Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Haihitaji kuwa CR7 kuwa na msimamizi

CR7 INV Cristiano Ronaldo

Sat, 8 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Karamu mbili zilimshinda fisi, kazi mbili si mchezo mwema, mtaka yote kwa pupa hukosa yote. Orodha ni ndefu ya misemo ya wahenga wakijaribu kueleza ugumu wa kufanya kazi zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Misemo hii ina maana sana kwa wanamichezo wenye nia hasa ya kupata mafanikio ya juu kwenye michezo wanayojishughulisha nayo mathalani riadha, soka, masumbwi. Usimamizi ni muhimu.

Wana michezo wanahitaji wasimamizi kwa ajili ya kuwalea, kuwaendeleza, kuwaelekeza na kusimamia maslahi yao. Tumekuwa na kawaida ya kusema mwanamichezo fulani ana kipaji, hivyo anaweza kuendelea hata bila kusimamiwa.Hilo si kweli; hata Lionel Messi na kipaji chake kikubwa asingeweza kufika alikofika kama si kupelekwa Hispania ambako alianza kulelewa na wazazi na klabu ya Barcelona na pia kuendelezwa na kuelekezwa na wataalamu.

Mwanamichezo anapokuwa mdogo anaweza kulelewa na wazazi, walimu au ndugu zake ili abaki kwenye misingi na nidhamu ya mchezo anaoupenda au ambao ana kipaji chake.Hapa atafundishwa kufanya mazoezi na mbinu nyepesi zinazohusu mchezo huo.Kwa mazingira ya kwetu hili jukumu walimu wa shule na wazazi wanaweza kulimudu, hivyo halihitaji mtu kuwa milionea ili kulea kipaji cha mtoto au mwanafunzi wake.

Kadiri anavyokua, malezi, mafundisho na maelekezo yanaanza kuhitaji uelewa na weredi zaidi. Hapa mwanamichezo huhitaji kuangaliwa mbinu na nidhamu yake ya kimichezo lakini pia mwanamichezo huitaji kutambua nafasi yake katika jamii na namna ya kutunza taswira yake.

Mfano tuna vijana katika soka ambao wanakuwa na mitindo ya mavazi au hata nywele ambayo wameiokota kwenye runinga bila ya kujua maana yake. Mchezaji anafunga goli, anaonyesha ndani fulana yenye maandishi ambayo si mazuri kwake na kwa jamii; anaharibu taswira yake na timu.

Kumbe angekuwa na mtu wa karibu wa kumshauri hilo lisingetokea.

Mwanamichezo anatakiwa kuwa na watu wanaoangalia anachoandika au kutolea maoni mtandaoni.Cristian Ronaldo alipopata mtoto wake iliwachukua muda wasaidizi wake kufikiria namna nzuri na mtandao upi wautumie kuutaarifu umma kuhusu tukio hili.

Wanajua maisha binafsi ya mchezaji yanagusa pia hisia na mtazamo wa umma na mtazamo wa jamii una nafasi katika maendeleo na thamani ya mchezaji.

Siyo rahisi kwa mchezaji wa Bongo kuwa na utitiri wa wataalam wa mitandao lakini inawezekana kuwa na washauri au wanafamilia ambao wanye uelewa wa nafasi ya mwanamichezo katika jamii na wakaweza kumsaidia katika mambo yake.

Tumeshuhudia mara nyingi ikitokea migogoro kati ya wanamichezo na waajiri au wadhamini.Mara nyingi, hasa kwetu imetokana na wanamichezo kuwa na haraka au kukubali presha ya kusaini mkataba kabla ya kuelewa kilichomo ndani ya mkataba.

Kwa uzoefu wangu wa kuingia mikataba ya wachezaji na klabu, nakumbuka eneo la ubishi mara nyingi huwa ni kipengere cha pesa hata kama mkataba una zaidi ya vipengere 20. Mkataba unaweza kuwa na vipengere 19 vibaya lakini mwanamichezo kwa kutoelewa au kwa kutopata usimamizi mzuri akasaini mkataba huo kwa kuridhika na fedha tu.

Usishangae mwanamichezo anaweza kusaini mkataba ulioandikwa kwa Kireno bila ya kuwa na mwanasheria au mkalimani wake wa lugha hiyo asiyoielewa kwa ufasaha. Matokeo yake, anaweza kutumiwa kinyume na matakwa yake, akacheza akiwa na msongo wa mawazo na kushindwa kufikia malengo aliyokusudia. Tuliwahi kufanya mazungumzo ya kumsajili mchezaji Kelvin Yondani zaidi ya mwongo mmoja uliopita.

Yondani hakuwahi kuja ofisini kwangu peke yake. Hakuwahi kuja na mwanasheria.Alikuwa akija na kaka yake na kamwe hakukubali kuongea na mtu yeyote akiwa peke yake. Kama kaka yake hakuwepo, basi siku hiyo hakuna biashara. Kuwepo kwa kaka kulikuwa kunamuondolea mchezaji msongo wa kushughulika na masuala ya ajira. Kamwe hakutoka nje ya mstari huo wa kinidhamu aliojiwekea. Hakuwa na fedha nyingi lakini alijua umuhimu wa kuwa na msimamizi.

Utunzaji wa fedha na uwekezaji pia ni sehemu ambayo wanamichezo wana mahitaji ya ushauri. Uzoefu wa hapa ndani na dunia kwa ujumla unaonyesha kuwa wanamichezo ambao hawana familia au washauri wazuri kwa mambo ya mapato, matumizi na uwekezaji huwa na mwisho mbaya. Si vema kuwataja hapa lakini orodha ni ndefu kutoka kwa Tyson, Frank Bruno mpaka Diego Maradona. Umri na muda wa kucheza ni mfupi sana lakini gharama yake ni kubwa hivyo ni muhimu sana kwa wanamichezo kuwa na washauri katika masuala mbalimbali ili la muda mfupi wa kucheza uwe na faida mpaka uzeeni mwao.

Mwanamichezo asisubiri kuanza kukamua mamilioni ya fedha ndiyo aanze kutafuta wasimamizi.Familia, shule, klabu na wote wanaomzunguka mwanamichezo wana nafasi muhimu katika kumjengea utamaduni wa kutafuta ushauri na usimamizi utakaomkuza na kumfanya awe bora na kuwa na maisha bora pia baada ya kuacha kucheza.

Makocha wetu

Kocha maarufu raia wa Afrika Kusini Pitso Mosimane alikaririwa juma hili akiwashangaa ndugu zake kwa kutotafuta kazi nje ya Afrika ya Kusini, labda kinyume na yeye aliye na kandarasi Saudi Arabia baada ya kufundisha kwa mafanikio Mamelodi Sundown FC na Al Ahaly. Katika maoni yake Pitso anashangaa kama kweli kwenye ligi ya nchini kwake (PSL) hakuna makocha wanaoweza kufundisha Tanzania ambako mpira wa miguu umechangamka.

Maoni ya Pitso yamenifanya nijiulize mengi kuhusu makocha wetu kuliko makocha wa Afrika Kusini.Mwanzo nilijiuliza hivi huyu mtu anawaona makocha wetu hawawezi kushindana na wale wa PSL? Baada ya kufikiria zaidi nikagundua Pitso haujui mpira wetu. Laiti angeujua angewashangaa zaidi walimu wa hapa kuliko wa PSL. Asingeshangaa kwa nini walimu wa hapa hawatafuti kazi kwenye ligi za nje; angeshangaa hata kwenye ligi ya yetu bado makocha wetu wanaonekana au nao wanadhani hawawezi kufundisha timu za juu (top clubs).

Afrika kusini, ni utamaduni hasa kwa watu weusi kuogopa kutoka ili kufanya kazi ‘Afrika’.Ni utamaduni wenye mizizi kwenye historia ya nchi yao na sera za ubaguzi za apartheid. Ni wachache kama kina Pitso na Senzo Mazingiza wanaothubutu kutafuta kazi nje.

Hapa kwetu ni mchezo wa mwenye kupenda cheti hayuko viwanjani na mwenye kupenda viwanja hana cheti. Hatuna makocha wazawa wenye kujiamini na kuchukua kozi za kimataifa kama Uefa Pro. Chini ya miaka 10 iliyopita, Tanzania ilikuwa na makocha wawili tu wenye cheti/leseni A ya kufundisha mpira wa miguu inayotambuliwa na CAF, na hao hakuna aliyekuwa anahusika moja kwa moja kufundisha mpira. Walikuwa na majukumu mengine.

Baadaye, ukafanyika utaratibu, nadhani kufikia 2015 au 2016 tukawa na makocha wenye leseni A au linganifu (equivalent) yake wapatao 22. Hawa sasa walikuwa na sifa ya kufundisha timu za Ligi Kuu kwa mujibu wa kanuni za hapa nchini.Baada ya hapo ukiuliza miongoni mwao ni nani amekwishakufanya kozi zaidi unaweza usimpate na ukimpata atakuwa hayuko active kwa maana ya ajira ya uwanjani; atakuwa kwenye shughuli nyingine za utawala.

Columnist: Mwanaspoti