Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Penalti za Soweto zilivyowaamsha Simba katika ndoto

Simba Orlandooo Kikosi cha Simba

Wed, 27 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simba waliondoka juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg kurejea Dar es Salaam wakiwa na hisia tofauti. Hisia kubwa ni kwamba wameshindwa kufuzu kwenda nusu fainali katika michuano mikubwa ya Afrika.

Hisia nyingine ni kwamba wana ushujaa ndani yao. Binafsi nitachukua hizi hisia za pili. Ndiyo wameshindwa, lakini kiasi wanaweza kupandisha mabega juu. Katika hatua kama hii wamecheza dhidi ya moja kati ya timu kubwa Afrika Kusini, halafu ugenini na hawakushindwa kirahisi.

Kwa ujumla mechi mbili zimeisha sare na wametolewa kwa matuta. Dakika 90 za kwanza Dar es Salaam walishinda kwa bao 1-0. Dakika 90 za pili Soweto wamefungwa bao 1-0. Mabao yote mawili yalikuwa na utata. Lile la Dar es Salaam na hili la Soweto.

Jonas Mkude na Enock Inonga walikosa penalti zao lakini huwa inatokea. Miaka takribani 20 iliyopita, Simba walifunga penalti zao zote tano katika ardhi ya Misri walipocheza na Zamalek. Ilikuwa mechi ya aina kama hii lakini katika michuano tofauti.

Juzi kocha wa Simba, Pablo Gomes aliamua kujaribu kitu tofauti uwanjani. Kucheza katika namna ya kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Ilitazamiwa hivyo kwa sababu alikuwa anaongoza kwa bao moja alilofunga kwa penalti Dar es Salam.

Simba ilianza na walinzi wote watatu mahiri klabuni. Haijawahi kutokea. Walianza Sergi Paschal Wawa, Enock Inonga na Joash Onyango. Ikaanza na walinzi wawili wa kulia, Shomari Kapombe na Israel Mwenda ingawa huyu Mwenda alikuwa anacheza pia kama winga.

Mbele ya ukuta walicheza Jonas Mkude na Sadio Kanoute. Winga ya kushoto akacheza Ousmane Sakho ambaye alikuwa na kazi kubwa ya kumtafuta mshambuliaji pekee kikosini, Chris Mugalu ambaye kipindi cha pili alipewa kadi halali nyekundu.

Ingawa namba ya walinzi ilikuwa kubwa, lakini ukweli ni kwamba hawakuwa wakijipanga vyema katika maeneo yao na kuziba njia ipasavyo. Wakati mwingine sio suala la idadi ni suala la uwajibikaji. Unaweza kuona kuwa Aishi Manula bado alikuwa katika mateso.

Nilidhani Simba wangeishia katika kukaba tu lakini baadaye wakawa na hamu pia ya kufika mbele. Walifanikiwa kupata faulo kuelekea katika lango la wenyeji. Simba pia walitofautiana na timu kadhaa za Tanzania zinazocheza mazingira kama ya jana.

Wakati wakiwa na mpira walau waliweza kumiliki vyema kwa sekunde kadhaa. Hawakupoteza mapema. Ni kitu ambacho walau kilikuwa kinapunguza kasi ya Pirates.

Hata hivyo Pirates walionekana kuwa hatari katika umiliki wa mipira mirefu lakini pia upigaji wa pasi ndefu.

Kama ilivyokuwa kwa bao la Simba Dar es Salaam, basi ndivyo lililovyokuwa bao la Pirates pale Soweto. Mfungaji Mghana Kwame Peprah alionekana ameotea.

Utatuzi wa sheria unadai kwamba mchezaji akiotea upande wa mkono huwa sio ‘offside’ kwa sababu mkono ni kiungo ambacho hakihesabiki katika soka.

Lakini Kwame alionekana kama vile ameotea katika upande wa kifua. Tutaendelea kubishana vilevile kama ambavyo tulibishana kuhusu penalti ya Bernard Morrison Dar es Salaam. VAR zimetumika na huo ndio uamuzi ambao tumepata.

Vinginevyo matukio mengine yaliinufaisha Simba kasoro tukio la Mugalu. Kwa mfano, Pirates wangeweza kupata penalti katika dakika za mwisho mwisho baada ya Kapombe kuushika mpira katika boksi. Hatujaelewa kwa nini mwamuzi aliamuru isiwe penalti.

Kadi nyekundu ya Mugalu ilikuwa halali. Tayari alishakuwa na kadi ya njano na kwa rafu aliyocheza angeweza kustahili kadi nyingine ya njano au kadi nyekundu ya moja kwa moja. Mwamuzi alikuwa na uamuzi wa aina mbili mkononi ambao wote usingeweza kuinufaisha Simba. Aliamua uamuzi wa pili wa kadi nyekundu ya moja kwa moja.’

Nilishangaa kwanini baadaye kocha Pablo alichukua uamuzi wa kumuingiza Meddie Kagere. Nilielewa kwamba Thadeo Lwanga aliingia uwanjani kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi katika eneo la kiungo. Dakika ya 77 kwanini aingie Kagere? Kwamba Simba walikuwa wanasaka bao licha ya kuwa pungufu halafu ugenini?

Walipaswa kufunga milango na kumuomba Mungu wa-ende katika penalti. Haukuwa uamuzi mzuri kutoka kwa kocha ingawa bahati nzuri kwa Simba walifanikiwa kwenda katika matuta. Kilichotokea wote tumeona.

Ni ngumu kuwalaumu wachezaji waliokosa penalti zao ingawa wakati mwingine wanahitaji kutuliza vichwa vyao vyema.

Mchezaji kama Inonga wakati mwingine anacheza kama mchezaji huku akiwa shabiki uwanjani. Hatulizi kichwa chake vyema. Inawezekana alikuwa anawaza namna ambavyo atatamba pindi akifunga penalti kabla hajajua atapigaje.

Mwisho wa siku safari ya Simba imeishia Soweto. Wamejitahidi hasa kwa namna walivyocheza katika mechi mbili za robo fainali dhidi ya Pirates. Zilikuwa mechi nzuri. Pirates ni timu bora kuliko hata ile Kaizer Chiefs ambayo walicheza nayo msimu uliopita.

Nini kinafuata? Watacheza mechi yao wikiendi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga. Kuna ukweli kwamba msimu huu hawana chao katika Ligi Kuu. Walitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere huku Yanga wakiongoza kwa tofauti ya pointi 13.

Hai-onekana kama mechi hiyo itabadili kitu kikubwa kuelekea mwishoni mwa m-simu. Baada ya pambano hili wataendelea kucheza ligi na pia kumalizia hatua iliyofuata ya michuano ya FA ambayo wapo katika hatua ya kusaka kwenda nusu fainali. Tunaweza kuona pambano jingine la nusu fainali kati yao na Yanga.

Kitu kikubwa ni kwamba baada ya kumalizika kwa michuano sasa wanaweza kurudi katika michuano ijayo wakiwa na usajili mpya. Lakini pia wakiwa na kiungo wao, Clatous Chotta Chama ambaye alikuwa haruhusiwi na CAF kucheza michuano hii.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz