Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Ubishi wa kujaza uwanja wa Mkapa ni kichekesho kingine

Uwanja Wa Mkapa DSM Ubishi wa kujaza uwanja wa Mkapa ni kichekesho kingine

Thu, 5 May 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mitandaoni wakubwa wamekuwa wakitambiana kuhusu uwezo wa kujaza Uwanja wa Mkapa katika mechi zao. Upande ule wanadai kwamba wao ni wababe. Upande huu pia wanadai kwamba wao ni wababe. Siku hizi tuna vita nyingi za kila aina. Tunaishi katika dunia ya mitandao.

Watu wakishamaliza kubishana nani zaidi kati ya Shomari Kapombe na Djuma Shaban wanahamia katika ubishi mwingine. Halafu unaibuka ubishi mwingine. Halafu unaibuka ubishi mwingine pia. Na sasa wanabishana nani anajaza sana kati ya Simba na Yanga. Na wasemaji wao pia wanabishana.

Rafiki zangu Haji Manara wa Yanga na Ahmed Ally wa Simba wameingia katika ubishi wa kutaka kuonyeshana umwamba wa nani anaweza kupiga promo kubwa ya kuwapeleka mashabiki kwa wingi katika Uwanja wa Mkapa. Kiasi hiki ni kichekesho.

Wanachokosea zaidi ni kushindwa kujiuliza. Kwanini tumefikia katika huu ubishi? Ni dalili mbaya kwa mpira wetu. Simba na Yanga hawakupaswa kuwa katika mjadala huu. Walipaswa kuwa katika mjadala wa kupunguza mashabiki uwanjani. Walipaswa kuwa katika mjadala wa kuzuia idadi kubwa ya mashabiki wasiende uwanjani.

Kwanini? Wana mashabiki wengi ambao hawaendi uwanjani kwa sababu za kizembe. Mashabiki wa Simba na Yanga waliopo wilaya ya Temeke tu wanaweza kuujaza uwanja wenyewe. Tuulizane sababu za msingi za wasemaji wa timu hizi kupiga debe ili mashabiki waende uwanjani.

Kwamba kwa sababu mechi hizi zinaonyeshwa katika televisheni ndio maana mashabiki hawaendi uwanjani ni uongo. Ulaya mechi zinaonyeshwa katika televisheni na tiketi za kwenda uwanjani zinaisha. Uwanjani kuna raha yake. Kwa Tanzania uwanjani kuna karaha nyingi kuliko raha na ndio maana mashabiki wamekacha.

Na wanapokacha wanakwenda katika baa au kumbi ambazo wanapata raha zaidi. Wanatazama mpira wa Uwanja wa Mkapa ambao unaonyeshwa vyema na Azam TV. Hapo hapo wanaweza kutazama pambano la Manchester City dhidi ya Liverpool linaloonyeshwa katika televisheni nyingine. Lakini hapohapo wanaweza kuendelea kupata vinywaji na starehe nyingine.

Tanzania mpira ni karaha. Inaanzia katika usafiri wa kwenda uwanjani. Barabarani foleni zilizopitiliza. Unajikunja katika daladala la Tegeta kuelekea Mbagala ili ushuke zako Uwanja wa Mkapa. Unafika Uwanja wa Mkapa ukiwa hoi na tiketi yako mkononi.

Hata hivyo licha ya kuwa na tiketi yako haikukalishi katika siti yako. Unakuwa na tiketi mkononi lakini bado unakuwa na vita ya kuingia uwanjani. Unapambana na mbwa wa Polisi getini, unasukumwa na makomandoo wa mlangoni. Mpaka wakati unaingia ndani tayari umeshachafuka vilivyo. Unahema huku ukiisaka siti yako.

Majuzi nilikuwa Ulaya nikitazama mechi za Ligi ya mabingwa nikakumbushwa namna gani ambavyo mpira ni starehe. Real Madrid dhidi ya Chelsea Santiago Bernabeu. Atletico Madrid dhidi ya Manchester City. Barcelona dhidi ya Frankfurt. Mpira ulikuwa starehe hasa.

Mashabiki wanajikusanya nje ya uwanja wanaimba huku wakiwa hawana wasiwasi wa kuingia uwanjani. Wanakunywa, wanakula, wanaimba. Wanaingia uwanjani dakika kumi au ishirini kabla ya pambano kuanza. Hakuna presha yoyote. Mwisho wa siku unaona wazi kwamba mpira ni starehe.

Tungekuwa katika hali hii naamini mashabiki wengi wangekuwa wanaenda Uwanja wa Mkapa kiasi cha klabu hizi kulazimika kuzuia mashabiki wasiende uwanjani mpaka kiwango kilichopitiliza. Mashabiki wa Temeke tu wangetosha kuujaza uwanja.

Kinachonichekesha ni namna ubishi huu ni pale ninapojiuliza ni kitu gani kinabishaniwa? Kwamba kuna mashabiki wa upande fulani hawana hela? Kwamba mashabiki wa timu fulani hawana mapenzi na timu yao zaidi ndio maana hawaendi uwanjani?

Wote tunafahamu namna ambavyo mashabiki wa Simba na Yanga ni wanazi wa timu zao. Tunaweza kuhoji uhalalinwa mapenzi yao kwa Simba na Yanga? Nadhani tusijadili sana suala hili. Tujadili kwanini mashabiki hawapendi kwenda uwanjani?

Zamani Uwanja wa Mkapa ulikuwa unatapika. Hakukuwa na televisheni wala starehe za nje na ndani ya uwanja. Hata hivyo mashabiki walikuwa hawana chaguo jingine zaidi ya kwenda uwanjani. Kwa sasa lazima tutambue kwamba ushindani mkubwa wa kibiashara. Soka pia ni biashara.

Lazima tujue kwamba mashabiki wana machaguo mengi na lazima huduma katika viwanja vya soka ziimarishwe ili kushinda soko jingine ambalo katika lugha inayoeleweka ni ushindani wa mechi nyingine za kimataifa zinazoonyeshwa katika televisheni. Mfano ni Ligi Kuu ya England.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukiwachukulia wateja (mashabiki) kimasikhara na sasa tunajiuliza mashabiki wamekwenda wapi kiasi cha kujisifu pindi uwanja unapojaa. Ni kitu kinachochekesha kidogo. Badala ya kujiuliza wapi tulipojikwaa sisi tunajiuliza wapi tulipoangukia. Na kila kitu huwa tunakiingiza katika ubishi wa mitandaoni.

Columnist: Mwanaspoti