Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Utamu wa filamu ya Barbra vs Bodi ya Ligi na TFF

CEO Babra Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba (C.E.O), Barbara Gonzalez

Wed, 15 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kwa sababu pambano lenyewe la Simba na Yanga lilimalizika kwa suluhu ya bila kufungana, utamu wa mechi unakufa haraka zaidi. Hakuna wa kumtambia mwenzake. Ndani ya saa 24 zijazo hakuna atakayeongelea pambano.

Kitu kizuri zaidi ni kwamba mwamuzi mwenyewe, Herri Sasii hakuharibu mechi yenyewe. Hakutoa penalti ya uongo, hakutoa kadi nyekundu ya uongo. Hakufanya kitu chochote ambacho kiliashiria alipendelea upande mmoja. Mechi yenyewe imekufa kibudu. Lakini ghafla likaibuka pambano jingine la nje ya uwanja. Pambano ambalo linaweza kuvutia zaidi pengine kuliko ile mechi. Pambano kati ya mtendaji Mkuu wa Simba, Barbra Gonzalez dhidi ya Bodi ya Ligi. Wakati mwingine unaweza kusema dhidi ya TFF pia.

Indaiwa mwanadada huyu mrembo alizuiwa kuingia Uwanja wa Mkapa akiwa na familia yake. Tuanzie mbele au turudi nyuma? Nadhani turudi nyuma kidogo kabla ya kuanza mbele. kulikuwa na kutazama vibaya kati ya Barbra na watu wa Bodi kuelekea pambano.

Kisa? Mkataba wa GSM na Bodi ya Ligi ambao unazitaka klabu za Ligi Kuu kuvaa jezi ambazo zina logo ya GSM. Hawa majamaa wameingiza kiasi cha Sh2.1 bilioni wakiwa ni wadhamini wapya wa ligi kando ya NBC. Simba hawataki. Hawataki kuvaa logo ya GSM wala mechi zao kuwa na mabango ya GSM. Wanaamini kuna sheria au kanuni zimevunjwa. Kuna maslahi binafsi kati ya wapinzani wao Yanga na GSM. Sielewi nani yupo sahihi. Sielewi kama TFF hawakulitazama hili mapema na kujua kwamba linaweza kuanzisha kasheshe.

Kitu ninachoelewa, kwa mtazamo wangu binafsi ni kwamba katika suala hili kuna ukweli (fact) na kuna hali halisi (reality). Simba kama Simba wanaweza kuwa wanazungumzia ukweli, lakini klabu nyingine zote hazitakwenda kwa Simba kwa sababu zitaangalia zaidi hali halisi.

Hali halisi ni ipi? Klabu zinajua zilikotoka. Klabu zinataka pesa. Kuvaa tu logo na mabango kuwekwa uwanjani kisha wao wanapata pesa? Jambo hilo haliwasumbui. Haishangazi kuona timu nyingi zimeanza kuvaa logo ya GSM. Ni vita ambayo Simba wa-tashinda kivyao lakini sio kwa kuwajumuisha wengine.

Hata Azam wanaweza kuvaa GSM. Uhusiano wa Yanga na Azam ni mkubwa na mzuri kwa sasa. Matajiri wapya wa Yanga na Azam ni marafiki. Tajiri wa zamani wa Yanga, bwana Yusuph Manji ndiye ambaye alikuwa hana uhusiano mzuri na Azam. Zama hizo zimepita.

Turudi kwa Barbara. Kuanzia hapo huyu mrembo akashinikiza watu wa Simba wasihudhurie mkutano wa awali na waandishi wa habari endapo kungekuwa na logo za GSM katika mabango ya mkutano. Na kweli. Watu wa Simba walipofika hawakukaa nusu saa. Wakaondoka zao.

Mechi ikaingizwa katika ‘tension’ kubwa. Wengine tuliingiwa hofu kwamba huenda hata pambano hilo lisingefanyika. Shukrani kwao watu wa Simba wakaamua kucheza ingawa bila ya mabango. Hata hivyo kulikuwa na kitu kinasubiriwa. Watu wa Bodi wa Ligi na Barbara walikuwa hawatazamani vizuri kuelekea katika mechi hii. Dada yetu alipojitokeza katika mlango wa kuingilia waheshimiwa akiwa na kadi maalumu ambazo hazikuwa na majina ya watoto, nadhani watu wa Bodi ya Ligi waliona huo ndio ulikuwa wakati mwafaka wa kulipa kisasi. Wakamzuia. Kilichoendelea hapo wengi hatufahamu hasa, lakini inadaiwa kulikuwepo na kurushiana maneno makali baina ya watu wa getini na dada yetu. Haya yote yasingetokea kama mambo mawili yangetokea kabla ya tukio. Huenda yasingetokea kama Simba wangekuwa na uhusiano mzuri na TFF kuelekea mechi hii. Uhusiano wao upo katika rehani. Hapohapo jambo kama hili lingeweza kutokea kwa mtu kama Fredrick Mwakalebela wakati ule uhusiano wa Yanga na viongozi wake ukiwa katika rehani na TFF.

Barbara inawezekana alikuwa hana tiketi maalumu za watoto wake, lakini ni wazi kwamba alikuwa ameingia katika anga za watu wa Bodi wa Ligi. Watanzania tuna ustaarabu wengi na huwa tunaoneana haya. Inawezekana ni kweli kwamba Barbara alikuwa hayupo sahihi, lakini kama angekuwa na uhusiano mzuri na watu wa Bodi ya Ligi, basi si ajabu mambo yangekwenda sawa.

Mara ngapi kanuni na sheria zimevunjwa kwa ajili ya kuwalinda watu maarufu? Imetokea mara kibao. Ni vile tu Barbara hana uhusiano mzuri kwa sasa na TFF. Na licha ya hasira zake si ajabu kwa nilichosikia ni kwamba huenda mwenyewe akaingia kikaangoni. Kitu kingine ambacho huenda kimesababisha haya ni labda tabia ya kujenga mazoea kwa watu wetu waheshimiwa. Mara nyingi kila kitu kinakwenda kiulaini kwao kwa sababu wamezoea kuona kanuni nyingi zinavunjwa kwa ajili yao. Watu wakisimamia kanuni basi inakuwa shida na wanaambulia matusi. Ni pale watu wanaposimamia kanuni ndipo linapojitokeza lile neno la ‘unajua mimi ni nani?’ Ni miongoni mwa kauli za kipuuzi zinazotolewa na watu maarufu, watu wenye pesa na watu wenye mamlaka. Trafiki anamsimamisha mtu maarufu na kutaka kumpiga faini ya kuendesha gari kwa swali na ghafla utasikia swali hili.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz