Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Kutoka Bocande mpaka Mane, Tanzania ijipange

Mane Pic Kutoka Bocande mpaka Mane, Tanzania ijipange

Wed, 9 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Niliwahi kwenda Barcelona mara kadhaa. Nilikutana na watu warefu, weusi, wakiwa kando za fukwe nzuri za Barcelona. Ni Wamachinga. Wanauza viatu kwa machale. Kwa sababu hawalipi kodi basi mara nyingi wanakuwa katika purukushani na Polisi.

Wanauza viatu, shanga, nguo na vitu kadhaa vinavyobebeka mkononi. Wanauza kwa Euro bei rahisi. Mara zote wanahamahama kutegemea tu ni wapi polisi wameweka kambi. Nilimuuliza rafiki yake mwenyeji hawa watu walikuwa wanatoka wapi. “Wengi wanatoka Senegal wengine wanatoka Mali”. Naam, inaonekana ni maisha yao. Wamezaliwa Ulaya kwa miaka mingi lakini pia wanaonekana wameizoea Ulaya. Umbali wa kutoka Dakar mpaka Ulaya ni kilomita 4,206. Wameachanishwa na bahari. Hapo hapo kumbuka kwamba umbali kutoka Mtwara hadi Kigoma zinakaribia kilomita 2000.

Juzi Senegal wamechukua ubingwa wa Afrika nikakumbuka mambo mengi. Nikawakumbuka wale Wamachinga wa Senegal waliopo Barcelona ambao pia niliwahi kuwakuta Milan. Nikakumbuka jinsi ambavyo wameizoea Ulaya. Nikakumbuka kwamba Senegal ni taifa la watu milioni 17 tu wakati Tanzania ina watu milioni 60. Kwanini Taifa la Senegal linatoa vizazi vya wachezaji wazuri? Nadhani inachangiwa pia na Jiografia yao. Kabla hatujajadili namna gani tunaweza kuwa Senegal kuna vitu inabidi tujikumbushe na kuumeza ukweli mchungu kama ulivyo.

Jiografia haitupi nafasi ya kuwa Senegal. Tunaweza hata kutambika lakini sidhani kama tunaweza kuwa Senegal. Wana watu wachache lakini wametapakaa Ulaya. Sisi tuna watu wengi lakini ambao hawajatapakaa Ulaya. Jiografia. Achilia mbali Jiografia lakini pia wenzetu walitawaliwa na Wafaransa. Wafaransa waliwapenda watu wao kupitia ile sera ambao iliwafanya watawaliwe wajione wao kama ni Wafaransa. Assimilation policy. Ni kama ambavyo Wacongo na watu wengine waliotawaliwa na Wafaransa wajione kuwa Wafaransa zaidi.

Najaribu kuwakumbuka mastaa wa Senegal. Tuanzie kwa Jules Bocande. Nenda google kamtazame vizuri Bocande. Niliwahi kumfuatilia nikiwa kijana mdogo., mwamba huyu ametamba na PSG, Metz, Nice, Lens na kwingineko. Kati ya mwaka 1984 mpaka mwaka 2002, Bocande alifunga mabao zaidi ya 100 katika Ligi Kuu ya Ufaransa. Kuna Mtanzania wa miaka hiyo amewahi kufanya hivyo? Bocande kwa sasa ni marehemu na alifia huko huko Ufaransa.

Ukiachana na Bocande jaribu kuangalia mastaa wengine. Watazame mastaa wenye asili tu ya Senegal ambao walicheza kwingine. Watazame Patrick Vieira na Patrice Evra ambao walizaliwa Senegal kabla ya kuvuka bahari na kwenda Ulaya. Nakukumbusha kwamba walikuwa Wasenegal asilia kama wale Wamachinga wa Barcelona. Na baada ya hapo kumbuka vizazi vyao vya kuanzia akina Khalilou Fadiga, El Hadji Diouf, Henry Camara, Tony Silva, Aliou Cisse na wengineo. Wote hawa wamezurura Ulaya wakiwa vijana wadogo. Yaani ni kama vile wamekwenda Ulaya katika umri wa Kelvin John.

Hawa ndio waliipeleka Senegal kombe la dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2002. Na walipoipeleka walikwenda moja kwa moja katika robo fainali. Nadhani wakati huo idadi ya watu wao ilikuwa watu milioni 10. Sisi inawezekana tulikuwa watu milioni 40. Baada ya hapo kikaja kizazi cha kina Demba Ba, Demba Cisse, Mamadou Niang na wengineo ambao hawakufanya vizuri sana. Na sasa wana kizazi kinachoongozwa na Sadio Mane. Wote wanacheza Ulaya halafu ni katika klabu kubwa. Nadhani katika timu zote ambazo zimeshiriki Afcon mwaka huu, Senegal ndio taifa ambalo lilikuwa na wachezaji wengi wanaocheza katika Ligi Kubwa tatu za Ulaya. Matumaini ya Tanzania kuwa kama Senegal ni finyu. Pengine Jiografia inatubana lakini hata watu wake pia hawana kitu ya mafanikio. Kwa mfano, mataifa yenye idadi kubwa ya watu huku mchezo wa soka ukiwa ni namba moja inakuwa rahisi kwa watu wake kuondoka na kusaka mafanikio nje ya nchi kwa sababu mgao wa keki ya taifa unakuwa adimu.

Haishangazi kuona nchi kama Nigeria na Brazil zikiwa na wachezaji wengi Ulaya hata kama Jiografia inaonyesha hawapo karibu na Ulaya. Kisa? Raia wake wengi wanatoka kwenda kusaka mafanikio nje. Na kwa sababu soka ni mchezo namba moja katika mataifa hayo, inakuwa rahisi kuwapata vijana wenye kiu ambao wanakwenda nje kusaka maisha. Baadaye inakuwa faida kwa taifa.

Tanzania haipo hivyo. Tuna watu milioni 60 wakiwemo vijana wengi wenye vipaji vikubwa vya soka lakini hawana kiu. Mpaka leo sioni kiini ni nini. Labda ni sera zetu za ujamaa ambazo zimesababisha Watanzania wengi kuwa na uhakika wa kula na kunywa hata kama hawana pesa.

Matokeo yake taifa lenye watu milioni 60 limemtwisha kijana mmoja tui kutoka Mbagala anayeitwa Mbwana Samatta ndiye awe tegemeo la taifa. Na kwa sasa tumeanza safari nyingine ndefu ya kuanza kumtegemea kinda Kelvin John ambaye nyota yake imeanza kung’ara Genk. Hili ni tatizo la kimsingi.

Unapofikiria mafanikio ya Senegal huku wakiwa wametwaa Afcon kwa mara ya kwanza unapata ganzi pale ambapo unafahamu kwamba tuna safari ndefu isiyoonekana kuwafikia walipo. Na wanachofanya wao ni kitu kile kile ambacho kinafanywa na mataifa ya Mali, Burkina Faso, Guinea na wengineo.

Bahati mbaya pia tatizo hili la Kijiografia inawezekana sio la Tanzania pekee ingawa Tanzania ipo chini zaidi. huu ukanda wetu wenye Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda pia unakabiliwa na matatizo haya haya ya Watanzania.

Rafiki zetu Burundi na Rwanda wametawaliwa na Wafaransa lakini nadhani Jiografia imewatenga. Waganda na Wakenya wana vipaji maridhawa na watu kama akina Victor Wanyama wameonyesha kwamba wanaweza kwenda mbali zaidi lakini nadhani kuna ukosefu wa kiu na mipango.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz