Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Morrison kutoka Yanga hadi kutua Yanga

Bernard Morisson Bm3 Morisson

Thu, 7 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kama biashara ya magendo hivi. Juzi usiku Yanga walitangaza kumrudisha Bernard Morrison saa sita na dakika moja usiku. Kabla ya hapo ilikuwa moja kati ya siri ambazo zilitunzwa vibaya zaidi katika soka letu. Karibu kila mtu alikuwa anafahamu kwamba Morrison anarudi Yanga.

Ni rasmi kwamba ametua Yanga lakini ebu tujadili mambo yasiyo rasmi ambayo yanaweza kuwa sababu ya yeye kurudi Yanga. Kifupi Morrison ni Mfanyabiashara mzuri tu wa soka. Ni tofauti na wachezaji wetu wazawa. Amekuja nchini akiwa hana mapenzi na Yanga wala Simba.

Awali alichungulia kwamba kwa wakati ule maslahi yalikuwa Simba. Yanga walikuwa wanajikokota ndani na nje ya uwanja. Rafiki yangu, Ghalib Said Mohamed alikuwa hajatanua mbavu zake kwa asilimia mia moja kwa ajili ya Yanga.

Morrison alikuwa mchezaji staa zaidi Yanga lakini wote hatukujua kwamba akili yake ilikuwa kufuata maslahi ya Simba. Akatumia mbinu za maudhi za kuwachosha Yanga ili aende zake. Akawashinda katika mkataba. Lakini zaidi ni kwamba kabla hajaondoka zake alihakikisha wanamchoka.

Alimtolea kisu mwandishi wa kambi pale Regency hotelini. Akacheza ovyo pambano la watani wa jadi. Akatolewa wakati wa mapumziko akaondoka zake uwanjani kuwahi nyumbani kwake. Mashabiki walimchoka ingawa viongozi walimng’ang’ania.

Alipokwenda Simba akatangaza ‘mapenzi’ yake na Simba. Akadai ni chuo. Hapo hapo akadai aliipenda Simba tangu zamani na aliwahi kuitazama Simba katika shughuli yao ya Simba Day mwaka mmoja kabla hajaja nchini kucheza soka.

Alipoanza kazi yake, upande wa pili ukaendelea kujipanga zaidi. Ghalib akatanua mbavu zake haswa. Noti zake zikaanza kuonekana hadharani zaidi. Timu ikahama Regency kwenda Avic Town Kigamboni. Mastaa wakatiririka. Yanga iliweza hata kukodi ndege binafsi kutoka Dar es Salaam hadi Port Harcourt Nigeria. Timu yenye pesa huwa haijifichi.

Zaidi ya kila kitu Yanga ikaendelea kuchanua uwanjani hasa msimu huu. Nadhani Bernard aliona uwezekano wa kurejea Yanga. Aliiweka Yanga katika akiba yake ya mawazo. Na hapa ndipo alipoanza visa vya hapa na pale. Ni kama vile vile tu ambavyo aliwahi kuwafanyia Yanga.

Simba ina misimamo zaidi, hasa nyakati hizi ambazo ina wachezaji walio bora. Wakati Ligi ikiwa imebakiza miezi miwili imalizike wakamuweka pembeni kwa likizo ambayo haijawahi kueleweka katika soka. Ni mpaka majuzi Morrison alipokuja hadharani kutuambia ilikuwa ni likizo ya aina gani.

Kitu ambacho sijawahi kukielewa ni kama watu wa Yanga walianza kuwasiliana naye muda gani kwa sababu katika muda mwingi wa maisha yake ya soka pale Simba yeye alikuwa katika vita nao ya kisheria ya mkataba pale CAS.

Ni namna gani mambo yaligeuka wakaanza ‘mapenzi’ ya siri siri na mabosi wa Yanga hapo nashindwa kuelewa. Ninachojua tu ni kwamba ghafla bifu lake na Haji Manara mitandaoni likatoweka. Lakini hata kama mimi sifahamu, basi inawezekana viongozi wa Simba walifahamu na ndio maana wakamuweka kando.

Nini kinafuata? Mambo ni mengi muda ni mchache. Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakigawanyika kuhusu kile ambacho Morrison anaweza kuwafanyia baada ya kurudi. Kiwango chake akiwa Simba kimewaganya Wanasimba, na hata Wanayanga ambao hawajui watazamie Simba.

Akiwa na Simba Morrison hakuwa na mwendelezo wa bora ingawa katika siku zake huwa hakuna mchezaji kama Morrison linapokuja suala la mawinga. Ni winga wa kisasa haswa. Ni zaidi ya wote aliowaacha Simba, na ni zaidi ya wote atakaowakuta Yanga. Zaidi ya Jesus Moloko na wengineo.

Tatizo ni kwamba kiwango chake hakupi kila wikiendi. Wiki hii yupo hivi, wiki ile yuko hivi. Labda ndio maana Simba waliamua kuachana naye kimya kimya. Kama angekuwa anacheza kama alivyocheza dhidi ya Red Arrows ya Zambia kila wiki wikiendi najua kwamba Simba wangepambana kumpatia mkataba mpya wakati msimu ukiendelea.

Yanga wanaweza kujipa matumaini katika jambo moja tu. Kwamba labda wakati huu Morrison anaweza kutulia na kupunguza mambo mengi ya nje ya uwanja kwa sababu hatakuwa na mahala pa kukimbilia kama akileta tabia za kitoto.

Kwamba uwezekano wa Morrison kuichezea Simba mara ya pili haupo. Labda kama akiharibu Yanga anaweza kwenda Azam lakini kwa mchezaji mpenda sifa kama yeye anajua kwamba akienda Azam ambayo haina mashabiki wengi basi atasahaulika mapema katika ramani ya soka letu.

Hawa wachezaji wa kigeni, hata kina Prince Dube, wanatamani kucheza Simba au Yanga kutokana na sifa za mitaani zilizopo katika mashabiki wa klabu hizi. Morrison anajua fika kwamba anaweza kupata pesa nyingi akiwa na Azam lakini hawezi kupata sifa nyingi. Ni kama tunavyowanyima sifa zao kina Kenneth Muguna licha ya umahiri wao.

Kulikuwa na uwezekano wa Morrison kurudi Yanga. Achilia mbali uwezo wake lakini pia inawezekana kulikuwa na hisia za kisasi kutoka kwa mabosi wa Yanga. Simba walishamaliza kisasi chao wakati Marehemu Zacharia Hans Poppe alipolazimisha kumpeleka Yanga. Lakini Yanga wametimiza sasa hivi. Sioni kama Simba wanaweza kurudia utoto huu.

Nini kinafuata kwa Yanga. Akiwa katika ubora wake, Yanga watakuwa na safu ya ushambuliaji iliyo tishio na ambao inatumia akili nyingi. Fikiria uwepo wa Morrison, Aziz Ki, Fiston Mayele na Fey Toto. Ni kitu kinachoogopesha kama watakuwa na utimamu wa mwili na akili.

Hata hivyo, itategemea na Morrison anataka kuwa mchezaji wa aina gani Yanga. Kipaji anacho lakini utulivu wake katika kazi yake ya msingi ya kucheza soka ni kitu muhimu zaidi kwake. Akifanya hivyo Yanga watamfaidi.

Columnist: Mwanaspoti