Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Harry Kane na ubabe wa kizazi chetu kazini

HARRY KANE M 1140x640 Harry Kane

Sun, 2 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jinsi gani maisha yanavyokwenda kasi. Tom Burke, mwanariadha mahiri wa Marekani wa mbio fupi, Aprili kama hii mwaka 1896 aliweka rekodi ya dunia ya kushinda mbio za mita 100 katika michezo ya Olimpiki. Alitumia sekunde 12.

Baadaye watu waliendelea kupunguza sekunde za rekodi. Wapo wengi waliovunja kwa sekunde 11. Wengine wakavunja kwa sekunde 10. Lakini miaka 116, Usain Bolt wa Jamaica, alivunja kwa sekunde 9 na nukta 63. Hivi ni namna mwanadamu wa sasa anavyokwenda kasi.

Nilikumbuka haya nilipokuwa namshuhudia Harry Kane akikabidhiwa kiatu maalumu cha kuwa Mfungaji Bora wa muda wote katika timu ya taifa ya England mwanzoni mwa wiki hii. Kwa sasa Kane ndiye Mfungaji Bora wa muda wote England. Amefikisha mabao 55.

Amempita Wayne Rooney ambaye ana mabao 53. Imenikumbusha kitu namna maisha yanavyokwenda kasi katika dunia tunayoishi. Kabla ya hapo rekodi yake ilikuwa inashikiliwa na mkongwe Bobby Charlton aliyekuwa amefunga mabao 49.

Charlton aliachana na soka mwaka 1970 na rekodi yake ilikuja kuvunjwa na Rooney miaka 45 iliyofuata. Hapo katikati walipita washambuliaji wengi wa Kiingereza, lakini walishindwa kuvunja. Kina Gary Lineker, Alan Shearer, Michael Owen na wengineo.

Hata hivyo, Rooney aliungana na mastaa wapya wa soka katika kizazi hiki ambao wamevunja rekodi nyingi katika timu zao za taifa na klabu. Lakini kuonyesha kwamba kizazi hiki kina kitu tofauti, wakati ilichukuwa miaka 45 kwa Rooney kuvunja rekodi ya Charlton imechukua miaka minane tu, Kane kuvunja rekodi yake.

Wachezaji wa zama hizi wanafunga sana? Kwanini sasa? Kuna kitu gani? Wapinzani wamekuwa dhaifu? Huyu huyu Kane wiki chache zilizopita alivunja rekodi ya kuwa Mfungaji Bora wa muda wote katika kikosi cha Tottenham Hotspur ‘The Coys’ akimpita kwa mabao mkongwe wa klabu yake, Jimmy Greaves.

Lakini tazama pale Brazili, Neymar amemfikia mfalme wa soka duniani, Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’, kwa ufungaji bora wa muda wote katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazili. Hadi sasa wote wana mabao 77. Neymar bado anaendelea kucheza na anahitaji bao moja tu kuweka rekodi yake.

Hapa katikati wamepita washambuliaji wangapi mahiri wa Kibrazili lakini walishindwa kufanya hivyo? Zico, Romario, Ronaldo de Lima, Ronaldinho na wengineo wote walishindwa kufanya kile ambacho Neymar amekifanya.

Pale Argentina, Lionel Messi alishaivunja rekodi ya ufungaji bora wa muda wote miaka kadhaa iliyopita. Kwa sasa ana mabao 102 na alivunja rekodi ya Gabriel Batistuta aliyekuwa na mabao 55. Kinachoshangaza katika hili ni kwamba mkongwe, Diego Maradona anashika nafasi ya sita katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote pale Argentina.

Maradona alifunga mabao 29 tu, licha ya kusifika kulikopitiliza kiasi cha kulinganishwa na Pele. Wakati mwingine inaweza kueleweka kwa sababu Maradona alikuwa mchezeshaji zaidi katika kikosi cha Argentina na alitengeneza mabao mengi ya wenzake.

Sehemu ambayo wafungaji wamekuwa wakisuasua katika zama hizi ni Ujerumani ambako licha ya Miroslav Klose kuvunja rekodi ya muda mrefu ya hayati Gerd Muller, lakini washambuliaji wa sasa wameshindwa kumfukuzia Klose.

Katika orodha ya wafungaji 10 bora wa muda wote katika kikosi cha Ujerumani ni Thomas Muller tu ambaye anaendelea kucheza soka na wengineo wote ni wastaafu. Hii inakuonyesha ni namna gani Ujerumani ina uduni wa washambuliaji katika zama mpya za soka.

Tukiachana na soka la kimataifa, lakini hata katika klabu wanasoka wengi wa sasa wamevunja rekodi za ufungaji bora wa muda wote ndani ya klabu zao. Huyu huyu Rooney ndiye mfungaji bora wa muda wote Manchester United akimpiku tena Charlton. Jiulize Manchester wamepita wafungaji wangapi kuanzia pale Charlton alipoacha soka mwaka 1970 hadi Rooney alipoingia United mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Lakini ndivyo ilivyo katika klabu nyingine. Thierry Henry ndiye mfungaji bora Arsenal, Frank Lampard ndiye mfungaji bora Chelsea wakati Sergio Aguero ndiye mfungaji bora wa muda wote Manchester City. Ni Liverpool tu ndipo ambapo Ian Rush anaendelea kushikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote.

Hata hivyo, jaribu kutazama. Rush aliichezea Liverpool katika vipindi viwili vya jumla ya miaka 15 ambapo alifunga mabao 346 katika mechi 660. Hata hivyo, Mohamed Salah tayari amefunga nusu ya mabao hayo katika mechi 293. Salah amefunga mabao 178 katika kipindi cha miaka mitano tu.

Kama Salah akidumu klabuni hapo kwa miaka mitano mingine sio ajabu akaivunja rekodi ya Rush ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo na hivyo kutumia miaka 10 tu kufikia rekodi ya Rush ambaye alitumia miaka 15 kuweka rekodi hiyo.

Kifupi baada ya Kane kuvunja rekodi ya Rooney ndani ya miaka michache kuna maswali kadhaa ya kujiuliza. Washambuliaji wa sasa wanacheza dhidi ya timu dhaifu? Kwanini amechukua muda mfupi kuvunja rekodi ya Rooney. Je Kane ni mkali kuliko Rooney? Kuliko Charlton?

Lakini hapohapo unaweza kujikumbusha ni namna gani soka imekuwa mchezo wenye kasi zaidi tofauti na zamani. Mifumo imekuwa ikifanya kazi zaidi tofauti na zamani. Zamani wachezaji walikuwa wakitumia juhudi binafsi katika ufungaji, lakini sasa wamekuwa wakisaidiwa zaidi katika upatikanaji wa mabao. Labda hili limesaidia kwa kiasi kikubwa.

Pia inatajwa kwamba mchezo wenyewe wa soka kwa sasa umekuwa laini tofauti na siku za nyuma. Kwamba sheria zimekuwa nyingi na wachezaji wamekuwa wakilindwa zaidi tofauti na zama za kina Maradona na Pele.

Vyovyote ilivyo, sisi watu wa kizazi hiki, tuna bahati ya kushuhudia mastaa wengi wa kizazi hiki wakivunja rekodi zilizowekwa kwa muda mrefu katika klabu na timu za taifa. Mastaa wengi ambao wamevunja rekodi za miaka mingi wamekuwa wakiendelea kucheza soka.

Lakini huenda tukapata bahati ya kuona rekodi zao pia zikivunjwa mapema kabla hatujafa. Kwa mfano, kama Erling Haaland akiendelea kuichezea Manchester City kwa miaka sita ijayo sio ajabu akaifikia rekodi ya Kun Aguero ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika kikosi hicho.

Columnist: Mwanaspoti