Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hata huku wanakiwasha vilevile

Meddie Kagere Singida Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Meddie Kagere

Sat, 1 Oct 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Presha ya kusaka mafanikio iliyopo katika klabu za Simba na Yanga inazifanya klabu hizi za soka kusajili wachezaji wengi wenye vipaji.

Mambo haya kwa pamoja husababisha vita kali ya namba na athari yake ni kwa baadhi ya wachezaji kujikuta wakipoteza namba ama kushindwa kupenya kikosini.

Makala hii inakupitisha kwa wakali hawa.

MEDDIE KAGERE (SINGIDA BIG STARS)

Kagere aliwagawa mabosi wa Simba kwani baadhi yao walitaka abakie huku wengine wakitaka aondoke kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake msimu uliopita.

Baada ya mapishano hayo mshambuliaji huyo alifikia uamuzi wa kuvunja mkataba kwa makubaliano ya pande zote mbili kufuatia aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Zoran Maki kutoridhishwa na kiwango chake licha ya hapo awali kuomba muda ili amwangalie vizuri.

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Simba 2018 akitokea Gor Mahia ya Kenya ameweka heshima kubwa ndani ya kikosi hicho kwani ndani ya misimu minne amefunga jumla ya mabao 65 kwenye Ligi Kuu Bara akianza msimu wa 2018/2019 aliomaliza na mabao 23, kisha kuongeza mengine 22 msimu wa 2019/20 na 2020/21 alifunga 13 huku 2021/22 akifunga saba nyuma ya Kibu Denis aliyemaliza kinara wa kikosi cha Simba akiwa na mabao manane.

Takwimu zake ndizo zilizombeba kujiunga na Singida Big Stars msimu huu licha ya kuonekana wazi kushindwa kukidhi mahitaji ya Simba msimu uliopita.

DAVID KAMETA ‘DUCHU’ (MTIBWA SUGAR)

Kiwango kizuri alichokionyesha akiwa na Lipuli 2020 kilimfanya kusajiliwa Simba akiaminiwa atakuwa mbadala sahihi wa Shomari Kapombe.

Mambo yalikuwa tofauti kwa staa huyu kwani hakuweza kuendana na matumaini aliyowekewa na kutolewa kwa mkopo, Geita Gold na sasa Mtibwa Sugar anayoichezea ambapo anaendelea kuonyesha kiwango kizuri huku akiwa ni beki wa pembeni tegemeo kwenye kikosi hicho.

IBRAHIM AME (KMC)

Beki huyu wa kati alijiunga na Simba msimu wa 2020/21 akitokea Coastal Union ambako alionyesha kiwango kizuri kilichowavutia mabosi wa timu hiyo kumsajili japo ushindani wa namba ulimfanya kutolewa mara kwa mara kwa mikopo kwenda Mtibwa Sugar na KMC.

Licha ya kutofanya vyema akiwa na Simba, Ame amekuwa mchezaji tegemeo kuanzia alipokuwa Mtibwa Sugar na sasa KMC huku akitengeneza pacha nzuri na Andrew Vincent ‘Dante’.

DEUS KASEKE (SINGIDA BIG STARS)

Kaseke alianza kuichezea Yanga msimu wa 2015/17 akitokea Mbeya City ambayo kipindi hicho ilikuwa ni timu tishio kwa vigogo hao nchini kabla ya kutolewa kwa mkopo Singida United msimu uliofuata wa 2017/18 kisha kurejea tena hadi mkataba wake ulipoisha Julai 14 mwaka huu.

Ushindani wa nafasi ulimfanya kushindwa kuwika huku mara nyingi akitokea benchi jambo ambalo lilimfanya kujiunga na Singida Big Stars msimu huu huku akiwa ni mhimili mkubwa kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu Mholanzi, Hans van der Pluijm.

BALAMA MAPINDUZI (MTIBWA SUGAR)

Julai 14 mwaka huu Yanga iliachana na kiungo mshambuliaji huyo aliyepewa jina la ‘Kipenseli’ baada ya kudumu naye kwa miaka mitatu tangu alipojiunga nayo Juni 22, 2019 akitokea Alliance.

Kiungo huyo aliyewahi kuwa nje ya uwanja msimu mzima wa 2019/2020 baada ya kuvunjika kifundo cha mguu wa kushoto na kufanyiwa upasuaji mkubwa nchini Afrika Kusini alikiri majeraha hayo yalimfanya kushindwa kutimiza malengo yake ndani ya Yanga.

Hata hivyo, msimu huu nyota huyo amejiunga na Mtibwa Sugar na amekuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.

YASSIN MUSTAPHA (SINGIDA BIG STARS)

Beki huyu wa kushoto alitambulishwa kuichezea Singida BS Julai 18, mwaka huu baada ya kutopata nafasi ya kucheza Yanga.

Mustapha hakuwa na msimu mzuri kwani mara nyingi benchi la ufundi la Yanga lilikuwa likiwapa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza Farid Musa, Kibwana Shomari na Brayson Raphael ambaye naye hakuwa na msimu mzuri kutokana na kupata majeraha kila uchao.

Nyota huyu aliyeanzia maisha yake ya soka Dodoma katika timu ya Shelly anaendelea kukiwasha kwenye maskani yake mapya huku akiwahi kuzichezea timu za Dodoma Jiji, Stand United, Mwadui United, Coastal Union pamoja na Maafande wa Polisi Tanzania.

MSIKIE MANICHE

Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma ‘Maniche’ anasema sio kila mchezaji anayeachwa na timu kubwa hana uwezo wa kucheza bali nafasi huwa finyu kwao kutokana na usajili wa mastaa wakubwa kutoka nje ambao unawaathiri kushindwa kupambania namba.

“Kusajiliwa kwao kunaonyesha wana kitu ndio maana wamefika hapo walipo ila suala la mabadiliko ya benchi la ufundi mara kwa mara kwenye timu hizi kubwa kulingana na mahitaji nayo inachangia kwa sababu kila kocha anakuja na mifumo yake na wachezaji wake,” anasema Maniche nyota wa zamani wa Simba aliyekipiga pia Mtibwa kabla ya kugeukia ukocha akianzia timu ya vijana.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz