Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Ugonjwa wetu jinsi, Yanga walivyokufa

Yanga Na Nuksi Ugonjwa wetu jinsi, Yanga walivyokufa

Wed, 15 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mei 15, 2021 iliwachukua Kaizer Chiefs dakika 34 tu kumaliza pambano dhidi ya Simba. Ilikuwa safari yangu ya mwisho kushuhudia timu ya Tanzania ikicheza ugenini. Juzi ilikuwa safari nyingine. Iliwachukua Monastir dakika 16 tu kumaliza pambano dhidi ya Yanga.

Kwanini nimekumbuka pambano la Simba? Kwa sababu kuna ugonjwa ambao timu zetu zinaumwa. Ugonjwa wa kushindwa kudhibiti mipira ya adhabu au mipira iliyokufa. Pambano lile la Kaizer Chiefs Simba ilifungwa mabao rahisi ya vichwa kwa mipira ya kona. Shukrani kwa Eric Mothoho na Samir Nurkovic.

Yanga nao iliumwa ugonjwa huuhuu juzi katika Uwanja wa Olimpiki Prasde. Ilifungwa mabao mawili ya vichwa na Watunisia huku wafungaji wakiwa huru. La kwanza lilifungwa la Mohammed Saghraoui wakati la pili lilifungwa na Boubacar Traore ambaye anacheza katika Timu ya Taifa ya Mali.

Labda ligi yetu haitufundishi kitu kuhusu mipira iliyokufa. Juzi tu Simba ilifungwa bao pekee na Horoya kwa mipira iliyokufa.

Wachezaji wetu hawaushambulii mpira unaopigwa katika kona au faulo. Hiki ndicho kitu kikubwa ambacho kiliiponza Yanga katika pambano la juzi. Basi. Mipira iliyokufa ndio iliyokuwa tofauti pekee kati ya Yanga na Watunisia na mara nyingi imekuwa tofauti pekee kati ya timu zetu na wageni.

Nilihoji kama kwanini Yanga haikujiandaa na mipira hiyo nikaambiwa kwamba ilijiandaa. Nikaambiwa awali Kocha Nasireddine Nabi alipanga kumuanzisha Mudathir Yahya badala ya Khalid Aucho, lakini baadaye akabadili mawazo na kumuanzisha Aucho kwa sababu ni mrefu kwa Mudathir. Haikusaidia lolote.

Kama ilivyokuwa kwa Simba juzi, mpigaji wa kichwa alikuwa huru. Inasemwa ni kwa sababu ya urefu wake lakini ukweli ni kwamba wachezaji wa namna hii walau huwa wanasukumwasukumwa ili wasiwe huru zaidi. Hata hivyo, Traore alijikuta akiwa huru.

Bao la pili mchezaji aliyeusogeza mpira kwa mfungaji alikuwa amekabwa na Dickson Job. Job alikuwa amemfikia mpinzani katika mabega tu. Hakukuwa na maajabu makubwa kutoka kwa mabeki wala wachezaji wa viungo katika kuzuia hatari ya mipira iliyokufa. Mbaya zaidi katika kona uzuiaji wa Yanga katika mipira ya kona ni ule wa kulinda nafasi na sio kucheza mtu na mtu.

Vinginevyo baada ya hapo Yanga iliukamata mchezo katika maeneo mengi hasa eneo la kiungo. Watunisia waliamua kubaki nyuma kidogo na Yanga ikawa watengenezaji wakubwa wa mipango kuliko Monastir. Kuna mahala kidogo huwa kunaiangusha Yanga.

Yanga ina mawinga wa kawaida hasa anapokosekana Bernard Morrison. Jesus Moloko na Tuisila Kisinda ni mawinga wa kizamani ambao mchezo wao unategemea kwenda pembeni na kupiga krosi. Mawinga wa kisasa kama kina Bukayo Saka huwa wanaingia kati. Kuna ukosefu wa ubora katika maeneo ya pembeni pale mbele kwa Yanga.

Baadaye alitoka Tuisila Kisinda kisha akatoka Moloko. Aziz Ki akaenda kulia na Farid Mussa akaja kucheza kushoto. Ukijumlisha na kutolewa kwa Shomari Kibwana na nafasi yake kuchukuliwa na Joyce Lomalisa halafu kuingia kwa Kenneth Musonda pia kuliibadili Yanga kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, hakukuwa na mabadiliko ya matokeo.

Kuna mambo ambayo Nabi ameanza kulalamikiwa na watu. Kwanini hampangi Lomalisa katika nafasi yake na badala yake anampanga beki wa kulia katika nafasi ya kushoto? Mwenyewe anadai Kibwana ana kasi kuliko kina Lomalisa na David Bryson, lakini ukweli ni kwamba Kibwana hana madhara makubwa katika kushambulia.

Lakini pia Tuisila ameshindwa kuonyesha makali yake kila kukicha lakini hata hivyo Nabi ameendelea kumng’ang’ania. Ni tatizo. Musonda alipoingia alionyesha makali kwa sababu ana kasi na nguvu, lakini pia kumbe ana uwezo wa kucheza sambamba na Fiston Mayele kwa sababu ya kasi yake. Anaweza pia kutokea pembeni.

Pambano lilipomalizika waandishi wa habari wa Tunisia walimuandama kocha wa Monastir wakidai Yanga ilikuwa bora kuliko wao. Kocha mwenyewe alikiri jambo hilo lilikuwa ni kweli na akashangaa namna ambavyo timu yake ilipata mabao mepesi ya haraka haraka kabla ya mechi kuwageukia.

Na sasa licha ya Yanga kuonyesha mchezo mzuri, na wao wamejikuta wakikabiliana na kibarua kilekile ambacho kinawakabili watani zao Simba. Wikiendi hii itakuwa ya kuamua hatima ya uhai wa kundi lao. Mnyama atakuwa akimkaribisha Raja wakati Yanga itaikaribisha TP Mazembe.

Juzi nilieleza kibarua ambacho kinamkabili Mnyama. Hatuhitaji kurudia sana lakini kwa kiasi ni kibarua ambacho kinaikabili Yanga hata kama kwa nje unaweza kudhani Raja ni bora kuliko Mazembe. Ukweli ni kwamba katika miaka ya karibuni Simba imekuwa ikijua kuutumia vizuri Uwanja wa Mkapa kuliko Yanga.

Na sasa Yanga italazimika kuondoka na pointi tatu dhidi ya Mazembe katika pambano la Jumapili. Mazembe ya sasa sio ile ya kina Mbwana Samatta, Reinford Kalaba, Stoppila Sunzu, Robert Kidiaba, Jean Kasusura, Tresor Mputu na wengineo. Lakini bado imepata matokeo katika mechi ya kwanza.

Kila kitu kinafanana na mtani. Ikipata sare bado itakuwa mbaya. Katika hatua ya makundi haupaswi kupata pointi moja katika mechi mbili. Lakini pia baada ya hapo italazimika kupata pointi ugenini dhidi ya Real Bamako ambayo haionekani kuwa timu imara.

Kocha Nabi anapaswa kuzichanga karata zake vyema kwa sababu michuano hii ni kipimo kikubwa kwake. Yanga kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu haijawahi kuwa habari kubwa Tanzania kwa sababu tayari ilishachukua mataji 27 kabla hajafika. Ni katika michuano kama hii ndipo atapimwa uwezo wake zaidi hasa kwa kuzingatia Yanga inaamini wana kikosi chenye ni kizuri.

Kama kuna kitu kinatia presha haraka zaidi katika soka letu ni wikiendi inayokuja. Waingereza wangeweza kuiita Super Weekend basi ni michezo hiyo miwili. Bahati iliyoje kuwa na mechi mbili kubwa za CAF ambazo zinaweza kuamua hatima ya wakubwa wetu katika michuano hii. Jumamosi Simba na Raja, Jumapili Yanga na TP Mazembe. Haitokei mara nyingi katika maisha ya soka letu.

Columnist: Mwanaspoti