Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Kelele za "Fair competition" zilivyokufa kifo cha mende

Karia, TFF President Rais wa TFF Wallace Karia

Wed, 22 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kampuni hii imeweka mezani Sh2.1 bilioni. Pesa za Kitanzania. Imeingia katika Ligi kama wadhamini wenza kando ya NBC. Kuna mambo mawili yalijitokeza. Awali Yanga waligomea kuvaa logo nyekundu ya NBC. Halafu Simba wamegomea kuvaa logo kabisa ya NBC.

Sitaki kuzama ndani kuhusu nani ana haki au nani hana haki. Nataka tu kuwakumbusha ni namna gani ambavyo klabu zetu zina njaa. Kiburi cha Yanga kutovaa logo nyekundu ya NBC kinatokana na shibe yao. Inatokana na ukubwa wao pia.

Kiburi cha Simba kutotaka kuvaa logo ya GSM kina mambo mengi nyuma yake. Tulichukue hili la kwanza la kwamba Simba haikushirikishwa. Wenyewe wanasema hivyo lakini majuzi nimewasikia watu wa Bodi ya Ligi wakisema Simba walishiriki.

Sitaki kujua sana kuhusu ukweli kitendo cha Simba kugomea kuvaa logo ya GSM kimetokana na ukweli kwamba GSM ambao ni wadhamini wa Ligi, pia ni wadhamini wa Yanga. Kuna uwezekano GSM ikawa na kauli kubwa kuhusu upangwaji wa matokeo kwa sababu inamiliki Yanga na ni wadhamini wa klabu nyingine? Sijui sana kuhusu hilo.

Hata hivyo wanaojua na kuchambua wanadai kwamba kutokana na hali hiyo hakutakuwa na ushindani halali (fair competition). Wanaweza kuwa wamefafanu zaidi lakini mimi nadhani ukosefu mkubwa wa fair competition upo baina ya klabu zilizoshiba dhidi ya zile ambazo hazijashiba.

Hili ni tatizo la msingi kuliko GSM kudhamini Yanga na klabu nyingine za Ligi Kuu. Wachambuzi na watangazaji wanajua ni kiasi gani klabu zetu zinakabiliwa na njaa na haziishi katika hadhi ya Ligi Kuu? Kabla hatujaangalia ukweli (facts) ambao wachambuzi na waandishi wanajaribu kuutazama nadhani inabidi pia wapige kambi katika klabu zetu na kuangalia njaa zinazozikabili klabu zetu.

Achana na Azam ambao wanamilikiwa na familia ya kitajiri. Wengine wana njaa kali. Azam wana biashara na Yanga kupitia Azam TV. Wangeweza kukataa. Lakini wengine wanazihitaji pesa za GSM kuliko kitu kingine chochote.

Tatizo hapa tunaongelea suala la Simba na GSM tu. Au Simba na Bodi ya Ligi. Tumewahi kuangalia maisha ya klabu nyingine? Hawa ndio ambao nilijua kwamba wataikwamisha Simba kama hawa wangekuwa na uwezo kama wa Simba basi tungeweza kujadili facts.

Ukichambua mpira wa Ulaya maisha yanakuwa rahisi kufuata kanuni na sheria. Kila klabu itapanda ndege katika safari ndefu na fupi, kila klabu ina viwanja vya kisasa, kila klabu inalipwa wachezaji pesa zao kwa tarahe zilizopangwa, kila klabu ina viwanja vya kisasa vya mazoezi kwa timu za wakubwa, vijana na wanawake. Kila klabu ina gym, sauna, mabwawa ya kuogelea na kila kitu.

Ukiwa katika hatua hiyo utajaribu kuangalia ukweliu kuliko uhalisia. Kwa klabu nyingine zilizobaki, kitu cha kwanza kuangalia ni uhalisia. Kwamba wazipinge pesa za GSM kwa utajiri gani ambao wanao? Kwamba wakatazame vifungu vya fair competition, ni kwa maisha gani ambayo wanaishi.

Kufikia hapo klabu 13 za Ligi kuu zitaangalia zaidi pesa yoyote inayokuja bila ya kujali anayeileta. Sijaona timu nyingine ya kukataa. Klabu hizi zimebeba mizigo mizito katika kulipa wachezaji mishahara, kusafirisha timu, kulipia gharama za hoteli.

Kuna timu ambazo hazijiwezi. Kuna timu moja imeshuka Ligi Kuu ilikuja kucheza na Yanga na wachezaji wake walilazimika kutandikiwa magodoro na kulala chini. Siku moja kabla ya mechi. Hii ni fair competition kuliko hiyo nyingine inayosemwa kuhusu GSM kudhamini Yanga na timu nyingine katika Ligi?

Misimu miwili iliyopita, Coastal Union walifika Dar es salam saa nane mchana siku ya mechi kuja kuikabili Simba iliyokuwa imetulia hotelini Mbezi Beach. Hiyo ni fair competiton tunayoitaka? Kulikuwa hakuna namna Simba wangepata washirika katika sakata hili. Timu zina njaa.

Hata sasa hivi Mohamed Dewji akipeleka pesa zake pale TFF kwa ajili ya kudhamini Ligi nadhani Yanga wanaweza kugoma lakini hawataweza kupata washirika wengine katika safari yao ya mgomo. Suala sio ukweli wa mambo bali ni uhalisia wa mambo.

Klabu zetu zinahitaji pesa za Azam TV, NBC na sasa GSM. Walau tunaweza kuwa na l;igi yenye hadhi kidogo tofauti na sasa ambapo tunajidanganya Ligi yetu ina hadhi kwa sababu ya uimara wa Simba, Yanga na Azam.

Huku kwingine wengine wapo hoi. Kuna klabu ambazo zinashindwa kumudu mambo ya msingi na wala sio anasa. Klabu inayoshindwa kula milo mitatu kwa siku inakuwa imeshindwa kufanya kitu cha msingi cha mwanadamu na moja kwa moja inajiondoa katika ushindani.

Kama kila klabu itaweza walau kukusanya shilingi milioni 60 kwa mwezi kutoka katika mikataba mbalimbali ya TFF na ya kwao binafsi walau klabu zetu zitaweza kujikomboa na kuishi katika hadhi ya Ligi Kuu. Acha wakubwa wengine waishi kwa anasa lakini tuna rundo la klabu ambalo linahitaji kwanza kutatua mambo ya msingi.

Sawa mchezaji wa Coastal Union au Biashara Shinyanga anaweza asiendeshe Mercedes Benz kama zinazoendeshwa na akina Khalid Aucho, lakini anapaswa kutimiziwa mambo ya msingi ili awe kucheza soka katika ushindani.

Timu zetu pia inabidi zionekane zina hadhi haswa. Ukiambiwa kwamba hoteli hii ndio ambayo wamefikia wachezaji wa timu ya Ligi Kuu inayoitwa Mbeya Kwanza unapaswa kutoa heshima yako. Sasa hivi wachezaji wa klabu nyingine wanafikia ‘guest house’ za vichochoroni tu.

Kelele za fair competition inabidi ziende katika haki ya kupunguza pengo kubwa lililopo kati ya wasio nacho na wale walionacho na sio kuhimizana kukataa pesa wakati klabu zenyewe zipo hoehae. Siamini kama klabu 13 zinaweza kumuandalia Yanga mazingira ya ubingwa kwa sababu tu Yanga wanadhaminiwa na GSM na wao wanadhaminiwa na GSM.

Umaskini wa klabu zetu ndio ambao umeua mjadala wa fair competition. Ikiwezekana tubadilishe baadhi ya kanuni ili tuendane sawa na hali halisi.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz