Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Operesheni ya kibabe Angola

Oparesheni Simba SC Msafara wa Simba SC wakiwa Uwanja wa Ndege, Luanda nchini Angola

Wed, 12 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Simba walikuwa na usiku mmoja kamili Angola, na hasa katika jiji la Luanda. Walivamia Jumamosi mchana, wakalala usiku mmoja, wakashinda mabao 3-1, wakaenda zao hotelini kuoga wakaondoka zao Luanda na kurudi Dar es Salaam.

Wapongezwe kwa namna walivyofanya kila kitu kuwa rahisi. Ilianzia kwa namna walivyoipanga safari yenyewe. Angola ni nchi isiyoeleweka linapokuja suala la kuunganisha ndege kuifikia nchi yao. Mara ya mwisho nilipokwenda Angola katika pambano lao la mwisho Angola dhidi ya Libolo nililazimika kupitia Dubai kuifikia Angola.

Ndani ya uwanja Simba walifanya operesheni maalumu dhidi ya Primeiro do Agosto. Walikwenda kucheza kama timu kubwa na kupata ushindi wao kama timu kubwa.

Nadhani watu wa Simba walifanya kazi maalumu ya kuwachunguza wapinzani wao na wakajua ni watu wa namna gani.

Mara nyingi tukicheza ugenini huwa tunakuwa na hofu ya kupima nafasi yetu dhidi ya wapinzani, hasa kama unacheza na timu ambayo inacheza katika Ligi tajiri kama Angola. Simba walifanya kazi yao maalumu ya kujua nafasi yao ni ipi katika mchezo na wakafanya kazi yao kwa ufasaha.

Kazi gani? kazi ya kucheza kama wapo nyumbani. Kazi ya kupishana na Waangola na kujaribu kushinda mechi. Ni rahisi kwa sasa kusema kuwa “Kwa Mkapa hatoki mtu”. Wakati mwingine haina haja ya kusema hivyo unapocheza na Primeiro Agosto. Unahitaji kushinda kwao huko huko na kumaliza kazi.

Kuna kundi la wachezaji, viongozi na mashabiki wameanza kuwa na imani chanya dhidi ya baadhi ya wapinzani wao katika michuano ya Afrika. kwa mfano, Al Ahly haiwezi kwenda kucheza na APR pale Kigali huku ikiwa na hofu kwamba haiwezi kumaliza mechi Kigali mpaka irudi Cairo.

Kuna timu ambazo unaweza kuwa na hofu nazo ugenini. Kwa mfano, Al Ahly anaweza kuja Temeke akacheza soka kwa namna ya kusubiri kumaliza mechi Cairo. Anaweza kwenda Casablanca kucheza na Raja akiwa na hofu hiyo hiyo. Lakini hawezi kwenda kucheza na APR au Agosto akiwa na hofu ile ile.

Hiki ndicho ambacho Simba wamekomaa nacho katika mechi mbili za ugenini dhidi ya Nyassa Big Bullets pamoja na wapinzani wao wa juzi. Wamekwenda ugenini wakiwa na akili hii. hauwezi kuipata akili hii kama haujafanya vizuri katika miaka ya karibuni.

Ndani ya uwanja, Simba walicheza kama Simba lakini kwanza unamsifu Juma Mgunda. Tangu akiwa na Coastal Union, Mgunda ni kocha ambaye anapenda timu yake icheze. Anapenda mpira usambae. Hana hofu kubwa dhidi ya wapinzani. Wakati mwingine inamgharimu kwa sababu anashindwa kupima ubora wa kikosi chake dhidi ya wapinzani wake. Haishangazi kuona aliwahi kufungwa mabao mengi na Simba na Yanga wakati akiwa kocha wa Coastal Union.

Hata hivyo alipopata kikosi imara tabia hii ilimsaidia na ndio maana Coastal Union walikwenda mpaka fainali ya kombe la Shirikisho. Nusu fainali walicheza na Azam FC na fainali walicheza na Yanga. Nini kilitokea fainali? Waliziona nyavu za Yanga mara tatu shukrani kwa mabao ya Abdul Hamis Sopu. Bahati mbaya pambano lilimalizika kwa sare ya 3-3 na Coastal wakapoteza katika matuta.

Na sasa Mgunda anatumia akili hii akiwa na wachezaji wakubwa zaidi wakiongozwa na hawa watu watatu. Patrick Phiri, Augustine Okrah na zaidi ya wote, Clatous Chota Chama. Huyu Chama anafanya mambo yatokee. Anafanya kwa namna mbili, ama kutengeneza mabao au kufunga mwenyewe.

Tazama alivyofanya bao la John Bocco lionekane rahisi kule Malawi. Na ndivyo hivyo alivyofanya bao lake mwenyewe juzi pale Luanda lionekane rahisi. Ana utulivu mkubwa wa maamuzi yake. iwe kufunga mwenyewe au kupika bado atafanya kwa utulivu mkubwa.

Lakini Okrah pia anacheza kwa ajili ya timu na anafanya mambo kuwa rahisi uwanjani. Ni tofauti na Ousmane Sakho ambaye anacheza kwa ajili yake mwenyewe. Okrah ana kasi, mbio na ana maamuzi. Kazi yake ina faida kwa ajili ya timu.

Halafu kuna Phiri ambaye amekuja kuchukua majukumu ambayo yaliwashinda mastaa watatu wa Simba msimu uliopita. Yaliwashinda John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere. Hapa kuna mawazo tofauti, inawezekana watatu hawa walikuwa hawafungi vya kutosha kutokana na kucheza sambamba na akina Kibu Dennis na Sakho ambao hawana maamuzi mazuri.

Utatu wa Okrah, Phiri na Chama unaweza kurudisha heshima ambayo walikuwa nayo ndani na nje ya nchi wakati Luis Miquissone alipokuwepo nchini. Hapa katikati Simba walipotea na haishangazi kuona Yanga walirudisha ubingwa wao kwa tofauti kubwa ya pointi msimu uliopita.

Ni katika kucheza kwa swaga hizi hizi ndipo ambapo walau kijana kama Israel Mwenda anaweza kujikuta katika nafasi ile aliyojikuta juzi na kufunga bao zuri. Bao ambalo litarudisha uwezo wake wa kujiamini awapo uwanjani. Ni kitu kizuri kwake kwa sababu viatu anavyovaa ni vikubwa.

Kuna tofauti kubwa kati yake na Shomari Kapombe aliye fiti lakini Simba hawana jinsi zaidi ya kumtumia aonyeshe uwezo wake. anajaribu kuitendea haki nafasi yake kwa kiasi kikubwa. Hauwezi kumpata beki mwingine wa kulia mzawa ambaye anamkaribia Kapombe kwa karibu. Inabidi uwakomaze hawa hawa akina David Kimeta Duchu na Mwenda.

Nini kinafuata baada ya operesheni ya Luanda kufanikiwa? Nadhani wamebakiza safari nyepesi na wanaruhusiwa kuanza kuwaza makundi. Agosto wanaweza kufunga mabao 2-0 na bado wakatolewa. Na ni kweli wanaweza kufunga mabao matatu Dar es salaam lakini Simba nayo lazima itafunga mabao.

Kazi nzito wanayo watani wao watakapokwenda Sudan au Azam watakaporudi Chamazi, lakini Simba wanaruhusiwa kuanzisha sherehe kimya kimya. Sioni kila kilichowatokea kwa Wabotswana kama kinaweza kutokea tena Uwanja wa Taifa. wamejifunza kutokana na makosa na walithibitisha hilo walipocheza dhidi ya Nyasa Bullets Kwa Mkapa.

Columnist: Mwanaspoti