Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Mwamnyeto wa juzi, jana na keshokutwa

Edo Pic Data HISIA ZANGU: Mwamnyeto wa juzi, jana na keshokutwa

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

WAKATI fulani mlinzi wa Yanga na timu ya Taifa Stars, Bakari Ndondo Mwamnyeto huwa analaumiwa kuwa na makosa fulani yasiyo ya lazima uwanjani. Ni kweli. Wakati fulani amewahi kuigharimu Yanga kwa makosa ya kitoto uwanjani.

Kwanini Mwamnyeto huwa anatazamwa kwa jicho la mwewe na watu wenye hisia kali? Ni kwa sababu dau lake la kutoka Coastal Union kwenda Yanga liliwashtua mashabiki wengi wa soka nchini. Kampuni ya GSM ililazimika kuipa Coastal Union mkataba wa udhamini wa miaka miwili kwa ajili ya kuinasa saini ya Mwamnyeto.

Na sasa jicho lote linaenda kwake. Anaweza kuwa mchezaji wa ndani aliye ghali zaidi. Ni kitu cha kawaida kuona watu wanataka kujua au kuulizana ‘Mwamnyeto ana kitu gani cha ziada?’ Yanga walifanya walichofanya kwa ajili ya kuhakikisha wapinzani wao Simba hawaipati saini ya Mwamnyeto.

Ni kitu cha kawaida kwa mchezaji aliye ghali kuchunguzwa kama ana uhalali wa pesa iliyotumika kumnunua. Hata Ulaya wachezaji ghali wanajikuta katika wakati mgumu. Wanachunguzwa zaidi kuliko wachezaji walionunuliwa kwa bei chee.

Huyu Mwamnyeto ni beki mzuri. Ana kimo kizuri. Ana mazuri mengi uwanjani kuliko upungufu wake. Hili ndilo jambo la msingi zaidi. Ana uwezo wa kukaba. Ana uwezo wa kucheza kwa kuanzia nyuma. Tatizo lake la msingi sio mzuri sana katika mipira ya juu.

Tatizo lake jingine ni tabia yake ya kujiamini kupita kiasi. Kuna wakati anajikuta anakosea. Bahati mbaya kwake yeye ni mlinzi. Anapokosea katika maeneo ya hatari inakuwa rahisi kwake kuadhibiwa. Imeshawahi kutokea zaidi ya mara moja tangu avae jezi za njano na kijani.

Hata hivyo, leo nasimama upande wake. Tanzania tuna tatizo moja la msingi. Wachezaji wetu wanachelewa kukomaa. Miaka ya karibuni tulikuwa tunawasifu zaidi Kelvin Yondani na Erasto Nyoni. Tumesahau kwamba iliwachukua muda mrefu kukomaa katika soka.

Kunahitajika uwezekaji mkubwa katika mwili na akili ya mchezaji wa Kitanzania ili akupe unachotaka. Kwa sasa

Mwamnyeto ameonyesha dalili (potential) ya kuwa mchezaji mzuri, lakini ukweli ni kwamba sio mlinzi aliyekamilika.

Ukiwatazama hawa kina Sergi Wawa na Josh Onyango ni wachezaji waliocheza nafasi zao kwa muda mrefu na katika michuano mbalimbali ya kimataifa. Huo ndio uwekezaji kwa mchezaji. Hata kina Nyoni na Yondani iliwachukua muda mrefu wa kucheza mechi mbalimbali ngumu za ndani na za nje kuweza kuimbwa katika kiwango ambacho wanaimbwa. Ni ngumu kumpata mchezaji aliyekamilika kutoka Coastal Union. Labda zamani tuliweza kupata wachezaji waliokamilika katika timu hizo lakini siku hizi ni ngumu. Coastal ilicheza wapi michuano ya kimataifa kuweza kutupa mchezaji aliyekamilika?

Hili ni tatizo kubwa la soka letu. Wachezaji wanachelewa kukomaa. Inawezekana Ligi yetu haina ushindani sana, inawezekana watalaamu wetu hawawezi kuwakomaza wachezaji katika kipindi kifupi. Hata hivyo hadithi ni tofauti na wachezaji wa Ulaya.

Mwangalie vyema Erling Haaland jinsi ambavyo anaonekana kukomaa mapema. Sawa, huenda bado anahitajika kukomaa zaidi lakini ukimtazama leo unapata picha jinsi gani anavyocheza kama mtu mzima. Kwetu mchezaji mwenye miaka 20 hawezi kucheza kama Haaland.

Mwamunyeto yupo katika mchakato wa kuwa mlinzi kamili. Bado hajatimia. Anahitaji kucheza mechi nyingi ngumu za kimataifa akiwa na Yanga na timu ya taifa. Hizi mechi zitamkomaza kwa kiasi kikubwa lakini kwa sasa bado hajakomaa. Mashabiki na wachambuzi wasiwe wepesi sana katika kumlalamikia kila anapofanya kosa.

Wachezaji ambao wana vichwa laini ni rahisi kupotea kama wakiandamwa sana. Wanajikuta hawajiamini tena. Wengine wanajikuta wakiangukia katika timu za kawaida ambapo baadaye wanaibuka kuwa wachezaji wazuri tena na timu kubwa zinaanza kuwataka.

Mfano ni mzuri ni mchezaji kama Hassan Dilunga. Alipokuwa Yanga nadhani watu wa Yanga hawakumlea vizuri. Sijui walitazamia nini kwa mchezaji wa aina yake. alitupwa katika rundo la mastaa akina Thaban Scara Kamusoko, Haruna Niyonzima na wengineo na bado watu wakatazamia mambo makubwa kutoka kwake.

Hakuna sababu ya kumpoteza Mwamunyeto. Kesho yake ipo salama kwa sababu mpira anajua na umbo lake ni nadra sana kulipwa kwa wachezaji wa kileo hapa nchini. Anahitajika kucheza kwa muda mrefu kabla ya kukomaa zaidi.

Tuna bahati mbaya hii hapa nchini. Wachezaji wa leo sio kama akina Edibily Lunyamila ambalo walikomaa wakiwa shuleni na wakaitwa katika timu ya taifa wakiwa wamemaliza mtihani wa Kidato cha nne. Hawa akina Mwamunyeto wanahitaji muda. Jaribu kumtazama Shomari Kapombe. Ni mchezaji aliyekomaa. Kila nikimtazama Kibwana Shomari najikuta namtazama Shomari Kapombe wa miaka saba iliyopita. Baada ya muda Shomari Kibwana atakuwa kama Shomari Kapombe. Anahitaji muda tu kwa sasa. Anahitaji kucheza mechi nyingi za kimataifa akiwa na Yanga na timu za taifa.

Tujifunze kuwajua wachezaji. wachezaji wengi huwa wanapotea kwa sababu ya kutoaminiwa au kushambuliwa kwa maneno na mashabiki wa timu zao. Hata Simon Msuva katika umri mdogo alikuwa anazomewa na mashabiki wa Yanga. Leo ni staa wa klabu ya Waydad Casablanca. Yanga wanaamini kwamba Simon huyu ni yule yule ambaye walimzomea? Sina uhakika kama wana kumbukumbu hizo.

Unaweza kuliacha hili kwa mashabiki na wanachama lakini wakati mwingine unaweza kukuta hata kiongozi wa timu hajui namna ya kumlea mchezaji. Na yeye anaingia katika kundi la mashabiki kumshambulia mchezaji wake bila ya kujua kwamba mchezaji husika anahitaji mchakato mzuri wa kumfanya kuwa staa.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz