Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Tusimgeuze Samatta kuwa malaika na shetani

Samatta 1?fit=800%2C455 HISIA ZANGU: Tusimgeuze Samatta kuwa malaika na shetani

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

NILIKUWA natazama pambano la Kenya dhidi ya Misri pale Nairobi. Nikamnong’oneze jirani yangu na kumkumbusha kitu kwamba Wakenya wako mbali kisoka kuliko sisi lakini hawana mchezaji wa kariba ya Mbwana Samatta katika safu ya ushambuliaji.

Nikamnong’oneza pia kwamba hata majirani zetu wengine wanaotutambia katika soka hawana mshambuliaji kama Mbwana Samatta. Katika maeneo mengine hatuna wachezaji kama wao lakini pale mbele Samatta yuko mbele.

Kenya wana Victor Wanyama katika eneo la kiungo. Ndiye supastaa wa ukanda huu achilia mbali nchi yake. Wana Michael Olunga ambaye ni mshambualiji staa wa nchi hiyo lakini takwimu na rekodi hazionyeshi kama yeye ni bora kuliko. Kuanzia wakati wanacheza Afrika hadi walipokwenda Ulaya na kwingineko.

Tatizo kubwa kwa Samatta ni hili hapa. Kama angekuwa mshambuliaji halafu ukamchomeka katika vikosi vya Uganda na Kenya si ajabu angefunga zaidi na zaidi kuliko anavyofunga sasa hivi akiwa na kikosi cha Taifa Stars.

Nilikuwa nikimuona katika pambano dhidi ya Guinea ya Ikweta na kisha dhidi ya Libya juzi katika uwanja wa Taifa. Ile mechi ya Ikweta timu ilizidiwa. Hii mechi ya juzi Stars walicheza vyema lakini nilikuwa namuona Samatta kama kiungo mchezeshaji zaidi katika kikosi chake.

Badala ya kusimama pale mbele afunge, Samatta kama ilivyo kawaida yake katika kikosi hiki cha Stars alijikuta akihaha maeneo ya nje ya lango kupika mipango. Akiwa na TP Mazembe, Genk, Aston Villa na sasa Fenerbahce, Samatta huwa anasubiri pale mbele kufunga.

Hata hivyo mashabiki hawana haja sana ya kujadili hilo. wanachosema ni kwamba Samatta hajitumi. Hata wachambuzi wameanza kuingia katika mtego huu. Lakini tujiulize, Samatta anacheza na akina nani pale Taifa Stars? Ni wachezaji wanaomsaidia? Sidhani.

Nimemtazama Simon Msuva katika hizi mechi mbili. Kilichomuokoa ni kufunga kufunga bao letu la ushindi juzi. Kama Waydad Casablanca wangekuwa wanataka kumnunua Msuva kwa mechi hizi mbili za Stars sidhani kama wangeidhinisha hundi ya manunuzi.

Simon alionekana kuwa mchezaji wa kawaida kama wengine. Lakini unawezaje kumlaumu Simon? Yeye ni kama Samatta tu. Ni mhanga wa kucheza na wachezaji wa kawaida katika kikosi cha Taifa Stars. Huu ni ukweli ambao lazima tuumeze.

Nilitazama jinsi ambavyo Wakenya walikuwa wamewabana Mafarao. Ukweli ni kwamba kama Samatta na Msuva wangekuwa wanacheza katika kikosi cha Kenya si ajabu wangeweza kuwa bora zaidi kuliko wanapocheza katika kikosi cha Stars.

Wakati mwingine Samatta huwa anapitia kipindi kibovu cha soka. Ni kama ilivyo sasa. Sio tu kwamba hafanyi vema Stars lakini pia hata Fenerbahce. Alikuwa katika majeraha ya muda mrefu na sasa amerudi uwanjani. Bado hajafanya vema tangu arudi.

Hata hivyo anapochezea Stars mashabiki huwa wanaweka matarajio makubwa kwake bila ya kujali chochote kinachomzunguka. Hili ndilo tatizo la kuwa mchezaji mkubwa zaidi kikosini kuliko wenzako. Samatta ni zaidi ya Didier Drogba alipokuwa nahodha wa Ivory Coast.

Wakati mwingine ungeweza kuhamisha lawama kutoka kwa Drogba na kuzipeleka kwa akina Yaya Toure, Kolo Toure, Didier Zokora, Wilfried Bony na wengineo. Nao walikuwa mastaa wakubwa. Lakini kwa Stars Samatta tu ndiye mkubwa zaidi. Hakuna mchezaji mwingine wa kariba yake. Hata Msuva kumbuka kwamba bado anacheza Afrika hata kama anacheza katika klabu kubwa.

Anapofanya vema Ulaya, kama vile kuwa mfungaji bora Ubelgiji, taifa zima linasimama nyuma yake na kumfanya malaika. Alipokuwa anahamia England, taifa zima lilimfanya kuwa malaika. Anapocheza vibaya mechi moja tu taifa zima linamgeuza kuwa shetani.

Hakuna anayeangalia kiwango cha timu yetu ambayo katika pambano dhidi ya Guinea ya Ikweta ilishindwa walau kupiga pasi saba mfululizo. Hawaangalii aina ya wachezaji anaocheza nao. Tunachotaka sisi Samatta apige chenga mabeki wote na kufunga au kutoa pasi za mwisho.

Wakati tukiendelea kumgeuza kuwa shetani Samatta ndiye mchezaji ambaye anakaribia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha Stars. Yuko nyuma kwa mabao machache kwa mchezaji anayeongoza katika nafasi hiyo, Mrisho Ngassa.

Tatizo hili lilikuwa linamkabili Lionel Messi na Argentina yake. Alionekana kuwa mkubwa sana na ilikuwa rahisi kwake kubebeshwa lawama pindi timu inapofanya vibaya. Baadaye Waargentina wakagutuka kwamba Messi ndiye mfungaji bora wa muda wote katika kikosi chao ambacho hata akina Diego Maradona na Gabriel Batistusta walicheza. Wakaanza kumuheshimu kimya kimya.

Ukiitazama Taifa Stars ni wazi kwamba ina matatizo makubwa ya kiuchezaji kuliko Samatta.

Tunapotoa maneno ya kejeli na kashfa kwake huwa inaumiza. Kitu cha msingi na kushukuru ni ukweli kwamba huwa anakuja nyumbani na kucheza hizi mechi za Stars.

Kama angekuwa anajali kinachosemwa dhidi yake nadhani angejisingizia kuumwa na kubakia uzunguni mwa Istanbul akifuatilia mechi hizi za kufuzu kupitia king’amuzi chake nyumbani. Suala la yeye kucheza mechi zote ni kujali.

Mara kibao makocha wa kizungu huwa wanawazuia kijanja mastaa wa Afrika kurudi katika mataifa yao. Jose Mourinho wakati ule alikuwa akiwazuia kijanja akina Obi Mikel, Didier Drogba, Solomon Kalou na Michael Essien wasirudi nyumbani kucheza mataifa yao.

Walau Samatta anarudi, anacheza, na anageuka tena Ulaya licha ya kashfa mbalimbali ambazo tunaendelea kumpa. Tusimpe ushetani mtu ambaye anajitoa kwa ajili ya taifa lake. Tuliangalie vyema taifa, lakini pia tujiambie ukweli kuhusu kiwango cha soka letu kwa ujumla. Bila ya yeye tulifanya nini katika michuano ya Chan pale Cameroon?

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz