Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Rally Bwalya anaondoka, lakini hatuna machozi mengi

Matolya Bwalya Kiungo wa Simba SC, Rally Bwalya na Seleman Matola

Wed, 22 Jun 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Swali kubwa ambalo viongozi wa Simba wangekabiliana nalo nyakati hizi lingekuwa hili. “Kwanini mnamuuza Rally Bwalya wakati ilibidi tujiimarishe kwa ajili ya msimu ujao? Wenzetu wanazidi kujiimarisha sisi tunabomoa kikosi.”

Lingekuwa swali kubwa zaidi nyakati hizi watani wao Yanga wakiwa wametoka kutawazwa ubingwa. Lingekuwa swali kubwa zaidi nyakati hizi ambazo mashabiki wa Simba wameanza kuamini kwamba kweli watani wao wamemnasa kiungo mahiri mchezeshaji wa Asec Mimosas, Stephane Aziz Ki.

Lingekuwa swali kubwa zaidi kwa sababu tayari mashabiki wa Simba wanaamini miongoni mwa sababu za timu yao kutofanya vyema msimu huu ni pamoja na mauzo ya mastaa wao wawili wakubwa wa misimu iliyopita, Clatous Chama na Louis Miquissone.

Lakini hapohapo bado mashabiki na wanachama hawajahoji kuhusu kiasi cha pesa ambazo Bwalya ameuzwa. Mara nyingi mashabiki walau huwa wanaunga mkono uamuzi wa viongozi kumuuza mchezaji pale wanapoambiwa kuhusu kiasi kikubwa cha pesa ambacho klabu itapata.

Hata hivyo, safari hii mashabiki wamepitisha uamuzi wa viongozi kumuuza Bwalya bila ya kuhoji kiasi ambacho wameingiza katika mauzo ya mchezaji huyo. Wakati ule walipowauza Chama na Miquissone walilainishwa na kiasi kikubwa cha pesa kilichotajwa kama mauzo yao.

Safari hii, licha ya matokeo yasiyoridhisha kwa Simba, lakini wamekubali tu Bwalya aondoke zake. Na juzi mashabiki walijitokeza katika Uwanja wa Mkapa kumuaga Bwalya ambaye aliichezea timu hiyo pambano la mwisho kabla ya kuondoka nchini.

Mara nyingi huwa inatokea kwa mchezaji kuagwa vile kama alikuwa mtumishi wa muda mrefu klabuni. Ni kama ambavyo itatarajiwa Simba kumuaga Jonas Mkude kwa mbwembwe zaidi baada ya kuitumikia klabu kwa zaidi ya miaka kumi. Lakini, hauwezi kufanya vile kwa mchezaji aliyeitumikia timu kwa miezi 24 tu.

Kifupi ilikuwa ni kama wanamng’ong’a Bwalya kwamba “huyu naye aende zake tu”. Huu ndio ukweli ambao sio watu wote wa Simba watakuambia, lakini wakiwa wenyewe huwa wanazungumza. Bwalya hakuwa na maajabu makubwa kama ilivyodhaniwa.

Aliwasili nchini miezi 24 iliyopita huku mabosi wa Simba wakiweka wazi kwamba walikuwa wamempora mchezaji huyo katika mikono ya watani zao, Yanga, ambao inadaiwa kwamba walimhitaji kabla yao kwa ajili ya kukifanyia mabadiliko kikosi chao ambacho kilikuwa kinasuasua.

Bosi mmoja wa Simba aliwahi kudiriki kuniambia kwamba Simba walikuwa wamempata kiungo hodari kuliko Chama. Aliniambia kwamba hata Zambia mashabiki wanaamini kwamba Bwalya alikuwa na uwezo mkubwa kuliko Chama.

Kitu hiki hatukukiona kwa macho yetu. Hatukukiona wakati Bwalya akicheza na Chama, lakini pia hatukukiona wakati Chama alipoondoka kwenda Morocco. Bwalya ni kiungo maridadi mwenye mguu wa kushoto kama sumaku. Lakini mguu wake hauna matokeo chanya sana.

Bwalya alikuwa mchezaji mzuri pindi Simba walipotawala mechi katika nyakati za Chama na Miquissone.

Hata hivyo, katika mechi ambazo Simba ilibanwa nadhani alishindwa kuamua mechi. Baadaye alipoondoka Chama tuliamini Bwalya angekuwa mchezaji imara zaidi ndani ya kikosi cha Simba.

Tuliamini Chama alikuwa anamzuia Bwalya kujitawala katika kikosi na kwamba labda sasa ungekuwa wakati wa Bwalya kuwa mchezaji muhimu zaidi ndani ya Simba. Hata hivyo, hatukuweza kukiona kitu hicho.

Kilichotokea ni kwamba kuna wakati ilishikiliwa na Benard Morrison. Na wakati huu tunamaliza msimu timu imeshikiliwa na Kibu Dennis. Hatuwezi kubishana kuhusu hili.

Hakuna nyakati ambazo Bwalya anakosekana halafu tukaulizana kwanini amekosekana. Hajawahi kuacha pengo katika mechi ambayo amekosekana.

Bwalya ni mzuri katika pasi, lakini hajawahi kutufanyia maajabu katika pasi za mwisho. Anacheza taratibu na hana uamuzi wa haraka katika eneo la mwisho. Nilikuwa napitia takwimu zake za misimu miwili aliyocheza Simba nikasadiki ambacho nilikuwa nakiamini kutoka kwake.

Kwa mfano, mpaka sasa katika msimu huu amefunga mabao mawili tu huku moja likiwa la penalti. Amepiga pasi za mabao tatu. Amecheza mechi 22. Sio takwimu nzuri kwa mchezaji ambaye aliachiwa majukumu ya timu wakati kina Chama hawapo.

Haishangazi kuona mashabiki hawana machozi mengi dhidi yake. Kuna wakati niliwahi kuandika hapa wiki chache zilizopita kwamba kama Simba wakipata kiungo mzuri zaidi ya Bwalya, basi wanaweza kuachana naye.

Kwa mfano, kama ungewaambia watu wa Simba wabadilishane Bwalya na Fei Toto wa Yanga nadhani wengi wangekubali, halafu wale wa Yanga wangekataa. Sababu ni rahisi tu. Angalia namba za Fei Toto msimu huu. Wanacheza katika nafasi sawa, lakini matokeo yao uwanjani ni tofauti.

Kifupi Bwalya hajatuachia kumbukumbu nyingi binafsi kuhusu yeye. Kikubwa ambacho ametuachia ni kwamba alikuwemo katika kikosi kizuri cha Simba ambacho kilifanya vizuri katika michuano ya Afrika kiasi cha kutishia kucheza nusu fainali.

Kwa mfano, haraka haraka unaweza kumkumbuka Miquissone na bao lake dhidi ya Al Ahly. Unaweza kumkumbuka Chama kwa kumbukumbu nyingi ikiwemo bao lake la ushindi dhidi ya Nkana ya Zambia katika Uwanja wa Mkapa. Hauwezi kupata kumbukumbu ya Bwalya katika mizani kama hii.

Ingawa kumekuwa na kificho kuhusu safari ya anakoelekea, inadaiwa kwamba Rally anakwenda zake Afrika Kusini kucheza katika klabu ya Ligi Kuu ya Amazulu. Inabidi abadilike kidogo na kuendana na kasi ya soka la Afrika Kusini. Kule huwa wana kasi zaidi yetu.

Hata hivyo, akiwa kule atajikuta yupo nyumbani kwa sababu ni ligi ambayo ina wachezaji wengi kutoka Zambia, Malawi, Zimbabwe na Botswana. Anachopaswa ni kuongeza kasi yake ya mchezo.

Kila la heri kwake ingawa ni wazi kwamba kwa soka letu hakuna machozi mengi ya kumlilia Bwalya.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz