Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Saido mtoto wa mjini aliyerudi tena mjini

Saido Training Saido Ntibazonkiza

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Saido Ntibazonkiza amerudi tena mjini. Amesaini mkataba wa miaka miwili Simba. Hivi ndivyo namna ambavyo maisha yanakwenda kasi katika soka letu. Wakati ule akisajiliwa na Yanga kuna watu wa Simba walikuwa wanadai kwamba Yanga wanamsajili mchezaji mzee.

Leo Saido amesajiliwa na Simba. Miezi sita tu ya kucheza Geita imewatosha Simba kukiona kitu ambacho Yanga walikiona zamani katika miguu ya Saido. Kwa kadri ninavyosoma mitandaoni naona mashabiki wa Simba wamegawanyika kuhusu usajili wake.

Kuna wanaoamini kwamba hii ni hatua moja nyuma kwa Simba. Kwamba wanamsajili vipi mchezaji ambaye Yanga waliachana naye. Na kwamba licha ya kuachana naye Yanga wameendelea kusonga mbele na kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ambayo inawakabili.

Ni kama vile kuna aibu fulani kwa Simba kumsajili mchezaji ambaye Yanga waliamua kuachana naye. Ni kama vile Yanga wakimsajili Meddie Kagere itaonekana ni aibu fulani hivi kumsajili mchezaji ambaye aliachwa na watani kwa kuonekana kwamba wanahitaji mchezaji mwenye kiwango kikubwa zaidi yake.

Halafu kuna hawa wanaoungana na mimi katika kuunga mkono viongozi waliomsajili Saido. Msimu uliopita akiwa na Yanga namba zake hazikudanganya. Msimu huu ndani ya miezi sita tu namba za Saido ni nzuri kuliko za wachezaji wengi wa eneo la mbele la Simba. Amefunga mabao ya kutosha na amepiga pasi za mwisho za kutosha.

Kifupi ni bora uwe na Saido katika eneo la mbele kuliko kuwa na Kibu Dennis au Ousmane Sakho. Wanaweza kuwa ni wadogo kwa umri lakini imethibitika kwamba Saido ana madhara zaidi kuliko hao. Wakati mwingine soka ni mchezo wa namba. Saido amezipata namba zake akiwa anacheza Geita. Vipi akiwa na Simba?

Na linapokuja suala la umri imethibitika kwamba umri sio kitu katika soka la Kitanzania. Inabidi umri uwe umesogea zaidi ili ushindwe kucheza soka letu. Kuna vijana wengi wameshindwa kutuonyesha kile ambacho Saido, Clatous Chama, Josh Onyango na wengineo wamekuwa wakituonyesha kila siku.

Sifahamu dhamira ya Saido ilikuwa nini baada ya kuamua kucheza Geita Gold pale alipoachwa na Yanga. Kuna wachezaji ambao ni watoto wa mjini. Wanajua namna ya kuziwinda klabu kubwa. Kuna uwezekano mkubwa Saido aliamini katika uwezo wake akaamua kujiegesha mahali kwa ajili ya kuziwinda klabu kubwa kama Simba na Azam.

Nahisi Saido alikuwa anajua anachokifanya. Kuachana kwake na Yanga hakukuwa kuzuri. Sawa mkataba wake ulikuwa umemalizika lakini namba zake zilikuwa nzuri tu. Watu wa Yanga walikuwa wanadai kwamba Saido alikuwa jeuri na anawasumbua na ndio maana waliamua kutomuongeza mkataba.

Nadhani Saido aliitazama ligi yetu na kuona uwezekano wa kurudi katika timu kubwa. Si ajabu ndio maana akaamua kujiegesha Geita Gold ingawa angeweza kwenda nje ya Tanzania au kurudi zake Bujumbura kumalizia maisha yake ya soka. Lakini sasa dhamira yake imetimia na amepata kitita chake cha mwisho kutoka Simba huku akirudi tena Kariakoo.

Ni ngumu kuwalaumu viongozi wa Simba kushawishika kumchukua Saido. Ingekuwa ile Simba ya Luis Miquissone, Hassan Dilunga, Chama, Meddie Kagere nadhani wasingeshawishika sana kumchukua Saido lakini kwa Simba hii Saido atawasaidia. Kwa jicho la ndani ya nchi wachezaji wenyewe wenye madhara ni hawa kina Saido. Labda tuwalaumu kwa kushindwa kutupa jicho nje ya nchi.

Sitashangaa hata kama Simba wataamua kumrudisha Meddie Kagere. Angalia umri wake lakini katika ligi yetu bado anafunga. Nadhani hata watu wa Simba sasa hivi wanajua katika mioyo yao kwamba ni bora uwe na Kagere kuliko Kibu. Labda kama unampata mshambuliaji mwingine nje ya nchi ambaye atakuwa bora kama Moses Phiri.

Kwa soko la ndani bado wachezaji wenye umri mkubwa wataendelea kutamba zaidi na zaidi. Saido amethibitisha hilo. Lakini hata kama kuna mtu anahitaji beki mzuri wa kushoto anaweza kwenda zake Kagera Sugar kumchukua David Luhende ambaye aliichezea Yanga zaidi ya miaka minane iliyopita.

Leo ni mabeki wachache wa pembeni wanaofikia uwezo wake. Kuna vijana wengi wa pembeni hawafikii walau nusu ya uwezo wake. Huu ndio ukweli mchungu unaolizunguka soka letu na wakati mwingine ni vigumu kuilaumu Simba kwa kumsajili Saido.

Namna gani Saido atacheza Simba ni jambo la kusubiri na kuona. Ni wazi kwamba atacheza kwa kutokea pembeni. Chama ataendelea kucheza katikati. Saido ni mzuri akitokea upande wa kushoto. Anaweza kufunga na pia kutengeneza nafasi.

Lakini huenda Simba wakawa wametibu lile tatizo lao la muda mrefu. Kwamba bila ya Chama timu yao inapata wakati mgumu kutengeneza nafasi. Huenda sasa Chama akakosekana lakini Saido akasaidia kutengeneza mashambulizi. Ni kitu ambacho katika siku za karibuni wamekuwa wakichekwa na wapinzani wao Yanga.

Columnist: Mwanaspoti