Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Tunaweza kuwa wengine lakini hatuwezi kuwa Morocco

Landscape Desktop Morocco Tunaweza kuwa wengine lakini hatuwezi kuwa Morocco

Wed, 14 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wanachokifanya Morocco pale Qatar ni kitu ambacho hakipaswi kukitamani sana. Hakituhusu sana sisi Watanzania. Kwamba kama tunaota tunaweza kuwa Morocco basi inabidi tusahau. Kuna maeneo mengine ambayo tunaweza kuanza kuiga siyo Morocco.

Tuanzie wapi? Katika kitu kinachoitwa jiografia. Huku sisi tupo chini, chini ya Bara la Afrika. Tupo katika uso mwingine wa dunia ambao umetufanya tuwe mbali na Ulaya. Morocco wapo karibu na Ulaya. Sisi tupo mbali na Ulaya.

Kwa vizazi na vizazi Wamorocco kama ilivyo kwa watu wengine wa Afrika Kaskazini kama vile Algeria na Tunisia wamejikuta wakizamia na kuzaliana Ulaya kwa miaka mingi tangu mwanzoni mwa miaka ya 1900. Haishangazi kuona vitukuu na vitukuu wa watu hawa wamezaliana Ulaya.

Matokeo yake ndio haya. Hakim Ziyech amezaliwa eneo la Dronten, Uholanzi. Sofiane Boufal anasumbua kweli kweli lakini amezaliwa Paris, Ufaransa. Romain Saiss amezaliwa Ufaransa. Achraf Hakimi amezaliwa Madrid. Sofyan Amrabat ambaye anakitibua kweli kweli pale katikati amezaliwa Uholanzi. Kipa wao Bono amezaliwa Canada.

Orodha ni ndefu, lakini kwa kifupi ni kwamba Wamorocco 16 katika kikosi hiki wamezaliwa nchi za Wazungu. Wamekulia katika mifumo ya wazungu. Na wengi zaidi wataibuka. Wengine watachezea katika timu za wazungu wengine watachezea za kwao. Walioamua kuchezea timu za wazungu ndio hawa kina Zidane. Walioamua kuchezea timu za Afrika ndio hawa kina Riyad Mahrez na Ziyech.

Nimewahi kutembelea nchi za Hispania, Ubelgiji, Ufaransa na Uholanzi. Kuna jamii kubwa za watu hawa. Katika Wamorocco elfu moja utawakuta Watanzania wawili tu. Haishangazi kuona hizi jamii zimetawala Ulaya katika maeneo mbalimbali na sio soka au michezo peke yake.

Katika hali hii sisi hatuwezi kuwa wao. Sisi tumeanza kuzamia Ulaya majuzi tu. Waliozamia zamani walikuwa mabaharia na wasomi wachache katika zama za Mwalimu Nyerere. Wenzetu walizamia bila ya kuwa na ubaharia wala usomi. Jamii zilihamia kwa wingi. Leo wanavuna walichopanda.

Kinachonichekesha ni kwamba hata tukitoa uraia wa nchi mbili kama ilivyo kwa Wamorocco ukweli ni kwamba sijaona Watanzania wengi walio nje wenye uwezo wa kutusaidia. Huwa tunadanganya tu kuwa uraia wa nchi mbili unaweza kutusaidia lakini ukweli haupo hivyo. Ni Wachezaji wangapi wenye asili ya Tanzania wanaotamba Ulaya? Nadhani ni mmoja tu, Yusuf Poulsen. Wengine wanacheza daraja la tatu au la nne.

Watanzania wengi waliozaliwa au kukulia Ulaya hawajafikia kiwango au mafanikio ya Mbwana Samatta. Ni Poulsen tu ndiye ambaye amefikia na kupita kiwango hicho. Ukweli ni kwamba wapo Watanzania wachache wanaoishi nje na hauwezi kupata wachezaji wengi katika jamii zetu kulinganisha na wenzetu.

Katika hili nadhani siwalaumu Watanzania peke yao. Kuna Wazambia wangapi waliozaliwa nje katika idadi kubwa kama Wamorocco? Wamalawi wangapi? Wakenya wangapi? Idadi yao ni chache kwa mujibu wa jiografia.

Kitu cha msingi kwetu ni kuanza kushindana na hawa hawa wenzetu na kuhakikisha tunakwenda Afcon mara nyingi. Lakini kitu cha msingi ni kupeleka watoto wengi nje kwa wingi. Ni kama inavyotokea kwa vijana wa Afrika Magharibi. Wapo wanaozaliwa kule, lakini hawawezi kushindana na mataifa kama Morocco, Algeria au Tunisia.

Kina Sadio Mane, Didier Drogba, Samuel Etoo na wengineo walikwenda kule wakiwa wadogo. Hawa ndio ambao inabidi tuangalie namna ya kujifunza kutoka kwao kabla ya kuwafikiria Morocco. Historia ukiitazama haishangazi sana kuona Morocco inakuwa nchi ya kwanza kutoka Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia.

Ni kweli kina Senegal, Cameroon na Ghana waliwahi kutangulia kuwa wa kwanza kufika robo fainali lakini unapoitazama historia ya Morocco na kikosi walichokwenda nacho haishangazi sana kuona wakiwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufika nusu fainali Kombe la Dunia.

Ni hapa hapa unapowaza kwamba pamoja na kuwa na timu ngumu katika Ligi yao kama Wydad Casablanca, Raja Casabalanca, FAR Rabat, Berkane na wengineo lakini wachezaji wao hawachezi katika timu ya taifa (ukiacha wawili-watatu) na sio tegemeo. Sisi tunaamini kwamba wachezaji wa Simba na Yanga watatuvusha. Haiwezekani. Ni kichekesho.

Katika pambano moja la soka tunaweza kuwafunga lakini katika ujumla wake hatuwezi kufanya vizuri zaidi yao. Fikiria mabingwa wa Afrika pamoja na mabingwa wa Shirikisho hawatoi wachezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha timu ya taifa.

Lakini kuna kitu kingine cha kuchekesha kidogo. Mwaka jana nilisafiri na timu ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20 katika michuano ya mataifa ya Afrika iliyofanyika nchini Mauritania. Pambano la mwisho la kundi la Ngorongoro Heroes dhidi ya Morocco lilipaswa kufanyika katika mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott.

Timu zote mbili zilisafiri pamoja kutoka katika mji wa Nouadhibou ambako kulichezwa mechi za mwanzo za makundi. Kichekesho kilitokea katika Uwanja wa Ndege wa Nouakchott. Wenzetu walisubiri gari kubwa kubeba vifaa vyao wakati sisi tulikuwa na mabegi makubwa matatu tu.

Wenzetu walionyesha namna gani walivyokuwa ‘serious’ na soka katika ngazi zote sisi tulionekana kama vile tunafanya masikhara. Kabla haujafikiria kufikia mafanikio yao nadhani inabidi tuanze kujadili mambo ya msingi.

Kuna mambo ya msingi ambayo bado hatujafanya achilia mbali suala la wenzetu kuzaliwa nje. Mpaka tutakapoanza kufanya mambo ya msingi ndipo tutakapoanza walau kufikiria namna ya kuwafikia wenzetu wa kawaida achilia mbali Morocco ambao wako mbali zaidi.

Columnist: Mwanaspoti