Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Haki kotekote! Usishangae, wapo waamuzi waliojipa kadi nyekundu

Kadi Nyekundu Pic Haki kotekote! Usishangae, wapo waamuzi waliojipa kadi nyekundu

Fri, 10 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sheria inatakiwa kumgusa kila mtu bila kujali ni mkubwa, mdogo, tajiri, masikini au anayo madaraka ya usimamizi au uongozi. Hii pia ipo katika michezo ikiwa ni pamoja na kandanda ambapo waamuzi nao hutakiwa kuhakikisha hawavunji sheria za kuongoza mchezo.

Hata katika mahakama sheria zinawatala mahakimu na sio tu kutoa uamuzi wa haki, bali na wao pia kutii sheria kama wanavyofanya washitakiwa, mashahidi, mawakili na wanaofika kusikiliza kesi.

Kwa mfano hivi karibuni wapo majaji walioonyesha mfano mzuri wa kuheshimu sheria kwa kujipa adhabu kutokana na wao kuvunja sheria inayokataza mtu kutoa kauli au kufanya jambo linaloashiria dharau kwa mahakama.

Kwa mfano Aprili, 2013 Jaji Mkuu wa Mahakama ya Michigan nchini Marekani, Raymond Voet alijipiga faini ya Dola 25 kutokana na simu yake kulia wakati akiwa anaendesha kesi.

Alisema alistahiki kuwa mfano mzuri wa kuheshimu mahakama na kwa vile aliwahi kuwapa adhabu watu wengine wakiwemo mawakili kwa dharau mahakama asingetenda haki kama naye asingejipa adhabu kwa kudharau mahakama.

Jaji huyo alijipa adhabu ya faini ya Dola 25 na kujipa saa 24 kulipa na alifanya hivyo papohapo kabla ya kuendelea kupokea ushahidi wa kesi aliyokuwa anaisikiliza. Kule Misri, Jaji Mkuu wa Jimbo la Aswan, Mohsen Klopp Aprili, 2021 alijipiga faini ya Pauni 500 za Misri (Dola 160 za Marekani) kwa vile simu yake iliyokuwa mfukoni ilipiga kengele kwa nguvu mahakamani.

"Samahani, ni bahati mbaya lakini hiyo bahati mbaya haitoshi kuwa kisingizio cha kusamehewa kwa kuidharau mahakama," alisema Jaji Klopp.

Katika kandanda wapo waamuzi ambao matukio waliyofanya hutolewa mfano wa uadilifu kwa vile walionyesha mfano unaofaa kuigwa katika kusimamia sheria za mchezo. Miongoni mwa waamuzi hao ni mwalimu wa sekondari, Melvin Sylvester ambaye alijipa kadi nyekundu wakati alipokuwa akisimamia mchezo wa ligi ya Jumapili kati ya klabu vya Southampton Arms na Hurstbourne Tarrant.

"Nilichokozwa na wachezaji na kilichoniudhi ni kunisukuma na nilipoona wanaendelea ndio nikaamua na mimi kuwasukumia makonde," alisema.

Sylvester alisema baada ya hasara kumpungua huku mchezo ukiwa umesimama ndipo alipoelewa kwamba alikuwa amefanya kosa la kupiga wachezaji na kwa vile inapotokea wachezaji kupigana mwamuzi huwa anatoa adhabu ya kuwatoa nje kwa kuwapa kadi nyekundu, basi pia alistahili kupata kadi nyekundu na ndio maana akajipa adhabu ya kadi nyekundu na kutoka nje ya uwanja.

Hata hivyo, mchezo uliendelea kwa vile mara tu alipotoka nje ya uwanja mmoja wa watazamji ambaye alikuwa anazijua sheria za kandanda aliingia uwanjani na kuwa mwamuzi. Kufuatia tukio hilo Chama cha Soka cha Hampshire kilimpa adhabu ya kutosimamia mchezo wowote kwa wiki sita na kulipa faini ya Pauni 20.

Mwamuzi mwingine aliyejipa kadi nyekundu na kutoka nje ya uwanja ni Andy Wain katika mchezo wa Peterborough North End na Royal Mail AYL 2005. Hii ilitokana na kipa wa klabu ya North End, Richard McGaffin kummwagia matusi ya nguoni kwa madai kwamba alikuwa haitendei haki timu yake.

Wain alipoona na wachezaji wengine walijiunga katika kumtukana, aliitupa chini filimbi akamfuata kipa na kumsukumia makonde mazito ya usoni.

Yule kipa hakujibu na baada ya hapo Wain akaichomoa kadi nyekundu mfukoni akaiweka mbele ya uso wake na polepole akatoka nje ya uwanja huku watazamaji wakishangilia.

Baadaye Wain alisema siku ile alikuwa amezongwa na mawazo ya nyumbani na pia mmoja wa marafiki zake wa karibu alikuwa amefariki dunia. Kwa hiyo yale matusi yalimtibua na kumzidishia hasira.

"Nadhani kosa kubwa halikuwa kumpiga yule kipa, bali lile la kuchukua jukumu la kuwa mwamuzi wa mchezo siku ile. Ni vizuri ningekaa pembeni na kumpa filimbi mwamuzi mwingine," alisema.

Wain alisema siku ile aliingia uwanjani akiwa na msongo wa mawazo ya kifamilia na baya zaidi alipokuwa anakaribia kuingia alipata taarifa ya kusikitisha ya mmoja wa marafiki zake wa mtaani alikuwa amefariki dunia.

Katika siku za karibuni wataalamu wa kandanda wamekuwa wakijadili hatua ya waamuzi kujipa kadi nyekundu na wapo wanaoshauri kwamba makamisaa wa michezo wapewe mamlaka ya kutoa kadi wakiona waamuzi wameonyesha uzembe kupita kiasi.

Hii ni pamoja na kukataa uamuzi wa wazi unaotokana na teknolojia ya uamuzi wa video (VAR) kuonyesha kama mpira uliotingisha wavu ni bao au sio bao ama madhambi yametendeka. Wapo wanaosema hata mwamuzi akiwa anachezesha mchezo na kubainika kuwa amelewa na hajielewi, basi apewe kadi nyekundu na mwamuzi mwingine achukue nafasi yake. Tusubiri tuone Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) litafanya uamuzi gani juu ya mapendekezo haya.

Columnist: Mwanaspoti