Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Nkane anakwenda kuwa Mrisho Ngassa mwingine au hadithi?

Nkane Pic Data Dennis Nkane

Wed, 5 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Sehemu mbili tatu nimependa jinsi ambavyo staa mpya wa Yanga, Dennis Nkane ametambulishwa kwa lugha ya kiingereza. Nimesoma mahala ametambulishwa kama Wonderkid. Nikasoma kwingine nako ametambulishwa kama Wonderkid.

Waingereza wananilitumia neno hili kwa kinda ambaye anaonekana kuwa na tofauti kubwa na wenzake. Kinda wa maajabu. Mara nyingi ni wachezaji wadogo ambao wanatabiriwa kufanya mambo makubwa siku za usoni. Sijui kama itatokea hivyo kwa Nkane.

Vijana wa Kitanzania wanaotua katika klabu kubwa wanapata wakati mgumu kupenya. Maisha yanakuwa magumu kwao kadri siku zinavyosonga mbele. kaka zao ambao wanawakuta katika klabu kubwa tayari wanakuwa na maisha magumu. Vipi kwao?

Kwa mfano, wikiendi iliyopita timu kubwa mbili zimeshinda. Yanga kamchapa Dodoma City mabao 4-0. Simba alimchapa Azam mabao 2-1. Mabao ya Yanga yalifungwa na mastaa wawili wa Congo, jingine likafungwa na staa wa Uganda, jingine Mtanzania akajifunga. Pambano la Simba mabao mawili yalifungwa na mastaa kutoka Senegal na Mali. Lile za Azam lilifungwa na staa kutoka Zambia. Haya ndio maisha ya kileo katika klabu hizi. Wageni wanatamba kweli kweli kiasi kwamba kaka zetu wanashindwa kutamba katika klabu hizi. Vipi kwa Wonderkid kama Nkane? Anahitaji bahati kuweza kutamba katika Yanga ya leo.

Zamani kina Mrisho Ngassa walitabiriwa kufanya makubwa wakati wakiwa makinda. Alipohama kutoka Kagera kwenda Yanga akafanya makubwa kweli. Ni kama ilivyo pia kwa Simon Msuva. Naye alitabiriwa kufanya makubwa. Alipotua Yanga akitokea Moro United akafanya makubwa kweli.

Vipi kwa Nkane? Atafuata mkumbo huu? Anazungumzwa vizuri na wanaomjua. Nimeangalia video zake anaonekana kuwa anateleza uwanjani. Tatizo ni kwamba katika miaka ya karibuni vijana wetu wanashindwa kucheza hizi timu.

Na wengi wanaoshindwa ni wale wanaocheza nafasi za mbele. katika maeneo ya ulinzi tumeona wengi wakiingia moja kwa moja lakini katika maeneo ya ushambuliaji na kwingineko maisha yamekuwa magumu kwa mastaa wetu.

Mfano, wakati huu Yanga wakimuimba Nkane wakumbuke kwamba Dickson Ambundo hajacheza mechi yoyote ya Ligi. Tunamuona tu katika picha za mazoezini. wakati akiwa na Dodoma City alikuwa staa mkubwa. Ilionekana Yanga hawajafanya makosa kumchukua. Leo hatumuoni.

Upande wa pili kulikuwa na akina mchezaji kama Abdulswamad Kassim. Alichukuliwa kwa mbwembwe kutoka Kagera Sugar na alionekana kama angekuwa kiungo ambaye angefanya makubwa lakini hakuna kilichoendelea katika upande wake.

Akina Yusuph Mhilu wapo hoi. Hatuwaoni wakicheza wala wakitamba. Wazir Junior alikuwa Yanga na aliamua kuchana mkataba. Hawa ndio wachezaji ambao tulitazamia wachukue nafasi zao kama ambavyo akina Ngassa walifanya enzi zao.

Kabla ya hapo walikuwepo akina Adam Salamba. Walikuwepo akina Ditram Nchimbi ambao tuliamini kwamba labda wangeweza kujitokeza kusimama na kuhesabiwa lakini hapana. Haikuwezekana na wageni wameendelea kutamba kwa kiasi kikubwa.

Matokeo yake mpaka leo mshambuliaji wa kizawa wa kutegemewa anabakia kuwa John Bocco tu ambaye naye ameanza kusuasua. Timu ya taifa ikiitwa tunawategemea zaidi Mbwana Samatta na Simon Msuva waje watuokoe. Lakini katika taifa ambalo halina wachezaji wa kigeni tulitazamia wachezaji wa timu kubwa waje watubebe.

Eneo la ulinzi sina mashaka nalo. Dickson Job ametoka mkoani na moja kwa moja amechukjua nafasi yake. Israel Mwenda ametoka KMC kwenda Simba na anaonekana taratibu kuwa mrithi sahihi wa Shomari Kapombe. Anaweza kuirithi nafasi hiyo katika timu yake ya Simba na pia ikiwezekana katika timu ya taifa.

Yanga upande wa kushoto wamemuongeza David Bryson aliyekuwa pacha wa Mwenda katika kikosi cha KMC. Bryson licha ya kusumbuliwa na majeraha wakati anaingia Yanga lakini sasa anaonekana kuwa imara katika upande wa kushoto.

Tatizo kubwa linabakia kwa mastaa wa kizawa wa maeneo ya mbele. sijui kama Nkane atafanikiwa au vinginevyo lakini kama akifanikiwa litakuwa jambo jema kwa taifa. tunahitaji watu wanaoingia na kwenda kupambana na wageni katika nafasi muhimu kama akina Jonas Mkude wanavyofanya.

Hauwezi kuwalaumu kina Nkane kwenda Simba na Yanga ingawa wanapishana na mastaa wa kizawa waliotoka kushindwa. Kila mtu ana bahati yake lakini kikubwa zaidi ni pesa. Kuna pengo kubwa la ofa ya pesa baina ya walionacho na wasionacho.

Kwa mfano, labda Biashara ingeweza kuwa sehemu mwafaka kwa Nkane kuendelea kukomaa lakini kama Yanga wameweka mezani mshahara wa shilingi milioni mbili na kule Biashara alikuwa anachukua laki tano, unadhani angefanya nini zaidi?

Wakati mwingine tunaweza kuwalaumu hawa wachezaji lakini hatujui wanachopitia katika meza za mazungumzo. Na klabu pia huwa zinaambulia chochote kwa ajili ya kujikimu kimaisha. Klabu zetu zinakabiliwa na hali ngumu. Kama klabu inawekewa mezani kiasi cha shilingi milioni 30 kumuuza Nkane hawawezi kukataa. Maisha yao wanayajua wenyewe.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz