Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Haaland anakaribia kuivuruga historia ya mchezo wetu

Erling Haaland X Pep G Haaland anakaribia kuivuruga historia ya mchezo wetu

Mon, 16 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mara moja katika maisha? Labda Erling Haaland anaweza kuwa mtu wa namna hiyo. Muache Lionel Messi na kipaji chake kikubwa cha mpira. Sijawahi kuona. Zaidi ya Pele? Zaidi ya Diego Maradona? Inawezekana. Kwa mtazamo wangu.

Lakini, mkononi nina Erling Haaland. Alizaliwa miezi saba baada ya dunia kushangilia kuingia katika milenia mpya. Alizaliwa Julai, 2000. Haaland ameanza kunitia hofu. Anaweza kuwa mfungaji bora wa muda wote katika historia ya soka duniani.

Majuzi nilimuona Cristiano Ronaldo akishangilia bao lake la 901 katika soka. Mabao ambayo unajumlisha katika klabu zote za soka ambazo amewahi kucheza. Mabao ambayo unajumlisha katika kikosi chake cha timu ya taifa ya Ureno.

Lakini kuna huyu Haaland. Ananitisha. Anafunga kadri anavyojisikia. Anachonitisha zaidi ni kwamba popote unapohesabu mabao yake, basi huwa yanazidi idadi ya mechi ambazo amecheza. Mfano mdogo wa karibuni ni msimu huu tu. katika mechi tatu alizocheza amefunga mabao saba.

Hiki ni kitu cha kawaida kwake. Msimu wake wa kwanza tu aliweka rekodi ya kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja. Yaani wale wote washambuliaji hatari ambao tulikuwa tunawasifia England walikuwa hawajawahi kufanya kitu kama hicho. Alifunga mabao 36.

Subiri kwanza. Msimu wake wa kwanza Red Salzburg alicheza mechi 16 akafunga mabao 17. Huo ndio ulikuwa msimu pekee. Dortmund kwa msimu miwili alicheza mechi 67 akafunga mabao 62. Manchester City katika mechi 69 amefunga mabao 70.

Kule kwao Norway katika timu ya taifa amefunga mabao 32 katika mechi 35. Kule Norway hachezi na Messi wala Kevin De Bruyne. Jina kubwa pekee ambalo anacheza nalo ni Martin Odegaard. Ndio maana walimkwamisha kucheza michuano ya Euro iliyofanyika Julai, mwaka huu pale Ujerumani.

Haaland anatisha. Katika umri wa miaka 24 ina maana ndani ya miaka 10 ijayo atakuwa na miaka 34. Hapa tunazungumza ndio kwanza ametoka kutimiza miaka 24 miezi miwili iliyopita. Ana huu mwaka wa kufunga mabao na miaka mingine tisa kabla hajatimiza miaka 34.

Hatujui atakuwa na mabao mangapi wakati huo, lakini bado atakuwa hajatimiza umri wa Ronaldo. Huenda hadi wakati huo akawa na mabao 900. Hapo ni kama ataamua kuendelea kucheza katika ligi hizi za Ulaya. Vipi kama akienda Saudia Arabia ambako ligi tunafahamu ni nyepesi? Ina maswali mengi.

Lakini inaacha maswali mengi zaidi pale unapofikiria ni namna gani wakati huu ambapo anafunga mabao mengi zaidi ya idadi ya mechi amejikuta akicheza katika Ligi Kuu England. Ligi ambayo inadhaniwa kuwa ngumu kuliko nyingine zote duniani.

Kuna ugumu mkubwa unapokwenda kucheza usiku wa baridi Jumatatu dhidi ya Stoke City ugenini pengine kuliko kwenda Metropolitano kucheza na Atletico Madrid. Lakini Haaland anafunga kadri anavyojisikia katika ligi hii. Vipi akienda Hispania au Italia? Vipi kama angebaki Ujerumani?

Kinachonipa hofu zaidi ni namna ambavyo Haaland alivyo. Ni nadra sana kumkuta mshambuliaji mwenye umbo kubwa kama yeye halafu akawa na mbio za mchomoko kama yeye alivyo. Si unaona namna ambavyo kina Zlatan Ibrahimovic na Dimitar Berbatov walivyokuwa na uzito fulani hivi. Haaland hayupo hivyo.

Haaland mzuri wa miguu yote. Mzuri hewani. Anajua kukimbia nyuma ya adui. Anajua kupiga mashuti ya mbali. Kitu kibaya zaidi ni kwamba watu ambao wangeweza kumkabili walistaafu mpira. Kina Tony Adams, Nemanja Vidic, Jaap Stam, Paolo Maldini na wengineo wa zamani.

Sasa wanamkabili walinzi wa kati ambao hawana roho mbaya. Labda Haaland alipaswa kucheza katika kizazi kilichopita nyuma. Bahati nzuri kwake amejikuta katika kizazi hiki cha walinzi laini. Na zaidi ya kila kitu mchezo wenyewe nao umekuwa laini. Hatugusani sana. Hakuna ubabe sana.

Jinsi ambavyo akicheza na Arsenal huwa anapata wakati mgumu kwa Gabriel Magalhaes, ndivyo ambavyo alipaswa kukutana na wakati mgumu popote ambapo angekwenda. Hata hivyo walinzi kama Gabriel wametoweka katika soka kwa sasa.

Inanitia hofu kwamba huenda Haaland ataendelea kufunga kwa kadri anavyojisikia katika soka la kisasa. Inanitia hofu kwamba katika umri wa miaka 30 huenda akawa na mabao ambayo Ronaldo amefunga sasa hivi. Kitu gani kitamzuia?

Bahati mbaya wakati huo ambapo atakuwa amempita mabao Pele na Ronaldo huenda tusimkumbuke Haaland kama alikuwa mchezaji mahiri. Hapana, yeye tutamkumbuka kama mfungaji mahiri zaidi. Haaland hana mambo mengi uwanjani, lakini anafanya kile ambacho anaweza kukifanya. Basi.

Wenzake kina Pele na Ronaldo ukimjumlisha na Messi tutawakumbuka kwa mambo mengi uwanjani. Chenga, kanzu na udambwidambwi mwingi uwanjani. Haaland tutamkumbuka kwa mabao tu. Na kwa jinsi kizazi kijacho kitakavyokuwa tutapata wakati mgumu wa kumuelezea Haaland alikuwa mchezaji wa aina gani.

Kila utakapowaelezea wajukuu wa wajukuu wetu namna ambavyo Pele, Maradona, Messi, Ronaldo, Ronaldinho, Zidane na wengineo walivyokuwa mahiri kuliko Haaland, wao watakuja na namba ambazo zitamuelezea Haaland namna alivyokuwa mahiri kuliko hao ambao tumewatajia. Kisa? Mabao yake.

Kama akibaki na afya njema, basi Haaland atakaribia kuivuruga historia ya mchezo wetu. Na ukizingatia kwamba alikuwa anatoka Norway na sio Brazil, Argentina, England, Ufaransa, Hispania, Ujerumani au taifa jingine kubwa kisoka ambalo huenda nimelisahau basi Haaland atakuwa anatupa wakati mgumu kumuelezea.

Ilizoelekea kwamba wachezaji wakubwa wanatoka katika mataifa makubwa kisoka, lakini huyu atakuwa ametoka Norway na atakuwa amefunga mabao mengi kiasi ambacho tutashindwa kuwaelezea wajukuu wa wajukuu zetu alikuwa mchezaji gani uwanjani.

Columnist: Mwanaspoti