Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Haji Manara ni msali kwa Simba?

Haji Mnr Haji Manara

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Haji Sunday Manara, aliyekuwa msemaji na mhamasishaji wa klabu ya Simba tangu 2015 ameondoka klabuni hapo kibabe ikidaiwa ni kutokana na kutoiva na mwanamama Barbara Gonzalez, ambaye ni mtendaji mkuu wa klabu hiyo.

Kwa miaka yake takribani saba aliyoitumikia klabu hiyo yumkini yeye ndiye mtu aliyedumu kwa muda mrefu zaidi kwenye nafasi huyo klabuni hapo. Mengi yamesemwa kuhusu yeye na yalitabiriwa kwa muda mrefu sana.

Lakini sitaki kujikita sana kwenye mjadala kwamba kaonewa au la ama yuko sahihi kusema alichosema kabla ya kuondoka au la. Ninachotaka kujadili hapa ni historia ya sintofahamu ya Haji Manara tangu kuzaliwa kwake.

KABLA HAJAZALIWA

Miaka ya 1970 kulikuwa na mchezaji mmoja fundi sana wa mpira hapa chini akiitwa Sunday Manara.

Kutokana na ufundi wake, watu wakamuita kompyuta katika zama ambazo yawezekana hakukuwa kabisa na kompyuta hapa nchini au zilikuwa chache zikitumika kwenye ofisi nyeti ambazo watu wa Uswahilini wasingeweza kuziona.

Katikati ya miaka hiyo Sunday akatokea kupata mchumba, binti mrembo mtoto wa mwenyekiti wa Simba, Hassan Haji. Kutokana usimba wake, mzee Hassan Haji akakataa binti yake kuolewa na mchezaji wa Yanga.

Ikabidi watu wazima wahusike kumfunulia hadi vitabu vya dini, ndipo akakubali kwa shingo upande, lakini hata hivyo kwa kutoa idhini kwa mtu mwingine kuhusika kwenye ndoa (walii) ili yeye asishuhudie binti yake akiolewa na mtu wa Yanga.

Ndoa hiyo ndiyo iliyomleta Haji Sunday Manara, ambaye sasa hivi tunajadili kuondoka kwake uongozini Simba. Kupitia historia hii, utaweza kuona kwamba ndoa ile isingefanyika, yawezekana Haji asingezaliwa.

Kwa hiyo mzee Hassan Haji ni kama alishakataa kuzaliwa kwa Haji Sunday hadi watu wazima walipohusika!

HAJI KARITHI?

Haji Manara ni mtoto wa Sunday Manara, nyota wa zamani wa Yanga ambao ni wapinzani wa jadi wa Simba. Mwaka 1976, mwaka ambao Haji alizaliwa Sunday alifukuzwa Yanga.

Kuna nadharia nyingi kuhusu kufukuzwa yeye na wenzake kadhaa akiwemo kaka yake Kitwana Manara, lakini mwisho wa siku ni kwamba alifukuzwa.

Baada ya kufukuzwa wakaenda kujistiri Morogoro kwenye klabu ya Nyota halafu wakarudi Dar es Salaam kuanzisha klabu ya Pan Africa.

Kwa hiyo sintofahamu juu ya Haji Manara leo ni mwendelezo kilekile kilichoanza tangu kwenye ndoa iliyomleta yeye hadi baba yake kufukuzwa Yanga.

Pia Haji ni mjukuu wa Hassan Haji, mwenyekiti wa Simba miaka ya 1970. Hata hili jina la Haji ameririthi kutoka kwa babu yake mzaa mama.

Mwaka 1975, mzee Hassan Haji alifukuzwa uenyekiti Simba akituhumiwa kuihujumu klabu hiyo dhidi ya Yanga. Simba ilifungwa na Yanga kwenye fainali mbili mfululizo zilizosababishwa kunyang’anywa makombe na Yanga mara zote mbili.

Kwanza ilikuwa fainali ya klabu bingwa ya taifa (sasa Ligi Kuu) iliyofanyika Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza 1974. Katika mchezo huo Simba walifugwa 2-1, huku Sunday Manara, mkwewe akifunga moja ya mabao.

Simba wakautema kwa Yanga ubingwa ambao waliushinda 1973. Halafu ikaja fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) mwaka 1975 iliyofanyika Uwanja wa Amaan - Zanzibar. Simba wakafungwa 2-0 huku Sunday Manara akifunga moja ya mabao.

Simba wakautema kwa Yanga ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati ambao walishinda 1974. Wanachama wa Simba wakaona haiwezekani kila siku wafungwe na Sunday, mkwe wa mwenyekiti wao.

Wakasema atakuwa lazima alimpa mbinu na siri, ndiyo maana anawanyanyasa. Wakamtaka mwenyekiti awaachie timu yao. Mzee Hassan Haji akawaachia timu yao na kwenda kuanzisha Red Star au Nyota Nyekundu.

Katika kumalizia mkutano wake na waandishi wa habari, Haji Manara alisema anasafiri kwenda Ulaya akirudi atakuja kufanya kazi kwenye klabu ya mpira.

Baba yake alipofukuzwa Yanga aliibukia Nyota kisha Pan Africa. Babu yake alipofukuzwa Simba aliibukia Red Star. Haji naye sasa anadaiwa kwamba anataka kuibukia klabu nyingine.

Ukichanganya mambo haya; ‘kukataliwa’ kwa ndoa iliyomleta, kufukuzwa kwa baba’ke na kufukuzwa kwa babu yake utaona kabisa Haji alizaliwa akiwa na maisha flani hivi yanayotupatia funzo nje na ndani ya mpira wa miguu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz