Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Half time’ Mwamnyeto, Mayele mbili Rivers sifuri

Nondo Mayele ‘Half time’ Mwamnyeto, Mayele mbili Rivers sifuri

Wed, 26 Apr 2023 Chanzo: mwanaspoti

Katika historia ya klabu yao iliyoundwa hawakuhi kukaribia kukifanya walichokifanya juzi pale Port Harcourt juzi alasiri ya jua kali. Lakini walikifanya kwa uhakika. Kukaribia kutinga nusu fainali ya miongoni mwa michuano mikubwa Afrika.

Yanga, au waite Wananchi juzi walikaribia hatua ya nusu fainali kwa mbwembwe pale Nigeria. Haikushangaza sana kwamba wameshinda. Ilishangaza kwamba walikuwa wameshinda bila ya hofu kama vile walikuwa wanacheza katika uwanja wa Taifa.

Msimu huu tayari Yanga na Simba zimeshinda mechi sita ugenini. Dhidi Nyassa Big Bullets, Primera Agosto, Club Africain, Vipers, TP Mazembe na sasa Rivers. Kila ushindi ulikuwa muhimu lakini huu ulikuwa muhimu zaidi kwa sababu ulikuwa unakaribia kuipeleka Yanga katika hatua ambayo hawajawahi kufika.

Zaidi ni namna walivyocheza na kushinda. Uwanjani, kocha Nesreddine Nabi alionekana kuwaogopa zaidi Rivers katika kipindi cha kwanza. Akawapanga mabeki watatu, Bakari Mwamunyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job. Mbele yao aliwaweka Mudathir Yahaya na Yannick Bangala.

Kushoto alimpanga Joyce Lomalisa lakini hapo hapo akampanga Farid Mussa mbele yake ili amasaidie. Kulia akampanga Djuma Shaaban ambaye alikuwa anasaidiwa kwa karibu na Job. Nabi alionekana kuwa muoga hasa.

Mbele aliwaacha Fiston Mayele na Aziz Ki watafutane wenyewe. Hapo mbele walikosa mabao machache katika kipindi cha kwanza. Aziz alitazamana na kipa akachagua kuupitisha mipira katika miguu yake. kipa akaucheza. Kipindi cha pili Fiston alimuonyesha namna ya kufanya pindi anapotazamana na kipa.

Mayele pia alikosa bao la wazi la kichwa. Kipindi cha Nabi akapunguza hofu kwa Rivers. Akawatoa Djuma, Lomalisa na Farid. Akawaingiza Tuisila Kisinda, Jesus Moloko na Shomari kibwana. Job akaenda kucheza katika ulinzi wa kulia ambako amekuwa akicheza pia katika siku za karibuni.

Timu ikafunga. Mbio za akina Tuisila na Moloko zikaanza. Walipokuwa hawana mpira wakati wakabaji zaidi. walipokuwa wana mpira wakafunguka. Hata hivyo bao la kwanza na la pili lilikuja kwa utaalamu wa nahodha Mwamunyeto. Akacheze nafasi ya Fei Toto pale mbele? tusitie chumvi lakini Mwamunyeto alikuwa katika ubora wake wa kupita pasi za mwisho.

Ya kwanza ilitokana na uzembe wa Rivers. Walipomuona mlinzi wa kati ana mpira. Amesogea mpaka katikati kisha akavuka. Bado waliamini kwamba ilimpasa mpasie mtu mwingine kabla ya huyo mtu mwingine kupiga pasi ya mwisho. Walikosea. Bakari aliamua kuchukua jukumu mwenyewe.

Alipiga pasi iliyovuka mistari miwili ya ulinzi ya Rivers na kumfikia Mayele ambaye alimfundisha Aziz Ki kile ambacho unapaswa kufanya ukitazamana na kipa. Kuna wale ambao wanajaribu kutafuta tobo lakini kama kipa yupo karibu unanyanyua mpira juu. Bao safi.

Baada ya hapo niliwaambia watu niliokuwa natazama nao mechi kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa Yanga kupata bao la pili kwa sababu Rivers wangepoteza nidhamu ya ulinzi na kujaribu kusawazisha bao kwa sababu walikuwa nyumbani. Na ndicho kilichotokea.

Walipoteza nidhamu wakati walipopoteza mpira mzuri wa faulo. Aliyetengewa alishindwa kuunganisha na Yanga wakaupora mpira. Hapo ndipo zilipoanza mbio za akina Moloko. Aliukimbiza kwa kasi kuelekea lango la Rivers.

Kilichonishangaza ni namna ambavyo Mwamunyeto naye aliunga katika msafara wa Mamba. Mara nyingi walinzi wa kati huwa hawajihusishi katika mashambulizi ya kushtukiza. Kazi hiyo inaachiwa kwa washambuliaji, mawinga, viungo na hata walinzi wa pembeni.

Lakini Nondo aliingia katika msafara na akajikuta katika nafasi nzuri mbele ya safari. Mpira wa Moloko ulikwenda kwa Mayele, halafu akarudishiwa Nondo ambaye alikuwa anatazamana na golikipa wa Rivers. Ni mara chache kwa wachezaji wa Kiafrika kupunguza mihemko katika nafasi aliyokuwepo.

Wengi wangechagua kufunga ingawa ni wazi kwamba kipa alikuwa amempunguzia lango kwa kiasi kikubwa. Nondo alichagua kupiga pasi kwa Mayele ili afunge bao rahisi. Na lilikuwa bao rahisi haswa. Bao la pili kwa Mayele. Bao la tano katika michuano hii. lakini bao ambalo lilikuwa linawahakikishia Yanga urahisi wa kutoka nusu fainali wiki moja baadaye pale Temeke.

Wakati Yanga wakishangilia bao hili. Wakati Yanga wakishangilia filimbi ya mwisho ya mwamuzi. Kule Misri, Pyramids walikuwa wakichomoa kwa penalti bao la dakika ya 55 waliofungwa na Marumo Gallants. Inashangaza na wakati huo huo haishangazi.

Licha ya kwamba Marumo inafanya vibaya katika Ligi ya moto ya Afrika Kusini, lakini wanafanya vizuri katika michuano hii. Hata hivyo ilitazamiwa kwamba huenda hatua hii ingekuwa moto kwao. Kwamba huenda hatua hizi zingekuwa maji ya shingo kwao, hasa unapocheza na timu kama Pyramids.

Hata hivyo mambo hayakuwa hivi katika pambano hili ambalo mshindi wake anaweza kucheza na Yanga katika nusu fainali kama Yanga wakimalizia karata yao vema dhidi ya Rivers. Ndio kwanza Pyramids walilazimika kuchomoa wakiwa nyumbani. Kuna mambo mawili hapa. Huenda Pyramids wameshuka kidogo kutoka kule walikokuwa. Au huenda tuendelee tu kuuheshimu moto wa Marumo.

Kitu cha msingi kwa sasa kwa Yanga kabla ya kuifikiria mechi ya nusu fainali kama ninavyofanya nadhani inabidi wamalizie kazi katika uwanja wa Taifa. majuzi Taifa Stars walitupa onyo kwamba tuendelee kuuheshimu mchezo wa soka.

Walikwenda Ismailia Misri wakashinda dhidi ya Ugaanda. Pambano la marudiano ambalo lilikuwa na hamasa kubwa kwetu tukachapwa uwanja wa Taifa mbele ya Waziri Mkuu wa nchi huku uwanja ukiwa umejaa.

Lile ni onyo kwa Yanga. Warudi katika uwanja wa Taifa na kujipanga hasa kwa ajili ya mechi ya marudiano. Mifano kama hii ipo mingi katika soka hasa katika hizi. Mifano hii unapata katika michuano ya CAF, Ligi ya mabingwa wa Ulaya, Europa na kwingineko.

Hata hapa nyumbani kuna mfano mwingine unaoudhi. Tena wa hatua muhimu zaidi kuliko hii robo fainali. Mwaka 1993, Simba walicheza na Stella Abidjan katika fainali za michuano ya CAF. Kule ugenini walitoka suluhu ya bila kufungana.

Katika fainali ya pili pale uwanja wa Taifa mnyama akachapwa mabao 2-0 shukrani kwa staa wa zamani wa Ivory Coast, Boli Zozo. Mpira lazima uheshimiwa na Yanga wanapaswa kufanya hivyo kama wanataka kwenda katika nusu fainali kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Hii ni kama mechi ambayo ipo katika mapumziko. Na katika mapumziko hayo tuendelee kusifu pasi mwili za mwisho za Mwamunyeto, kisha mabao mawili ya Mayele lakini mechi bado haijamalizika. Yanga wauheshimu mchezo.

Columnist: mwanaspoti