Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Kwanini mastaa wetu wanaondoka na kurudi mapema?

Chama Mbeya Clatous Chota Chama, kwa sasa amerejea tena Simba SC

Wed, 19 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kwanini mastaa wakubwa wa Ligi yetu huwa wanaondoka na kisha kurudi nchini kwa moyo mkunjufu. Wawe wa kigeni au wazawa, huwa wanaondoka kwa mvumo mkubwa kisha wanarudi baada ya miezi kadhaa tu.

Clatous Chota Chama ni mfano mwingine. Jina kubwa katika soka la Tanzania. Aliondoka nchini kwenda Morocco kucheza katika klabu ya Berkane. Kila mtu aliamini kwamba Chama angeenda kuwa staa mkubwa katika klabu hiyo.

Miezi sita baadaye Chama tunaye nchini. Rafiki yake, Tuisila Kisinda ameendelea kuwepo nchini humo. Kama ungeulizwa ni nani angeendelea kubaki na nani angerudi ungeweza kuamini kwamba Tuisila angerudi na Chama angebakia Morocco. Imekuwa tofauti.

Chama ni mwendelezo wa majina mengi makubwa nchini ambayo yaliwahi kuondoka na kisha kurudi kimya kimya bila ya matarajio ya mashabiki. Wakati mashabiki wakiamini kwamba mchezaji fulani anakwenda kuwa mchezaji mkubwa nje ya nchi hali inakuwa tofauti. Anarudi kimya kimya.

Hata katika ubora wake, Emmanuel Okwi alikuwa hivi hivi kama Chama. Tulikuwa tunaamini kwamba siku akiondoka ataenda kuwa mchezaji mkubwa nje lakini ghafla akawa anarudi nchini. Mpaka mpira ulipoanza kuondoka miguuni ndipo alipoondoka moja kwa moja.

Kwanini mastaa wanarudi? Kitu cha kwanza ni utamu wa maisha ya kijamii Tanzania. Nimekuwa nje mara kadhaa. Hakuna nchi nzuri kuishi kama Tanzania. Hata Watanzania wanaoishi nje watakwambia tu kwamba wanaishi huko kwa sababu ya kusaka pesa na si vinginevyo.

Tanzania imefuata misingi ya Ujamaa. Watanzania wanapendana. Ukiwa staa mkubwa Tanzania unashangaa ni namna gani watu wanakupenda kiasi cha kukununulia kinywaji wakati wewe una uwezo wa kipesa kuliko anayekununulia.

Haya ndio maisha ambayo akina Chama wamekuwa wakiishi. Ni rahisi kutengeneza ufalme Tanzania kuliko Morocco. Ukienda nje unaanza upya wakati hapa unaimbwa mitaani na pia unatukuzwa mitaani. Inachukua muda kutengeneza ufalme nje ya mipaka yako.

Ni Tanzania pekee ndipo ambapo mchezaji anaweza asitumie mshahara wake. Wachezaji wetu mastaa wanaishi nje ya mishahara yao. Unashangaa kuona mashabiki wenye uwezo wanawalea wachezaji wetu bila ya sababu za msingi.

Mchezaji akienda katika nchi za nje anajikuta analazimika kuishi katika misingi halisi ya mwanasoka wa kulipwa ambayo hakuzoea. Zaidi ya kila kitu anajikuta akiwa sio kipenzi cha mashabiki. Ni baada ya kazi ngumu ndipo walau unaweza kuanza kuwa kipenzi cha mashabiki. Lakini hata ukiwa kipenzi cha mashabiki malezi ya mashabiki kwao yanakuwa tofauti.

Kitu kingine ambacho kinawarudisha sana mastaa wa wa Ligi yetu ni ushindani uliopo katika nchi wanazokwenda. Kuna ushindani wa kupata nafasi kikosini, lakini pia kuna ushindani mkubwa baina ya mechi na mechi. Ni tofauti na hapa.

Hapa mchezaji akishakuwa staa tayari ameshakuwa staa. Unajua nani alikuwa anamuweka benchi Chama pale Morocco? Unajua uwezo wake? unajua Chama ilimpasa afanye nini kuweza kuipora nafasi yake? ni maswali ambayo wachezaji wetu hawataki kuyajibu na badala yake wanakimbilia kurudi.

Tanzania ukiwa staa ushakuwa staa. Hakuna maadili. Mchezaji anafanya mazoezi chini ya kiwango lakini lazima apangwe. Mchezaji anakesha Baa lakini lazima apangwe. Hakuna mchezaji ambaye hapendi kuishi maisha ya uhuru huu. Ni vile tu nje ya nchi wenzetu wanalazimika kuishi katika maadili haya. Tanzania mchezaji anaweza asiishi katika maadili haya na akaabudiwa.

Bahati nzuri kwa mastaa wetu ni kwamba wakati mwingine wanalazimika kufanya kazi ndogo tu uwanjani kuendelea kutamba na kuabudiwa. Nje ya nchi unalazimika kuishi katika mateso makubwa ili uabudiwe.

Kwa mfano, mechi ijayo Chama anaweza kuwa na mechi mbovu lakini akipiga kanzu mbili tu uwanjani itatosha kwa mashabiki wa kawaida kuamini kwamba Chama amefanya kazi kubwa uwanjani. Kifupi ni kwamba Tanzania kuna maisha rahisi ndani na nje ya uwanja.

Haishangazi pia kuona kuna wachezaji wengi wa kigeni ambao waliamua kuendelea kuishi Tanzania baada ya kustaafu soka. Wanajua kwamba Watanzania ni watu waungwana na wenye msaada mkubwa katika maisha yao.

Sababu nyingine ambayo inawafanya mastaa wengi kurudi mapema ni ukosefu wa ushindani pindi wanaporudi nyumbani. Viongozi huwa wanashindwa kutafuta wabadala wao haraka iwezekanavyo na mara zote mawazo yao ubakia kwa wachezaji husika.

Ukosefu wa kuskauti wachezaji vizuri umepeleka haya. Kwa mfano, tangu aondoke Simba haikupata mbadala wa Chama. Mawazo yao yote yalikuwa kwa Chama. Sio Simba tu, hata wapinzani wao Yanga mawazo yao yote yalikuwa kwa Chama.

Leo Fiston Mayele akiondoka utasikia anarudi tena kucheza Yanga au Simba au Azam. kufungua milango na kuziba pengo la mchezaji ni jambo gumu. Mchezaji akiondoka viongozi na mashabiki wanaendelea kubakia na jina la mchezaji huyo huyo kama mbadala wa nafasi yake.

Haishangazi kuona kuna wachezaji wengi wa kigeni ambao wamecheza Simba, Yanga na Azam kwa nyakati tofauti. Ni kama vile Obrey Chirwa. Aliondoka Yanga kwenda nje. Azam ikamfuata baada ya muda mfupi. Azam haikuona mchezaji mwingine wa kigeni kando ya Chirwa?

Mchezaji wa kigeni kama akicheza poa tu anajua kwamba nafasi yake ipo na itaendelea kuwepo. Ni kama ambavyo tunamsubiri Jose Luis Miquissone. Sio kwamba Msumbiji hawajaibuka mastaa wengine, hapana. Akili yetu ipo kwa Miquisonne kurudi nchini kuliko kusaka staa mwingine wa kariba yake.

Kuna sababu lukuki za mastaa hawa kurudi nchini na kila unapokumbuka idadi yao basi ndipo unapoendelea kuwaheshimu wachezaji kama Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Simon Msuva. Hawakutazama nyuma.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz