Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Upande mwingine wa rafu mbaya aliyochezewa Bangala

Bangala Yanga Kl Yannick Bangala

Wed, 24 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezaji mwingine wa Yanga, Yannick Bangala alichezewa rafu mbaya wikiendi iliyopita katika pambano dhidi ya Coastal Union. Video ya marudio ya rafu ile ilisambaa mitandaoni kwa haraka kama tu ilivyosambaa rafu ya kindava ya Henock Inonga dhidi ya Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ katika pambano la watani hivi karibuni.

Sijui kama imetokea kuwa bahati mbaya au sijui kama wachezaji wa Yanga wanapaniwa. Kilichochekesha zaidi ni uamuzi wa waamuzi. Nilijadili kuhusu rafu ya Inonga, lakini sasa ni wakati wa kujadili rafu aliyochezewa mchezaji mstaarabu uwanjani, Bangala.

Kuna sura tatu hapa. Kwanza ni uzembe wa mwamuzi Raphael Ikambi. Kwanini Albano Mtenje hakupewa kadi nyekundu. Ilikuwa ni rafu ya kadi nyekundu. Mwamuzi alikuwa ameona na ndio maana alitoa kadi ya njano. Afadhali angedai kwamba hakuona kabisa tungeweza kumuelewa.

Ni kama ilivyokuwa kwa Inonga dhidi ya Sure Boy. Mwamuzi wa siku ile Eli Sasi ni bora angesema hajaona kuliko kutoa kadi ya njano. Tukio la juzi lilikuwa na mambo mawili. Ama kutoona na hivyo usitoe kadi yoyote au utoe kadi nyekundu moja kwa moja. Hakukuwa na chaguo la kadi ya njano. Mchezaji wa Coastal alikuwa amekimbia kwa hatua tatu mguu mmoja ukiwa juu kwa lengo la kumdhuru Bangala.

Kwanini mwamuzi hakutoa kadi nyekundu? Nadhani ni kwa sababu angelazimika pia kumtoa kwa kadi nyekundu Bangala ambaye baada ya rafu alinyanyuka na kwenda kumsukuma Mtenje. Wote wawili wangelazimika kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Kwa ajili ya kubalansi mambo, huku akihofia kumtoa Bangala nje ndipo alipolazimika kuwapa wote kadi za njano. Uamuzi mbovu.

Hisia zinaniambia kama Bangala asingemsukuma mchezaji wa Coastal mpaka chini basi huenda labda mchezaji wa Coastal angetolewa nje kwa kadi nyekundu. Tatizo unamtoaje nje na mchezaji wa Yanga ambaye mashabiki wanaamini kwamba amejibu mapigo kwa sababu ya rafu aliyochezewa ni

mbaya. Waamuzi wetu wameishi katika maisha ya kubalansi kwa muda mrefu sasa. Ni kama tu Eli Sasi alivyobalansi kwa kutowatoa nje kwa kadi nyekundu Inonga na Sure Boy. Kisa? Kuna kanuni maalumu za mashabiki linapokuja suala la mechi hiyo.

Kwa mchezaji mwenyewe aliyecheza rafu nadhani amecheza rafu ya kizamani. Rafu ambayo watu wengi tulishaisahau katika soka.

Hata wachezaji wakorofi kina Kelvin Yondani huwa hawachezi rafu hiyo siku hizi. Hata mechi za mitaani rafu hiyo imetoweka. Imetoweka kwa sababu sheria zimekuwa kali.

Waamuzi kama Ikambi ndio ambao wamesababisha rafu hizo ziendelee. Waamuzi wengine wameziondoa kwa sababu kwa mujibu kwa sheria, hata wachezaji wenyewe wanajua kwamba rafu ile adhabu yake ni kadi nyekundu. Nadhani hata mchezaji wa Coastal Union alifahamu kwamba rafu ile ilistahili kadi nyekundu.

Mchezaji anayecheza rafu ile akili yake ujue ipo katika soka la Tanzania tu. Hajajiandaa kucheza nje ya mipaka yetu. Hakuna mahala kwingine anakoweza kucheza soka halafu rafu kama ile ikakubalika. Imebaki Tanzania tu ndipo rafu kama ile au ya Inonga zinaweza kukubalika. Kwingineko hapana.

Inasemwa kwamba Coastal Union imekuwa timu ambayo inapata uamuzi mzuri kwa sababu waamuzi wanawahofia viongozi wakubwa. Coastal ni timu pendwa ya rais wa TFF, Wallace Karia lakini pia ni timu ya mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto ambaye juzi alikuwepo uwanjani wakati Bangala akichezewa rafu ile.

Kwa hali ilivyo sasa na kwa namna ambavyo waamuzi wamekuwa wazembe, tulipaswa kutengeneza kanuni ambayo uamuzi wa mwamuzi haupaswi kuwa wa mwisho. Ulaya Ikambi angeitwa kwenda katika VAR kwa ajili ya kujiridhisha tena hata kama awali alitoa kadi ya njano.

Hapa kwa sababu hatuna na VAR basi ingetengenezwa kanuni ambayo hata kesho yake uamuzi mpya ungeweza kuchukuliwa baada ya kamati fulani kupitia upya rafu iliyochezwa na hivyo kumfungia mchezaji wa Coastal Union mechi nyingi kuliko adhabu ya kadi ya njano aliyopewa.

Tupo katika nyakati ambazo Azam TV inaonyesha vyema matukio kama yale na wangepaswa kuaminiwa katika kutumia video zao kupitia uamuzi mwingine kama huu.

Kitu ambacho kinapaswa kubaki kama kilivyo ni matokeo ya mechi yenyewe hata kama mwamuzi aliamua tofauti kuhusu mabao.

Hali ikiendelea hivi wachezaji wataendelea kujiona salama pindi wanaponufaika na uamuzi wa ajabu wa waamuzi. Wanapaswa kucheza kwa tahadhari wakifahamu kwamba wakati mwingine uamuzi wa mwamuzi unaweza usiwe wa mwisho kama ukifanya ujinga uwanjani. Hatuna VAR lakini kuna kitu tunaweza kufanya.

Kwanini bahati wachezaji wa Yanga wanachezewa ubabe? Huwa inatokea timu inapokuwa nzuri. Popote duniani timu nzuri inajikita katika kucheza soka safi halafu wapinzani wanajikita katika kuwadhibiti. Hauwezi kuwa na timu nzuri inayofurahia soka halafu wachezaji wake wakajikita katika kucheza rafu.

Mwanzoni mwa msimu uliopita Simba walilalamika wachezaji wao kuchezewa rafu za mara kwa mara. Safari hii ni Yanga. Wote hawa wanajikuta kuwa wahanga wa ubora wao.

Matukio kama haya yatawatokea wakikutana na Tanzania Prisons au timu nyingine ambazo zinapenda kucheza kibabe katika kuwadhibiti wapinzani wao.

Ni jukumu la mwamuzi kuwalinda wachezaji bora uwanjani. Wakati mwingine wapinzani wanatafsiri kuwa kucheza kwa nguvu ni kucheza rafu. Sio sahihi.

Nazijua timu ambazo zimeweza kujikita kucheza vizuri na zikapata matokeo dhidi ya Simba au Yanga. Kagera Sugar ni miongoni kwa timu hizi. Pongezi kwao. Hawana muda wa kucheza rafu za kijinga.

Columnist: Mwanaspoti