Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Tajiri Yusuph Manji atarudi Yanga kama nani?

10799 Manji+pic HISIA ZANGU: Tajiri Yusuph Manji atarudi Yanga kama nani?

Wed, 14 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MINONG’ONO kwamba baadhi ya watu wa Yanga wanamtaka Yusuph Manji arejee klabuni imeanza. Kuna sababu mbili. Kwanza labda kwa sababu nchi ilimpoteza Rais John Magufuli ambaye inaaminika serikali yake haikuwa na mahusiano mazuri na Manji. Ikamlazimu Manji kuondoka zake nchini.

Taarifa zisizo za uhakika zinadai kwamba amereja nchini kimyakimya. Vyovyote ilivyo, kuondoka kwake kulikuwa mwanzo wa Yanga kuyumba kiuchumi. Timu yao nzuri ikaanguka chali. Simba wakachukua nafasi.

Lakini pia inawezekana watu wa Yanga wanataka Manji arudi labda kwa sababu wanaona timu yao haifanyi vizuri kama ilivyokuwa katika utawala wake. Siku hizi lile soka la ‘kampa kampa tena’ limeondoka na kuhamia Msimbazi.

Na sasa swali linakuja. Wanaotaka Manji arudi Yanga wanataka arudi kama nani? Mwenyekiti? Mfadhili? Au mdhamini? Jibu lolote ambalo utapata hapo utaongezea na swali kama Yanga wanataka arudi halafu GSM waondoke au?

Hapa kuna mambo mawili. Kwanza kabisa Yanga lazima waheshimu juhudi zote ambazo zimefanywa na kampuni ya GSM. Bila ya GSM kuingilia kati Yanga ingekuwa hoi kwa kila kitu. Ndani na nje ya uwanja ingekuwa hoi zaidi.

Kama GSM wangeamua kuendelea kuishi klabuni hapo kwa mkataba wa mauzo ya jezi peke yake nadhani sasa hivi Yanga wangekuwa hoi zaidi. Wakati wakiutumikia mkataba kwa njia hiyo tuliona jinsi ambavyo Yanga ilitawaliwa na michango.

Inahitajika heshima kubwa kwa GSM wakati unazungumzia ujio wa Manji ndani ya Yanga. Wamefanya mambo mengi katika kipindi kifupi. Tatizo kubwa la watu wa Yanga ni kujaribu kuifananisha Yanga na Simba. Hapa ndipo wanapohisi Yanga haijafanya kitu.

Ambacho Wanayanga wanasahau ni ukweli kwamba timu yao ilibomoka zaidi wakati Manji alipopata matatizo na hapohapo Simba ikaanza uwekezaji mzuri wa kikosi. Usitegemee kwamba Yanga wanaweza kurudi tena juu kwa usiku mmoja. Wanahitaji kupitia mchakato mwingine wa kuwa na timu imara uwanjani. Hauwezi kuwa mchakato wa siku moja au msimu mmoja.

Wanachokifanya Yanga kwa sasa katika kikosi chao ni panga pangua ambayo baadaye itawarudishia timu imara. Hata Yanga ile ya Manji haikujengwa usiku mmoja. Mpaka walipofika kwa Donald Ngoma kumbuka walishapita kwa Jama Mbah.

Kitu kingine ambacho mashabiki hapaswi kusahau ni kwamba Yanga ile ilikutana na Simba ambayo ilikuwa hoi kipesa. Wakati Yanga wakijenga timu ya ushindani Simba walikuwa na ukata kiasi cha kufikiria kutumia wachezaji vijana tu katika kikosi cha kwanza.

Wakati ule wa ukata Simba ndio wakajidanganya kwamba wangeweza kuunda timu yao kupitia kwa vijana kina Jonas Mkude, Abdallah Seseme, William Luician ‘Gallas’, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla na wengineo. Walikuwa wanafungwa kila kukicha.

Yanga ilikuwa na watu wa maana kwelikweli. Kina Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Thaban Scara Kamusoko, Amissi Tambwe, Saimon Msuva, Juma Abdul, Haruna Niyonzima na wengineo. Hawa walikuwa na

mishahara mikubwa na wengine waliletwa klabuni kwa madau makubwa.

Leo hata kama Manji angekuwepo Yanga ni wazi kwamba asingeweza kuzuia ubora wa Simba hii kwa sababu sasa Simba wameamua na tajiri Mohamed Dewji naye

ameamua kuwekeza nguvu zake katika kuijenga Simba yake. Mambo yasingekuwa rahisi.

Tukirudi katika swali la msingi la Manji arudi Yanga kama nani? Nadhani kuna mambo ya kuangalia. Wote tunapenda matajiri warudi katika mpira. Tunapenda kina Manji warudi katika soka na kuonyeshana ubabe kwa sababu ndio afya ya soka.

Kitu cha kuangalia ni kwamba wasirudi kama wafadhili. Warudi kama wawekezaji halali wanaotambulika na mifumo rasmi. Hii itawafanya wafanye mambo makubwa kuliko awali. Wanunue hisa na kuwekeza zaidi.

Hii pia itazifanya timu zisiwe maskini pindi wakiondoka. Kumbuka namna Yanga walivyoanza kuteseka dakika chache tu baada ya Manji kutupwa Gereza la Keko. Maisha yalianza kuwa magumu na kina Donald Ngoma wakaanza migomo.

Katika dunia nyingine ambayo wenzetu wanaishi watu kama GSM, Manji na Rostam Aziz wanaweza kuwa na hisa zao ndani ya Yanga kwa wakati mmoja. Kama kuna kiongozi atatoa ndani yao basi ni kwa mfumo wa uwekezaji.

Wanaotaka Manji arudi kama mwenyekiti inawezekana wanataka arudi katika mfumo ule ule wa

zamani ambao Mwenyekiti Manji alijikuta anatoa pesa zake za mfukoni kwa ajili ya kuisaidia timu.

Wakati mwingine alikuwa anaikopesha kiasi kwamba Yanga walijikuta na deni la Sh11 bilioni kwake, kwa mujibu wa Manji mwenyewe. Watu ambao wanamtamani Manji wafanye mambo mawili. Kwanza waendelee kuiheshimu GSM ambayo imewatoa katika michango ya mchele na maharage kupitia kwa nahodha wao wa zamani, Ibrahim Ajibu.

Lakini pia watuambie tu Manji arudi klabuni kama nani. Binafsi namkubali Yusuph Manji. Ukimchukia tajiri aliyetumbukiza pesa zake nyingi katika soka unaweza kuwa mchawi.

Yusuph anajua kutumia pesa katika soka. Pesa zake ndizo zilisababisha tuone soka maridadi la Yanga chini ya kina Kamusoko. Lakini ni muhimu kujua atarudi klabuni kama nani.

Katika soka la kisasa hakuna kitu kinachochukiza kama neno ufadhili. Hizo Manchester United, Arsenal, Liverpool na nyinginezo hazina wafadhili. Zina wadhamini au wawekezaji. Hii inazisaidia timu kuwa imara hata baadhi ya matajiri wanapokufa au kuondoka.

Pale Manchester United alipofariki dunia tajiri Malcom Glazer watoto wake wameichukua timu na mpaka sasa United imeendelea kuwa imara kipesa.

Hapa nchini kwa mfumo huu wa ufadhili tajiri akifa nadhani kila kitu kinakuwa kimekufa. Timu inarudi katika shida.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz