Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Manula anatufikirisha ukweli mchungu

Aishi Manula Top Golie Aishi Manula

Wed, 13 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Nilimsikiliza Aishi Manula, kipa wa Simba na timu yetu ya taifa. Alikuwa akihojiwa wakati amekwenda katika tuzo za Ligi Kuu pale hoteli ya Rotana mapema wiki iliyopita. Aliongea baadhi ya mambo yaliyonifikirisha wakati akihojiwa.

Aishi alikuwa amehojiwa uwezekano wa yeye kucheza nje ya nchi. Alijibu kwa ufasaha kwamba yeye hawezi kwenda kucheza nje ili mradi amekwenda kucheza nje. Kwamba huwa anapokea ofa kutoka katika timu za kawaida tu na yeye lengo lake ni kucheza michuano mikubwa ya CAF ambayo Simba inampatia nafasi.

Lakini hapo hapo akaongeza kwamba kuna ofa nyingine huwa ni ndogo kuliko ofa anayopewa klabu yake ya Simba. Hili linawezekana kwa kiasi kikubwa. Wakati huu akiwa ametoka kusaini mkataba mpya, Aishi amepewa kiasi kikubwa cha fedha na waajiri wake. Nadhani ni zaidi ya shilingi 200 milioni.

Mkataba wake na Simba ulikuwa umekata roho na Azam walipania kumrudisha nyumbani Chamazi kwa gharama zozote zile. Simba wamepambana hasa kuinasa tena saini ya Aishi. Kumbuka kwamba walikuwa hawapambani kwa mdomo. Walikuwa wanapambana kipesa.

Lakini Aishi aliongeza kwamba hata wachezaji wa kigeni wamekuwa wakivamia katika soka letu kwa sababu wanapata pesa nyingi ambazo inawezekana hawawezi kuzipata makwao. Jambo hili lina ukweli wake. Mfano, siioni timu ya Zambia ambayo inaweza kumpa Clatous Chama pesa nyingi kama Simba inavyofanya.

Kufikia hapa Aishi alikuwa amenifikirisha mambo. Suala la kwanza ni suala binafsi zaidi. Suala la kipato. Ni kweli Aishi hawezi kwenda Amazulu ya Afrika Kusini kama hawajafikia dau ambalo Simba imemuahidi. Kwa kujitazama yeye mwenyewe na familia yake ni lazima ataangalia pesa zaidi.

Lakini hapo hapo tunajadili jambo jingine. Aishi amesema anataka kujikita katika michuano ya kimataifa na klabu kama ya Amazulu haiwezi kumpa nafasi hiyo. Simba wanampa nafasi hiyo. Huu ni ukweli mwingine ambao hatuwezi kuupinga.

Ina maana Aishi anataka akitoka hapa akacheze Mamelodi, Kaizer Chiefs, Waydad Casablanca na timu nyingine zenye hadhi hizo. Timu ambazo zitampa nafasi kama ambayo Simba wamekuwa wakimpa kila kukicha. Tatizo ni kama hizo timu hazimpi ofa. Labda ndio maana tunaendelea kumuona nchini.

Lakini kuna jambo jingine hapa ambalo inabidi tulitazame kwa jicho la mwewe. Kwa maslahi ya taifa timu kama Amazulu inaweza kumpa ofa Aishi kucheza katika Ligi yenye ushindani zaidi kila wikiendi tofauti na anapokaa katika lango la Simba huku akicheza mechi chache za kishindani katika Ligi.

Ina maana mchezaji kama yeye wikiendi hii atacheza dhidi ya Orlando Pirates, wikiendi ijayo atacheza dhidi ya Supersport United, wikiendi nyingine atacheza dhidi ya Kaizer Chiefs halafu ile nyingine atacheza dhidi ya timu nyingine ngumu.

Nadhani hiki ndicho ambacho Wazambia wataenda kunufaika kwa Rally Bwalya baada ya kuondoka Simba na kutimkia Amazulu. Wazambia tayari wanakuwa wameongeza mchezaji mwingine katika ardhi ya Afrika Kusini. Huu ni ukweli mchungu.

Hata hivyo hauwezi kumlaumu Aishi kwa sababu mwisho wa siku aanza kuangalia maslahi yake binafsi kwanza kisha maslahi ya taifa baadae. Ni wangapi kati yetu tusingechukua maamuzi kama yake? Kwamba kama Aishi angekuwa mdogo wako ungekubali achukue shilingi 50 milioni za Amazulu na kuacha shilingi 200 milioni za Simba?

Mfano huu upeleke kwa raia wa Burkina Faso. Inawezekana kwa kiasi kikubwa wangependa kumuona kiungo wao, Aziz Ki akienda kucheza Ulaya au Asia. Lakini ameamua kuja Afrika Mashariki kwa sababu ya maslahi yake binafsi. Zamani hili suala lilikuwa linanitatiza kwa sababu niliamini kwamba wachezaji walipaswa kuweka maslahi ya taifa mbele.

Kadri siku zinavyokwenda mbele ndivyo nilivyobadilisha mtazamo wangu. Wachezaji wanapaswa kuweka maslahi yao binafsi mbele kama ambavyo Wanasiasa wa Afrika wanavyofanya. Vinginevyo ni rahisi kufa maskini huku ukichekwa na wale wale ambao walikuwa wanakutukuza zamani.

Wakati fulani wachezaji wa Kiingereza wote walikuwa wanacheza kwao. Ni nadra mpaka sasa kuona mchezaji wa Kiingereza akicheza nje. Lakini kumbe huwa hawafanyi hivyo kwa sababu ya kukosa uwezo, au kupenda sana kucheza nyumbani. Wanafanya hivyo kwa sababu ya ofa ambazo wanapokea.

Tatizo lililopo kwa wachezaji wetu ni kwamba tukiachana na wachezaji wachache wa aina yake ambao wanachota pesa za klabu kubwa, bado kuna makundi mengine ya wachezaji ambao hawaeleweki. Mfano ni yule mchezaji ambaye anakataa ofa kubwa kutoka katika klabu ya nje kwa ajili ya kuendelea kuwepo nchini.

Mchezaji ambaye anakataa dau la kucheza TP Mazembe au Al Marreikh kwa ajili ya kuendelea kucheza nchini anashangaza kidogo. Anko Mrisho Ngassa aliwahi kukataa mshahara mkubwa kutoka kwa Al Marreikh akasaini timu yake pendwa Yanga. Hapa kuna tatizo.

Lakini pia kuna kundi la wachezaji ambao wanacheza katika timu za kawaida lakini mawazo yao makubwa yapo Simba na Yanga tu. Hawafikirii kuondoka moja kwa moja kutoka katika timu zao kwenda nje. Wanafikiria ofa za Simba na Yanga kwanza. Hapa kuna tatizo.

Shukrani kwa wachezaji kama Nizar Khalfani, Novatus Dismas, Kelvin John na wachache wengine ambao walichomoka moja kwa moja kwenda nje bila ya kugusa Simba na Yanga. Wengine wanaanzia kwa Simba na Yanga kwanza kisha wanafikiria nje.

Lakini pia Aishi alizungumzia jinsi wachezaji wengine wanavyofuata maslahi nchini. Ni kweli. Hawa ndio akina Chama. Kitu kizuri kwa mataifa yao ni kwamba hata wakituletea wachezaji hawa bado pia wana wachezaji wengi mahiri nje ya nchi yao ambao wanacheza kwingineko.

Mfano, katika kikosi cha Zambia Chama sio mchezaji tegemeo. Kuna wakati haitwi katika kikosi cha timu ya taifa na hakuna anayeshtuka. Kikosi chao kimesheheni mastaa. Ni kama akina Bernard Morrison ambao hawaitwi Ghana lakini Ghana ina bwana kubwa la kuvua wachezaji wengine mahiri. Tatizo tunalo sisi.

Columnist: Mwanaspoti