Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Wacongo wawaduwaza Wacongo wenzao Taifa

TP Mazembe Squad Wacongo wawaduwaza Wacongo wenzao Taifa

Thu, 23 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Picha za mwisho mwisho katika pambano la juzi, kwa sisi tuolitazama mechi katika televisheni zilimuonyesha kiungo, Mukoko Tonombe akiwa anashangaa. Alionekana akiwa haelewi vizuri kilichotokea. Rafiki zake wa zamani kina Kibwana Shomari walimliwaza lakini haikuwezekana.

Kuanzia pale alipoondoka Yanga maisha yameenda kasi zaidi. kwa mfano, sehemu ya kiungo, yeye na Gift Mauya ilikuja kutia nguvu kubwa baada ya GSM kuanza matanuzi ya pesa Jangwani. Lakini kuanzia pale Yanga imekwenda juu zaidi.

Katika eneo hilo, sio yeye wala Gift Mauya walioanza katika mechi hiyo licha ya kwamba wanacheza katika timu tofauti. Wote waliingia baadaye. Lakini kwa Yanga kuna sura mpya zaidi. Khalid Aucho, Yannick Bangala, Sure Boy, Mudathir Mudathir wote wamekuja kuking’arisha kiungo chao.

Lakini zaidi ni katika timu yenyewe wamekuja Wacongo ambao alipishana nao kwa miezi michache. Bangala, Fiston Mayele, Djuma Shaaban, Jesus Moloko na Tuisila Kisinda. Wameinyanyua timu kutoka kwa Ditram Nchimbi hadi kwa Mayele. Timu yo imebadilika.

Achilia mbali Wacongo hawa Yanga imeongeza wakali wengine. Kwa mfano, wachezaji wawili waliofunga mabao mawili ya kwanza ya Yanga wote wametua klabuni hapo katika dirisha la Januari. Kenneth Musonda pamoja na Mudathir Yahya.

Nadhani hili lilikuwa linamshangaza Mukoko. Lakini zaidi upande mwingine wa shilingi maisha yamebadilika. TP Mazembe aliyokwenda kuikuta leo sio ile ambayo ilitamba katika mpira wa Afrika. Kina Mbwana Samatta, Reinford Kalaba, Jean Kasusula, Nathan Sinkala, Tresor Mputu na wengineo, sio tena kikosi sehemu ya kikosi cha Mazembe.

Nini kilitokea? Yanga ilifanikiwa kugeuza kibao katika namna ile ile ambayo iligeuziwa kibao nchini Tunisia wiki iliyopita. Katika pambano lile, ndani ya dakika 16 tayari Monastir ilimaliza mechi pale Tunis. Yalikuwa mabao mawili ya haraka haraka kupitia mipira iliyokufa.

Juzi, ndani ya dakika 10 Yanga ilimaliza mechi. Katika mabao yao matatu ni bao moja tu ambalo Wacongo hawakuhusika. Bao la Mudathir ambaye alivunja mtego wa kuotea baada ya kupokea pasi kutoka kwa nyota wa Zambia, Musonda.Vinginevyo Mazembe ilimalizwa na Wacongo wenzao ambao walikuwa katika ubora wao juzi. Bao la kwanza la Musonda lilitokana na uhodari mkubwa wa mpira wa adhabu uliopigwa na Djuma Shaaban. Ilipigwa kiumaridadi mkubwa kama Yanga ilivyopigiwa wiki iliyopita na Monastir.

Wiki ile kuna wachambuzi waliuzungumzia kuhusu ufupi wa mabeki wa Yanga hasa Dickson Job lakini safari hii hawazungumzii kama Mazembe walikuwa wafupi. Kitu kikubwa katika mipira hii wakati mwingine sio kimo. Ni ‘timing’ sahihi ya mabeki kushughulika na mpira. Wakati mwingine unamsifu na mfungaji pia.

Baada ya hapo Yanga ilitegemea zaidi mipira ya kushtukiza kwa ajili ya mashambulizi. Fiston Mayele hakufunga lakini alikuwa ni Mcongo aliyewaletea shida Wacongo wenzake katika namna ambavyo alikuwa na uwezo wa kukaa na mpira lakini pia kuchomoka kwa kasi.

Kupitia yeye ndipo lilipopatikana bao la Mcongo. Kombinesheni ya bao kutoka Kinshasa ambalo lilifungwa katika Uwanja wa Temeke. Kasi ya Mayele halafu akapiga pasi murua kwa Tuisila ambaye wote tunafahamu ana kasi kubwa.

Tuisila alitazamana na golikipa lakini kama angekosa tusingeshangaa sana. Amekuwa akishindwa kufanya maamuzi sahihi wiki baada ya wiki. Kama angekuwa ana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kwa ufasaha kama alivyofanya juzi basi si ajabu angekuwa mchezaji hatari zaidi.

Tayari anajikuta uwanjani akiwa mchezaji mwenye kasi kuliko wachezaji wengine 21 waliopo uwanjani. Tatizo lake ni kushindwa kuchukua maamuzi sahihi katika wakati sahihi. Sehemu ya kupiga kama vile angebutua mpira nje. Sehemu ya kupiga pasi nzuri ya mwisho yeye anachukua maamuzi mengine anayoyafahamu yeye tu.

Juzi alimaliza matumaini ya Wacongo wenzake kupata sare kwa sababu alifanya kila kitu kwa usahihi. Alikimbia katika nafasi kwa usahihi kwa ajili ya kupokea mpira uliokuwa katika miguu ya Mayele. Akamalizia kwa usahihi na katika nyakati sahihi ambazo Mazembe walipaswa kumalizwa.

Kwa ujumla ilikuwa mechi nzuri ya soka. Kama ilivyokuwa katika pambano dhidi ya Monastir, licha ya Yanga kufungwa lakini ilicheza vema kiasi cha kupunguza maneno kwa mashabiki wao.

Baada ya kufungwa mabao mawili ya haraka haraka walicheza kikomavu katika namna ambayo walionyesha wana hadhi ya kushiriki michuano yenyewe.

Lakini juzi pia walionyesha ukomavu katika maeneo mengi kiasi kuwatia moyo mashabiki wao walau baada ya muda mrefu kwa sasa wana kikosi ambacho kinaweza kushindana katika michuano kama hii. kushinda au kufungwa ni jambo moja lakini kucheza vema katika maeneo mengi ya mchezo ni jambo jingine.

Kundi lao limekaaje? Ushindi wa Yanga juzi ulitiwa chumvi na ukweli katika hali ya kushangaza Monastir ilisafiri mpaka Bamako na kutoa sare na timu ya Real Bamako. Nilidhani Waarabu walikuwa na nafasi nzuri ya kushinda pambano hilo lakini wakaishia kwa sare tu.

Hii ina maana wamevutika mpaka pointi nne tu ambazo zinaweza kufikika kirahisi na Yanga na Mazembe na hata Real Bamako kama watacheza vizuri zaidi siku za usoni. Kundi linaonekana kukosa mwenyewe.

Kinachotakiwa kwa Yanga ni kupata pointi sita katika mechi zake mbili zijazo dhidi ya Real Bamako.

Moja itakuwa wikiendi hii pale Bamako wakati nyingine itakuwa wikiendi ijayo pale Temeke.

Yanga inahitaji pointi nne au sita katika mechi mbili zinazofuata ili ajiweke katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali.

Columnist: Mwanaspoti