Paul Peter katika mchezo wao na Mtibwa Sugar waliopoteza pia kwa bao 1-0, Oktoba 25, mwaka jana sawa na Aman Kyata aliyekosa timu yake ikishinda mabao 2-1 na Ruvu Shooting Desemba 3.
Mbwana Kibacha alikosa mbili akianza kwenye mchezo na Tanzania Prisons waliopoteza mabao 2-0 Desemba 21 mwaka jana sambamba na kichapo pia cha 2-0 dhidi ya Geita Gold Januari 14 mwaka huu.
GEITA GOLD (5)
Katika penalti tano iliyopata timu hii mastaa wake wote wamefunga akianza Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ anayeichezea Simba kwa sasa aliyefunga akianza kwenye ushindi wa mabao 2-1 na Namungo Oktoba 22.
Nyingine aliyofunga Saido ni ile ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mtibwa Sugar Desemba 4, mwaka jana.
Offen Chikola alifunga pia wakati kikosi hicho kikitoka sare ya bao 1-1 na Azam FC, Desemba 21 sawa na Haruna Shamte aliyefunga dhidi ya Singida Big Stars walipopoteza 2-1 Desemba 30, mwaka jana.
Nyota mwingine ni Geofrey Manyasi aliyeifungia timu hiyo bao moja wakati ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Nyankumbu Februari 17 mwaka huu.
SINGIDA BIG STARS (4)
Katika penalti hizo ni moja tu waliyokosa ambayo ni ya staa wake, Meddie Kagere kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Ihefu, mechi iliyochezwa Uwanja wa Liti mkoani Singida Oktoba 24, mwaka jana.
Mastaa waliopata ni Dario Frederico katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City Agosti 21 huku Deus Kaseke akifunga bao moja wakati timu hiyo ilipopoteza 2-1 na Coastal Union Desemba 7, mwaka jana.
Mbrazili na nyota wa kikosi hicho, Bruno Gomes alifunga pia mkwaju wa penalti kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold katika mchezo uliochezwa Desemba 30, mwaka jana Uwanja wa Liti.
TANZANIA PRISONS (4)
Kati ya hizo nne masta wa Prisons wamefunga zote akianza Ismail Mgunda katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji Agosti 20, mwaka jana, mechi iliyopigwa Uwanja wa Liti mkoani Singida.
Jeremiah Juma alifunga mara mbili akianza na ushindi wa 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania Oktoba 25, mwaka jana kisha akafunga tena katika kichapo cha 2-1 na Ihefu Januari 21, mwaka huu Uwanja wa Sokoine.
Nyota mwingine aliyefunga ni Jumanne Elifadhili wakati timu hiyo ilipofungwa mabao 2-1 dhidi ya Singida Big Stars katika mchezo wa kuvutia uliochezwa Desemba 17, mwaka jana Uwanja wa Sokoine.
YANGA (3)
Mabingwa hao watetezi wamepata penalti tatu na kati ya hizo ni moja tu waliyopata iliyopigwa na winga wake, Bernard Morrison kwenye ushindi wa timu hiyo wa 1-0 dhidi ya Geita Gold Oktoba 29.
Fiston Mayele ambaye anaongoza kwa ufungaji mabao hadi sasa akifunga 15 alikosa katika mchezo wao na Polisi Tanzania Agosti 16, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid licha ya timu yake kushinda 2-1.
Nyota mwingine aliyekosa ni Djuma Shaban katika mchezo dhidi ya Azam FC Septemba 6, mwaka jana wakati timu hizo zilipofungana mabao 2-2, mechi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Timu nyingine zilizopata penalti tatu ni Coastal Union ambayo imepata zote kati ya hizo, Ruvu Shooting imepata moja, KMC ikitupia zote huku mastaa wa Ihefu wakipata moja tu na kukosa mbili.
Simba msimu huu hadi sasa imepata penalti mbili na zote imefunga akianza Clatous Chama dhidi ya Geita Gold katika ushindi wa mabao 3-0 Agosti 17, mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ alifunga pia penalti wakati wa mchezo na Mbeya City walioshinda 3-2 Januari 18, mwaka huu katika mechi kali na ya kusisimua iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Nyingine zilizopata penalti mbili mbali na Simba ni Azam FC iliyopata zote huku Namungo ikipata moja sawa na Mbeya City pia.
Timu zilizopata penalti moja ni Kagera Sugar ilikosa katika mchezo wao dhidi ya Yanga Novemba 13, mwaka jana ilipochapwa kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza iliyokoswa na Erick Mwijage.
Mbali na Kagera ila Polisi Tanzania imepata moja na kuiweka kimiani iliyofungwa na nyota wake, Idd Kipagwile katika mchezo na Dodoma Jiji uliopigwa Novemba 1, mwaka jana na kumalizika 1-1.
MSIKIE MEDO
KOCHA wa Dodoma Jiji Mmarekani, Melis Medo ambaye kikosi chake kinaongoza kwa kukosa penalti nyingi kwenye Ligi Kuu Bara hadi sasa msimu huu anasema sababu inayochangia hali hiyo kujitokeza ni kujiamini kuliko pitiliza.
“Mchezaji anaweza kufanya vizuri wakati wa mazoezi lakini kwenye mechi husika akaanza kuingiwa na hofu au akajiamini kuzidi kiwango hivyo ni suala tu la kuwajenga kisaikolojia,” anasema kocha huyo raia wa Marekani.