Ni kama vile mgonjwa mzee hivi. Kila siku anaumwa sehemu mpya bila kufahamu chanzo cha tatizo lake. Ndivyo ilivyo Azam FC. Ina shida kubwa sehemu, lakini hata wenyewe hawaifahamu.
Baada ya watu kuamini kuwa Azam haijafanya usajili mkubwa kwa miaka mingi ndio maana inashindwa kushindana na Simba na Yanga, kwa msimu huu walivunja benki na kufanya kweli.
Wakasajili wachezaji mahiri kutoka maeneo mbalimbali Afrika. Wachezaji wawili Kipre Junior na Tape Edinho walikuwa kwenye kikosi bora cha Ligi ya Ivory Coast.
Wakasajili kipa mahiri sana, Ali Ahmada. Mabeki Malikou Ndoye na Nathaniel Chilambo. Viungo wa shoka Issah Ndala na James Akaminko.
Kwa kifupi Azam ilifanya usajili mkubwa sana msimu huu. Pengine kuliko Simba au Yanga. Walijiimarisha kila eneo.
Ndio maana ukikitazama kikosi cha Azam kwenye makaratasi kinatisha. Kinaonekana kina wachezaji mahiri kila eneo. Yaani kimekamilika.
Hebu fikiria kwenye ushambuliaji kuna Idris Mbombo, Rogers Kola na Prince Dube. Mastraika halisi. Achana na Dube ambaye kila mtu uwezo wake anaufahamu.
Huyo Mbombo ni straika mwenye wasifu mkubwa hapa Afrika. Amefanya makubwa pale Zambia. Amecheza Sudan na Misri. Ni mchezaji mkubwa.
Kola pamoja na umri kuanza kumuacha, Ila pia ni straika mahiri. Amecheza hadi Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Kwa mawinga Azam inao bora sana. Ina Ayoub Lyanga, Kipre Junior, Idd Seleman ‘Nado’, Abdul Suleiman ‘Sopu’ na wengineo. Kocha ana chaguo pana kila sehemu.
Lakini pamoja na wachezaji hao mahiri, bado Azam haifanyi vizuri. Kuna tatizo gani pale Chamazi?
Wachezaji wengi wamekuja wakiwa mahiri, lakini sasa wameishia kuwa wa kawaida. Nini kinawakuta wachezaji hawa?
Kwanini Fiston Mayele bado yupo kwenye ubora wake ule ule tangu ametua Yanga, kwanini Dube ameisha? Ni swali gumu.
Kwanini Djigui Diarra yupo kwenye ubora wake ule ule, lakini Ali Ahmada ameporomoka Kilango chake kwa kasi ya kimbunga? Inafikirisha sana.
Kuna tatizo mahala pale Azam. Mwanzo wa msimu walileta kocha bora sana. Kocha Mkubwa. Kocha amewahi kutamba kwenye michuano ya CAF. Nini kilitokea? Alifukuzwa baada ya mwezi mmoja tu.
Kwanini kocha aliyewahi kufanya vizuri na timu nyingi Afrika ashindwe kudumu Chamazi miezi miwili? Kuna tatizo mahala. Kinachoumiza ni kwamba inawezekana hata Azam wenyewe hawajui tatizo linalowatafuta liko wapi.
Kuna wakati naamini tatizo ni Mtendaji Mkuu wa timu, Abdulkarim Amin ‘Popat’ ana shida. Pengine utendaji wake hautoshi kwenye timu. Ameshindwa kuwa na wasaidizi wazuri.
Mfano leo Azam ikiwa inacheza Mbeya, nani huwa anaratibu shughuli za safari? Pale Simba wana Abbas Ally wakati Yanga ina Hafidh Salehe. Azam wana nani? Sijui!
Nani anasimamia kambi yao pale Chamazi. Yawezekana tunaona wachezaji wa Azam wanashuka viwango kila siku kumbe nidhamu yao kambini ni ndogo. Yawezekana wachezaji hawakai kambini usiku. Nani anajua? Hakuna!
Hapa majuzi nilisikia Dube, Mbombo na Kola wamegoma kufanya mazoezi wakitaka kufahamu hatma ya mikataba yao mipya. Inachekesha sana.
Mastraika hawajawa na msimu mzuri wanapata wapi jeuri ya kugoma? Kuna tatizo mahala. Ofisi ya Mtendaji Mkuu ni sehemu ya tatizo hili. Anahitaji kuongezewa nguvu ama kubadilishwa.
Ukweli ni kwamba kwa uwekezaji wa Azam, ulipaswa kuwa pale juu kushindana na Simba na Yanga. Lakini wameangukia pua mapema. Wako huku chini wanashindana na Singida Big Stars kuwania nafasi ya tatu. Aibu iliyoje!
Nilitazama mchezo wao dhidi ya Ihefu. Azam walikuwa ovyo kila mahali. Walicheza kama timu isiyokuwa na wachezaji wazuri wala mipango. Inashangaza sana.
Azam wanafungwaje na Ihefu wakiwa wamezidiwa kila kitu? Ihefu walikuwa bora kila mahala. Na hii ni mechi moja tu. Kuna mechi lukuki msimu huu Azam walikuwa ovyo mno. Kuliko uhalisia wao.