Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Mpole chanda chema ambacho hakikuvikwa pete

George Mpole Vv George Mpole

Wed, 31 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna mahala wahenga waliwahi kutuambia ‘Chanda chema huvikwa pete’. Inawezekana walikuwa sahihi lakini kumbe haikuwa hivyo kila mahala. Kuna wakati chanda chema hakivikwi pete.

Nakumbuka hivi kila ninapomuona George Mpole katika jezi ya Geita Gold kwa mara nyingine. Mabao yake 17 aliyofunga msimu uliopita hayakusaidia kumsogeza popote ndani wala nje ya nchi. Nilidhani yangetosha kwake kupata timu kubwa ya kuchezea. Haikuwa hivyo.

Nilidhani hata Simba wangekimbizana kuisaka saini yake kama ambavyo walikuwa wanashangilia katika mbio zake za kukisaka Kiatu cha Dhahabu dhidi ya Fiston Mayele wa Yanga. Hata hivyo, Simba waliamua kukaa kimya na badala yake wakaibuka kwa Habib Kyombo ambaye tayari alishasaini Singida Big Stars.

Nilidhani Azam wangeenda kasi na kuinasa saini yake. Hapana. Hawakufanya hivyo na badala yake wakatumia misuli kuinasa saini ya staa wa Coastal Unioni na Timu ya Taifa, Abdul Hamis ‘Soup’ ambaye nyota yake iling’ara zaidi katika pambano la mwisho la msimu dhidi ya Yanga fainali za Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Kwanini Mpole alidoda sokoni licha ya kufunga mabao 17? Inawezekana kuna sababu nyingi. Labda wakubwa waliamini kwamba alikuwa ni mchezaji mwenye maajabu ya msimu mmoja. Wazungu huwa wanaita ‘One season wonder’. Labda ni kwa sababu Mpole alishacheza ligi lakini hakuwahi kuonyesha maajabu hayo hapo kabla.

Kama Mpole angekuwa amefunga mabao 14 msimu mmoja kabla ya huu, huenda klabu zingeamini alikuwa mfungaji asilia zaidi. Hata hivyo kulikuwa na aina ya wasiwasi kwa namna ambavyo ghafla aliibuka kutoka kusikojulikana kuwa mfungaji bora.

Huenda msimu huu Mpole akifunga mabao mengi klabu zitajihakikishia ni mfungaji asilia na msimu wake uliopita hakuwa amebahatisha. Hata hivyo, mpaka sasa hajafungua akaunti yake ya mabao wakati hasimu wake wa msimu uliopita, Mayele tayari amecheka na nyavu mara mbili.

Sababu nyingine ambayo huenda imepelekea wakubwa wasimchukue Mpole ni kutokana na kutoamini viwango vya wachezaji wa klabu nyingine nchini. Kuna baadhi ya mastaa walichukuliwa kwa mbwembwe wakiwa katika klabu zao lakini walipofika Simba na Yanga hawakuonyesha makali hayo.

Miongoni mwao ni Waziri Junior. Msimu mmoja kabla hajatua Yanga alikuwa amefunga mabao 14 akiwa na klabu ya Mbao FC ya Mwanza. Baada ya hapo Yanga wakamfanya kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa klabuni. Alipofika Yanga makali yake yakapotea. Mabao ambayo alikuwa anakosa usingeweza kuamini.

Walikuwepo pia kina Charles Ilamfya. Aling’ara akiwa na jezi ya KMC. Simba wakawania saini yake. Walipompata hakuna kitu kikubwa alichoonyesha. Mwishoni mwa msimu wakampeleka kwa mkopo katika klabu yake ya zamani. Mkataba wake ulipoisha wakamuonyesha mkono wa kwaheri.

Bahati mbaya sio kwa washambuliaji tu. Hata wachezaji wa nafasi nyingine nao huwa hawaaminiki pindi wanapotua timu kubwa. Ni wachache ambao wamefanikiwa moja kwa moja kutinga katika timu kubwa na kuonyesha makali yao moja kwa moja. Katika siku za karibuni katika timu kubwa za Kariakoo wanaweza kuwa Dickson Job na Kibwana Shomari.

Lakini huenda Mpole pia ameponzwa na kasumba ya klabu zetu kuamini zaidi washambuliaji kutoka nje. Kuna kila sababu ya kutozilaumu klabu kwa kununua washambuliaji kutoka nje kwa sababu katika miaka ya karibuni wameibeba ligi yetu.

Kina Meddie Kagere, Amiss Tambwe, Prince Dube, Fiston Mayele, Steven Sey na wengineo walijipambanua kuwa washambuliaji hatari katika ligi yetu miaka ya karibuni. Ni John Bocco pekee ndiye ambaye alikuwa anapambana nao. Labda msimu uliopita Mpole naye ndiye ambaye ametutoa kimasomaso.

Jaribu kuangalia wakati Rais wa Yanga, Hersi Said akisaka mshambuliaji. Aliamua kwenda kwa Lazorius Kambole wa Kaizer Chiefs ambaye rekodi inaonyesha alifunga bao moja tu msimu uliopita. Kwa nini hakumuamini Mpole ambaye alifunga mabao 17 katika msimu ulioisha?

Angeweza kumpata Mpole kwa bei rahisi zaidi kuliko Kambole ambaye nina uhakika dau lake lilikuwa juu zaidi kutokana na malipo ya dola huku pia Yanga wakilazimika kumlipia vibali vya kazi. Hata hivyo, tunarudi katika lugha ileile ya kutowaamini wachezaji wa ndani.

Lakini inawezekana mabosi wa mjini hawakumuamini Mpole kwa sababu ya aina yake ya mabao. Labda wameona amefunga mabao rahisi ingawa binafsi siamini kama kuna mabao rahisi katika soka. Mayele alikuwa anafunga mabao magumu na yanayovutia zaidi kuliko Mpole lakini lazima uheshimu nafasi aliyokuwa anajiweka katika kufunga.

Mwisho wa kila kitu hata kama Mpole hakupata timu kubwa Tanzania lakini angeweza kupata timu kubwa nje ya nchi. Mabao aliyofunga na kuibuka kuwa mfungaji bora yalitosha kumpa wasifu wa kucheza nje. Dunia ina tatizo la wapachika mabao. Unafungaje mabao 17 ya msimu na bado ukashindwa kucheza nje?

Zaidi ya hayo mabao lakini Mpole ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars aliyeanza kuifungia mabao timu ya taifa.

Nadhani ni ukosefu wa mawakala wa uhakika au wasimamizi wa uhakika kuifanya kazi hii. Angeweza kwenda popote kama wakubwa wa hapa walimsusa.

Columnist: Mwanaspoti