Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Tofauti ya kuwa Mayele na tofauti ya kuwa Lusajo

Mayele Pic Tofauti ya kuwa Mayele na tofauti ya kuwa Lusajo

Wed, 9 Mar 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Reliant Lusajo alitangulia kufunga mabao kumi wiki mbili zilizopita. Fiston Mayele ametimiza mabao kumi juzi jioni katika pambano dhidi ya Geita Gold. Ilikuwa safari ndefu kwa Mayele kumfikia Lusajo, lakini ilifikirika.

Kuna tofauti kati ya kuwa Mayele na kuwa Lusajo. Sitaki kuzungumzia tofauti zao za ndani ya uwanja. Kwa kiasi kikubwa wamefanana. Wote wanafunga na kutengeneza mashambulizi. Wanasaidia wenzao kufunga.

Lakini nje ya uwanja wanaweza kuwa na tofauti kidogo. Kwa mfano, namna ambavyo kwa muda mrefu Mayele ameimbwa nchini ungeweza kudhani kwamba alikuwa ndiye mfungaji bora mbele ya Lusajo na George Mpole. Kuna sababu mbili za kwanini ameimbwa sana.

Kwanza ni kwamba Mayele anachezea timu kubwa - Yanga. Ina mashabiki wengi. Hata Lusajo anajua kwamba mabao haya angefunga akiwa na Simba au Yanga angeimbwa zaidi. Maskini, amefunga akiwa na timu inayotoka Wilaya ya Ruangwa.

Sitashangaa kuona mwisho wa msimu Lusajo akitamani kwenda Yanga au Simba. Ni jambo la kawaida kwa washambuliaji hatari wanaocheza timu ya aina yake. Nafahamu kwamba hata Harry Kane anatamani kuhama Tottenham Hotspurs na kwenda kwa wakubwa zaidi.

Lakini kuna kitu kina Lusajo labda wanakosea. Unaposikia majina ya kina Mayele, Stephen Sey, Herieter Makambo na Meddie Kagere kuna vitu viwili vinakuingia akilini. Kwanza kabisa ni wageni. Pili ni wafungaji hodari. Lakini tatu wametuachia staili za ushangiliaji pindi wanapofunga.

Waingereza wanaziita staili hizi kama trademark. Kagere anaziba jicho moja kwa kiganja cha mkono wake, Makambo anawajaza, Sey anawaaga. Mayele ndio kama tunavyojua. Staili yake imekuwa staili ya taifa ingawa kwa kiasi kikubwa inachangiwa na aina ya timu ambayo anaifungia mabao. Inavyoonekana wageni wana mbwembwe zaidi yetu. Inaonekana labda wageni wanathamini zaidi mabao wanayoyafunga kuliko sisi tunavyoyathamini. Labda wachezaji wetu wazawa wanachukulia kuwa ufungaji wa mabao ni kitu cha kawaida. Kina Lusajo hatujui wana staili ipi. Sio yeye tu, kaka zake Mbwana Samatta, John Bocco na Thomas Ulimwengu pia hawajawahi kutuachia staili za kushangilia. Walau Simon Msuva huwa anakwenda kupiga sarakasi kando ya uwanja.

Nini maana yake? Staili ya Mayele inamuongezea umaarufu kama ilivyo kwa Sey. Ni rahisi kwa watu wasiohusika na mchezo wa soka kumtambua kwa urahisi Mayele kuliko Lusajo hata kama Lusajo ataibuka kuwa mfungaji bora mwishoni mwa msimu. Kufikia hapo jina la Mayele litakuwa kubwa katika idadi ya mashabiki wa soka na wale wasio wa soka kwa sababu kuna kitu kitakuwa kinamtambulisha zaidi. katika dunia ya kibepari tayari Mayele atakuwa na faida nyingine mkononi nje ya kucheza mchezo wa soka.

Kwa wenzetu pia inakuwa na faida kibiashara. Kwa mfano, Mayele anaweza kutoa fulana akauza huku staili yake ikitokea mbele ya kifua chake. Zinaweza kutoka fulana nzuri tu ambazo zinaonyesha mkono mmoja wa Mayele ukichapa mkono mwingine. Atauza.

Lakini kwa sababu mbalimbali kampuni zinaweza kuvutika na Mayele na akafanya matangazo nao kuliko ilivyo kwa Lusajo au wachezaji ambao hawana staili za ushangiliaji. Ndivyo inavyokuwa. Huu mchezo nao unahitaji mbwembwe kidogo.

Ni rahisi kwa meneja wa Mayele kumnadi kibiashara katika kampuni za simu, benki, viwanyaji vikali na laini kwa sababu anaweza kutumia staili yake kufanya matangazo. Rafiki yangu Lusajo hata akiwa mfungaji bora umaarufu wake unajikuta upo chini kwa Mayele.

Zamani mchezo wa soka ulikuwa mkavu, lakini siku hizi una vionjo vya Hollywood. Haishangazi kuona watu wengi tunaamini kwamba Lionel Messi ni bora kuliko Cristiano Ronaldo ndani ya uwanja, lakini nje ya uwanja Ronaldo amekuwa bora kuliko Messi.

Sababu ni rahisi tu. Kuanzia ndani ya uwanja Ronaldo ana staili yake ya ushangiliaji ambayo dunia nzima inaielewa. Lakini nje ya uwanja Ronaldo amekuwa mtanashati na ambaye staili zake za nywele na mengineyo vinamfanya afuatiliwe zaidi. Haishangazi kuona Ronaldo ndiye mwanadamu mwenye wafuasi wengi katika mtandao wa Instagram. Sio kwa sababu ya mabao yake tu bali wapo watu wengi, hasa mabinti ambao wamekuwa wafuasi wake kwa sababu ya mtazamiko wake na namna alivyochagua kuishi. Wayne Rooney inawezekana alikuwa mchezaji bora kuliko David Beckham wote wakiwa katika ubora wao, lakini Beckham alitengeneza kiasi kikubwa cha pesa kuliko Rooney kutokana na aina ya maisha ambayo aliamua kuchagua.

Wakati mwingine wachezaji wetu lazima watafute staili zao ndani na nje ya uwanja. Inashangaza kidogo wakati wasemaji na waandishi wanapokuwa na wafuasi wengi mitandaoni kuliko mastaa wetu wa klabu kubwa na ndogo nchini. Mohamed Hussein Tshabalala ndiye mchezaji mwenye wafuasi wengi kwa wachezaji wanaocheza ndani. Ametimiza wafuasi milioni moja mwezi uliopita na haishangazi kuona anapata mikataba ya biashara nje ya uwanja wa soka. Tshabalala anajinadi zaidi mitandaoni kuliko wenzake. Aliyepaswa kuwa staa zaidi nadhani ni John Bocco. Washambuliaji hutazamwa zaidi. Hata nje ya nchi mastaa wengi zaidi wanakuwa washambuliaji. Lakini mitandaoni Tshabalala ni zaidi ya Bocco. Hii ndio dunia ya kisasa ambayo wenzetu wanaishi kwa sasa. Wanasoka wetu wamegoma kabisa kuishi katika dunia hii. Wanataka kuwa mastaa uwanjani halafu basi. Kuna dunia ya mbwembwe ambayo pia huwa inampatia Diamond Platinumz pesa nyingi. Hawataki kuishi. Dunia ya kutazamika kama staa. Mchezaji kama Lusajo anapaswa kutupa sababu nyingine zaidi za kumjua ndani na nje ya uwanja kuliko mabao yake pekee.

Columnist: Mwanaspoti