Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Mtoto wa mama Efua alivyochafua kundi D

Bernard Morrison Afunga Mtoto wa mama Efua alivyochafua kundi D

Wed, 23 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Soka la Afrika mara nyingi kila mtu anashinda kwake. Labda Ulaya kuna maajabu mengi ya soka la ugenini kuliko Afrika. Kwa mfano, mechi ijayo kati ya PSG na Real Madrid pale Santiago Bernabeu - Madrid wanaweza kuchapwa tena nyumbani licha ya kuchapwa pale Paris, Ufaransa.

Soka la Afrika ndipo ambapo wengi wanashinda nyumbani halafu wanafungwa ugenini. Ukitaka kulichafua kundi na kuweka taswira tofauti fanya kile ambacho Bernard Morrison alichofanya juzi jioni pale jijini Niamey nchini Niger.

Morrison alifunga kwa kichwa bao maridadi la kusawazisha katika pambano dhidi ya US Gandermarie Nationale ya Niger huku Simba wakiwa ugenini katika mji wenye vumbi wa Niamey. Bao hilo limeifanya Simba iongoze kundi.

Kabla hatujaenda mbali tujiulize Morrison alifungaje bao hilo? Ni uzembe mkubwa kutoka kwa walinzi wa wapinzani. Kama Simba, Yanga, Azam au Taifa Stars ingefungwa bao hilo katika mechi ya kimataifa kama ile basi tungelia na wachezaji wetu zaidi kuliko kumsifia mfungaji.

Mfupi kama alivyo, Morrison anafungaje kiurahisi katika mpira wa kona? Tatizo alikuwa peke yake. Kona ya Shomari Kapombe ilifika katika kichwa chake akiwa hajakabwa. Rafiki zetu walikuwa wamekaba kwa macho tu wakitegemea mpira utawafikia waokoe.

Kwa sasa Simba wana pointi nne kibindoni. Wengine wawili - ASEC na Raja wana pointi tatu wakati rafiki zangu wa Niger wana pointi moja waliyoiambulia kutoka kwa Simba juzi jioni pale nyumbani. Kundi limechanganya.

Simba anaweza kuvuka kiulaini katika hili kundi kama tu akishinda mechi zake mbili za nyumbani dhidi ya hawa rafiki zetu wa Niger pamoja na Berkane. Haitajalisha sana nini kitatokea katika mechi zao mbili dhidi ya Berkane pale Morocco au dhidi ya Asec pale Abidjan.

Ukifikisha pointi 10 ni ngumu kutofuzu hasa pale inapohitajika timu mbili zipite katika kundi ambalo kabla ya Morrison kusawazisha kila timu ilipaswa kuwa na pointi tatu. Kila mmoja angekuwa ameshinda mechi moja nyumbani na kufungwa mechi moja ugenini. Ni Morrison tu ndiye ambaye amevuruga utaratibu.

Nini kinafuata? Ni vigumu kutabiri. Kuna mambo ya kushangaza kidogo. Awali nilidhani Berkane kwa sababu ni Waarabu wa Morocco basi wangekuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kushindana na Simba katika kuongoza kundi hilo. Hata hivyo ninaanza kuwa na mashaka nao.

Mashaka yangu yalianza katika pambano la kwanza walipocheza na rafiki zetu wa Niger. Ilikuwaje wageni wakapata mabao matatu ugenini? Kumbuka pambano lilimalizika kwa Berkane kushinda mabao 5-3. Ushindi haukuwa tatizo. Tatizo lilikuwa kwa US Gendermarie kupata mabao matatu katika ardhi ya Morocco.

Hakuna shaka ukuta wa Berkane unavuja. Na zaidi ni kwamba juzi wameshindiliwa mabao matatu wakiwa ugenini Abidjan. Ina maana mpaka sasa Berkane wamefungwa mabao sita katika mechi mbili tu. Simba wameruhusu mabao mawili katika mechi mbili.

Tatizo ni kwamba Simba haifungi sana. Imefunga mabao matatu tu lakini ni wazi kwamba wapo imara. Je Simba anaweza kupata matokeo Morocco? Hili ni swali. Akipata matokeo ya kushinda au kupata sare pale Morocco basi anaweza kujikuta akifuzu hatua inayofuata bila ya kumaliza mechi zake hasa ukizingatia Simba anajua kutumia vyema uwanja wa nyumbani.

Itakuwa mechi ya kuvutia. Kuna uwezekano Simba ikapata mabao lakini wasiwasi unakuja kwamba na Simba nao wanaweza kufungika. Mpaka sasa wamefungwa mabao mawili tu ikiwa ni timu iliyofungwa mabao machache katika kundi lake, lakini kumbe wanafungika.

Simba watalazimika kufanya kazi hii ngumu katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Berkane. Kwanza kabisa kazi itaanzia Morocco. Maisha yatakuwa magumu Morocco. Berkane wametoka kufungwa ugenini na hawatataka kufanya makosa nyumbani. Watafanya kila hila.

Pili, wanajua kwamba wakishinda pambano hilo watakuwa na pointi sita wakati Simba atabakiwa na pointi nne. Lakini zaidi watataka kumalizana vyema na Simba huko Morocco kwa sababu baada ya wiki moja watakuja Dar es Salaam kucheza na wakali hao wa porini.

Baada ya hizi mechi mbili Simba watapumzika kwa kucheza na rafiki zao wa Niger. Haitakuwa mechi ngumu kwa Simba. Kama ambavyo ilikuwa juzi basi ndivyo ambavyo itakuwa Dar es Salaam. inatazamiwa Simba itachukua pointi zote tatu.

Tatizo litakuja wakati watakapofunga safari ya kwenda Abidjan kucheza pambano lao la mwisho dhidi ya Asec. Litakuwa pambano la kufa na kupona kwa sababu nahisi hadi dakika hizo Asec anaweza kuwa anasaka nafasi kwa sababu kumbuka kwamba mbele yake kuanzia sasa ana mechi mbili dhidi ya Gandermarie ugenini na nyumbani. Anaweza kukusanya pointi nne au sita hapo.

Endapo pambano la Asec na Simba likaangukia kuwa la kufa na kupona maisha yatakuwa magumu kwa Simba kwa sababu litakuwa pambano la ugenini. Aliyeipanga hii ratiba ni afadhali angeifanya Simba imalize pambano la mwisho nyumbani au imalize ugenini kwa Gendermarie.

Pambano likiwa la kufa na kupona kwa Asec maisha yatakuwa magumu kwa Simba. Haitakuwa rahisi pale Abidjan.

Taswira ilijionyesha katika pambano la kwanza baina yao pale Temeke, lakini taswira pia imejionyesha kwa kile ambacho kimewatokea Berkane juzi walipokwenda Abidjan. Kumbe kwao ni kugumu.

Kitu kingine cha msingi kwa Simba kwa sasa ni kuombea Gendemarie asikubali kuwa kibonde wa kundi. Kile ambacho kimefanywa na Simba pale Niger kisirudiwe na Berkane au Asec. Walau waugeuze uwanja kuwa mgumu kwa wengine ili wawapunguze kasi Berkane na Asec. Vinginevyo maisha yatakuwa magumu kwa Simba.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz