Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: West Ham United wanapopata jeuri ya kumtaka Hazard

Hazard Pic Nyota wa Real Madrid, Eden Hazard

Sun, 12 Dec 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mwingine ukiwa maskini hata wanyama wanakudharau. Mbuzi naye anakuja anakunusanusa halafu anaondoka zake. Dharau iliyoje. Akimuona mwanadamu tajiri anakaa mbali kidogo. Anahofia kushikwa na kuchinjwa.

Nimesoma mahala juzi West Ham wanamtaka Eden Hazard. Labda nikukumbushe. Hazard mwenye umri wa miaka 30. Kumbuka kwamba Hazard aliondoka Chelsea akiwa na miaka 28 tu. Ina maana miaka miwili iliyofuata anatakiwa na West Ham. Nini kimetokea?

Labda kama West Ham wangenunuliwa na tajiri fulani wa Kiarabu kama ilivyo kwa Newcastle United. Hapana. West Ham ni walewale tu. Wapo katika umiliki uleule. Hakuna kilichobadilika. Kilichobadilika ni maisha ya mchezaji mwenye, Eden Hazard.

Inadaiwa kwamba tajiri wa Real Madrid anataka Pauni 43 milioni wakati West Ham wanaamini Hazard ana thamani ya Pauni 25 milioni. Maisha haya. Leo Hazard anatakiwa na West Ham halafu kwa kiasi hicho cha pesa. Kutoka kununuliwa kwa Pauni 140 milioni miaka miwili iliyopita. Sahau kuhusu pesa. Kuna madaraja mangapi ambayo Hazard atavuka kwenda chini kama atachukuliwa na timu za usawa wa West Ham. Hajatakiwa na Arsenal. Hajatakiwa na Manchester United. Hajatakiwa na Tottenham. Hajatakiwa na Bayern Munich.

Nini kinatokea? Hazard anasumbuliwa na majeraha tangu alipotua Santiago Bernabeu. Amecheza mechi 55 tu katika misimu miwili. Fedheha iliyoje. Na hata wakati anacheza Hazard huwa anasumbuliwa na uzito fulani hivi. Kama ule ambao wakati fulani ulikuwa unamsumbua Ronaldo de Lima.

Kwanini majeraha yanasumbua sasa? Hatuwezi kuipinga kazi ya Mungu lakini kuna ukweli ambao huwa unajificha nyuma ya bahati za wachezaji. Kuna wachezaji ambao wakihama tu wanaharibu kila kitu. Kila kitu kinaanza kwenda mrama.

Wachezaji ambao wanakuwa wafalme walikotoka lakini wakibadilisha upepo maisha hayaendi sawa. Imewahi kuwatokea wengi huko nyuma lakini miaka ya karibuni nadhani utamkumbuka Fernando Torres. Alipohama Liverpool kwenda Chelsea kila kitu kikavurugika.

Huyu Torres ungeweza kusema mfumo wa Chelsea haukuwa mwafaka kwake, sawa, lakini vipi alipokwenda AC Milan? Hadithi ilikuwa ileile. Vipi aliporudi nyumbani kwake Atletico Madrid? Hadithi ilikuwa ileile. Hakuna kilichobadilika. Ni hadithi ya Philippe Coutinho. Alipohama kutoka Liverpool kwenda Barcelona kila kitu kikabadilika. Hakuwa tena Coutinho yule ambaye alitokea upande wa kushoto pale Anfield au katika uwanja mwingine wa soka. Mambo yalipokuwa ovyo alikwenda zake Bayern Munich akatwaa ubingwa wa Ulaya kwa nguvu za wenzake lakini kiwango chake kilikuwa cha kawaida. Akarudi tena Barcelona lakini bado tunaendelea kumuona akiwa yuleyule aliyeshuka kiwango. Siamini kama sasa ukimpeleka Tottenham au Newcastle au akirudi tena Liverpool anaweza kurudia maajabu yake.

Wakati mwingine maisha mzuri ni ndoto ambayo haupaswi kujitingisha. Inabidi uendelee tu kuiota miaka na miaka.

Labda haishangazi kuona kuna wachezaji huwa wanaridhika pindi wanapohusudiwa katika klabu moja. Hawa ndio akina Paolo Maldini, Francesco Totti, Matt Le Tisier na wengineo. Waliona isiwe shinda. Hawakutaka kuhama wakiwa katika ubora wao.

Kuna wale ambao wanahama wakati umri unapokuwa umewatupa mkono. Hauwezi kuwalaumu. Hawa ndio akina Steven Gerrard. Kina Frank Lampard. Akina Thierry Henry. Walionyesha ubora wao kwa muda mrefu katika timu moja. Walipoona mambo yamefika ukingoni wakaondoka zao. Hata kama walifeli au walicheza kawaida walikokwenda lakini tayari walishaanza dalili za kuonyesha mwisho huko walikotoka.

Rafiki yangu Hazard aliondoka Chelsea akiwa wa moto sana. Ilionekana kama vile anakwenda Santiago Bernabeu kwa ajili ya kuwa mrithi wa Ronaldo. Hapana, nimekosea. Namaanisha kwamba walau kufanya robo ya kile ambacho Ronaldo alikifanya pale.

Sababu kubwa inaweza kuwa majeraha yake. Lakini wakati mwingine imani ni kitu cha ajabu pia. Kuna ambao watajiuliza “kwanini alipokuwa Chelsea hakusumbuliwa na majeraha?” Jambo hilo linaangukia katika imani. Labda Madrid haikuwa kwa ajili yake. Hata yeye mwenyewe si ajabu kuna nyakati ambazo anaweza kukiri kimya kimya bila ya kumwambia mtu kwamba huenda Madrid haikuwa kwa ajili yake.

Hazard yule ambaye alikuwa anaufanya mpira anavyotaka pale Stamford Bridge leo anauzwa kwa pauni 43 milioni tu? Anatamaniwa na klabu ambazo hazichezi hata katika michuano ya Ligi ya Mabingwa? Kweli maisha yanaenda kasi.

Columnist: Mwanaspoti