Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Sakho, bao bora sawa lakini bao ana madeni

Sakho Pic Pape Ousmane Sakho

Wed, 27 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Katika dakika za majeruhi za msimu ambao ulitajwa kuwa mbovu kwa klabu ya Simba, ghafla winga wao mfupi kutoka Senegal, Pape Sakho akawapa Simba kitu cha kutamba. Alibeba tuzo ya mfungaji wa bao bora la CAF kwa msimu uliopita. Sio kitu kidogo.

Ina maana kwamba kwa mabao yote yaliyofungwa katika michuano ya CAF msimu uliopita kuanzia mechi zote za Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho na mechi za kufuzu michuano mbalimbali ya Afrika kwa timu za Taifa, bao la Sakho lilikuwa bora zaidi. Ni kitu kikubwa. Baada ya hapo Sakho amejaribu kufunika kila kitu kilichomhusu yeye katika msimu uliopita. Baada ya kugusana bega na kina Sadio Mane kuna mambo yametafakarisha kuhusu Sakho. Ameibuka shujaa, lakini binafsi kuna mambo nimeyaweka akiba.

Ukweli ni kwamba bao la Sakho halikutosha kumpa ushujaa mkubwa staa huyu ndani ya Simba. Sakho bado hakuweza kuikamata Simba kama ilivyofikirika. Hata baada ya kutwaa tuzo hiyo tumesikia kwamba anatakiwa na klabu mbalimbali za Morocco. Sioni mashabiki wa Simba wakiwa na wasiwasi kama akiondoka klabuni. Ni wasiwasi ambao ulikuwa umetanda katika miaka ya karibuni pindi mchezaji kama Emmanuel Okwi alipokuwa akihusishwa kuondoka klabuni. Watu wa Simba walipata fadhaa katika mioyo yao. Huyu Mganda alikuwa ameikamata timu kupita kiasi.

Kuondoka kwake kulileta hofu. Mashabiki walikuwa hawaoni kama timu yao inaweza kwenda bila yeye. Hata alipoondoka viongozi na mashabiki walipambana arudi klabuni. Na kweli aliporudi alikidhi matazamio. Sakho bado hajafikia kiwango hiki cha kuwa roho. Halafu kuna huyu Clatous Chotta Chama. Naye aliwahi kufikia kiwango hiki cha Okwi. Kwamba timu haiwezi kwenda bila ya yeye. Alipohusishwa kuondoka Msimbazi mashabiki wa Simba roho zilikuwa juu. Na bahati mbaya alikuwa anahusishwa na kujiunga pia na watani wao Yanga.

Alipokwenda Morocco, Simba bado waliamini kwamba timu yao haiwezi kwenda bila ya yeye. Shinikizo lilikuwa juu kutaka arudi. Hatimaye sasa amerudi. Na mashabiki wanaamini kwamba watakuwa na msimu mzuri zaidi michuano mbalimbali ikianza kwa sababu Chama atakuwa fiti.

Sakho hajawahi kufikia kiwango hiki. Hata yeye ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wanatupiwa lawama kwa kushindwa kuziba pengo la Chama wakati hayupo. Ufundi katika kutengeneza nafasi ulipungua na hawezi kukwepa lawama hizi.

Vivyo hivyo kwa Luis Miquissone. Alifika mahala ambapo Sakho bado hajaweza kufika. Mpaka leo ukiwauliza Simba kwamba Sakho aondoke na Miquissone arudi, basi kura zitakuwa nyingi kwa Miquissone kurudi na Sakho kuondoka klabuni hapo.

Bao zuri la CAF nadhani lisimvimbishe kichwa Sakho. Ameshindwa kuishika timu kisawasawa kama ilivyopaswa kuwa. Mpira wake bora aliucheza katika michuano ya Kombe la Mapinduzi. Sijui ulitoka wapi mpira ule. Hatujawahi kuuona tena. Kama angekuwa akicheza vile kila wikiendi katika ligi na michuano ya Afrika, basi angeikamata timu. Baada ya pale tuliendelea kumtazama Sakho lakini leo angeweza kuwa hivi na kesho angekuwa vile. Hakuwahi kuwa na mwendelezo wa ubora (consistency). Leo angekuwa shujaa, kesho angekuwa mchezaji wa kawaida. Kikubwa zaidi ni katika mchezo wake mwenyewe. Sakho hana uamuzi mzuri uwanjani. Ana uwezo mkubwa wa kukaa na mpira. Kama angeweza

kuwatazama wenzake zaidi basi wangefunga zaidi. Ameondoka katika ligi akiwa amepiga pasi tano za mwisho. Angeweza kufanya zaidi. Chama aliondoka na pasi za mwisho 14.

Sakho alifunga mabao saba na mengi yalikuja mwishoni wakati ligi ikiwa imeanza kusinzia. Ina maana hakupitisha mabao kumi kwa msimu huku pia hakuwa amepitisha asisti kumi kwa msimu. Akivuka hizi namba nadhani ndio atakuwa ameingia katika umuhimu wa kina Okwi na Chama.

Ni kweli ulikuwa msimu wake wa kwanza tu klabuni tofauti na kina Okwi, lakini napata hofu zaidi kama ataendelea kuimarika siku za usoni kila ninapokumbuka aina yake ya mpira. Sakho ni mchoyo. Anacheza zaidi kwa ajili yake. Akiuelekeza mchezo wake katika timu zaidi nadhani ndipo ataishika timu vyema.

Wakati huu ambapo anahusishwa kuondoka naona watu wa Simba hawashtuki. Ina maana hajaikamata vizuri timu. Kama akiendelea kuwepo msimu ujao inabidi aurekebishe mchezo wake.

Bao bora la CAF halimaanishi kwamba amekuwa mfungaji bora wa CAF. Ni vitu viwili tofauti.

Bahati nzuri kwake ni kwamba atakosa visingizio. Msimu uliopita angeweza kudai kwamba hakuwa na wachezaji wazuri kando yake. Msimu huu Simba imesajili wachezaji wazuri kando yake. Wanaweza kumng’arisha zaidi au akawang’arisha zaidi na hivyo kusimika umuhimu wake klabuni tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Hata hivyo ujio wa mastaa wapya nao ni changamoto kwake. Ushindani utakuwa mkubwa zaidi. Hatuwezi kujua kama anaweza kujikuta akiishia katika benchi kama mastaa wapya watakuwa wakali zaidi yake na wanaweza kucheza nafasi mbalimbali pale mbele. Ni kama ambavyo tunaweza kujiuliza kama angekuwa na nafasi ya kudumu kama angewakuta kina Miquissone na Hassan Dilunga wakiwa fiti.

Kama akibaki msimu ujao utaamua hatima yake Msimbazi. Kuna mastaa ambao hatima zao ziliamuliwa katika msimu wa kwanza tu. Ni kama vile Enock Inonga. Lakini yeye na baadhi ya wenzake tunategemea kuamua hatima yao kwa umakini zaidi katika msimu ujao. Ni kama kule kwa watani zao namna ambavyo Fiston Mayele aliamua hatima yake katika msimu wa kwanza tu.

Columnist: Mwanaspoti