Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Karibu tena Heritier Makambo, tumekwishazoea

Makambo Pic Heritier Makambo (kulia) akiwa na Injinia Hersi

Wed, 4 Aug 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Aliifungia Yanga mabao 17 katika msimu ambao klabu ya Horoya ya Guinea iliamua kuisaka saini yake na kumchukua. Heritier Makambo. Anaweza kuwa mshambuliaji wa mwisho kuifungia Yanga mabao mengi. Tangu hapo hawajawahi kupata mshambuliaji kama yeye.

Kabla yake alikuwepo Amiss Tambwe kisha akaja yeye. Walikuwa washambuliaji wawili wa mwisho wenye hadhi ya kuitwa ‘washambuliaji wa Yanga’ kabla ya Yanga kuanza kukosea tena katika usajili wa washambuliaji.

Walikuja washambuliaji ambao walikuwa wanapishana kwa unafuu tu, lakini ukweli ni kwamba hawakuwa katika hadhi ya Yanga. Watu wa Yanga wenyewe wanalifahamu hili na ndio maana wamefanya haraka kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.

Juzi, Makambo amerudi tena katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Yanga wamempa mkataba wa miaka miwili kwa mara nyingine. Anakumbukwa kwa kuichezea Yanga yenye tabu kabla ya kuondoka kwake.

Kurudi kwake kunajadilika katika kona mbalimbali. Kona ya kwanza ni namna ambavyo ni rahisi kurudi katika timu hizi kama uliwahi kufanya makubwa. Inakuwa rahisi. Mashabiki wa Yanga ndio haswa ambao wameshinikiza Makambo arudi.

Sina uhakika kama wamechunguza kiwango chake wakati yupo Horoya. Naambiwa kwamba msimu wake wa pili ulikuwa mgumu kwa sababu hakupata sana nafasi. Je aliyekuwa anacheza nafasi yake alikuwa mtu hatari kuliko yeye au ni kwamba kiwango cha Makambo kimeshuka?

Hatujui. Tunachojua ni kwamba Yanga wamemchukua Makambo kwa ajili ya kuanzia pale alipoishia. Wanaamini kwamba kwa Yanga hii ambayo imeimarika zaidi kuliko ile ya wakati ule, basi Makambo atafunga mabao mengi.

Hizi ni hisia tu lakini Yanga walipaswa kujiridhisha kwanza kuhusu uwezo wa sasa wa Makambo. Ni yuleyule? Wana uhakika gani? Wakishamaliza kujiridhisha kama ni yuleyule wajiridhishe tena na afya yake. Hana majeraha yoyote yaliyokwamisha kiwango chake huko alipo?

Nimeshtuka kuona mchezaji kama Fiston Mayele akitambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga juzi bila ya kuonyeshwa picha wala video ambazo zingemuonyesha akipimwa afya. Yanga walichoangalia ni rekodi zake tu nzuri za mabao kule DR Congo.

Hadithi ya Makambo na Yanga imenikumbusha hadithi ya Emmanuel Okwi na Simba. Hata sasa Simba inahusishwa tena na Okwi. Yaani hizi timu ukizifanyia makubwa basi unaweza kuwa mfalme wa kudumu bila ya wao kujihangaisha kwingine.

Kwa mfano, Yanga hawakutaka sana kujihangaisha kwingine lilipofika suala la Makambo. Nadhani hawana mfumo mzuri wa kusaka wachezaji (scouting system). Wana uhakika gani kwamba wasingepata mchezaji mwingine hatari zaidi ya Makambo alivyokuwa kabla hajaondoka? Hawakutaka kujisumbua sana.

Hata hivyo, inawezekana Makambo akatuziba mdomo. Hii inatokana na ukweli kwamba Makambo aliyeondoka alikuwa hatari kuliko warithi wake wote waliokuja, David Molinga na Michael Sarpong. Kama akiwa Makambo yule basi ni wazi kwamba afadhali yeye kuliko hao. Tena afadhali zaidi.

Hapohapo kama aking’ara itatupa wakati mgumu wa kuelewa kiwango cha ushindani kati ya Yanga na Horoya. Labda kiwango cha ushindani cha Horoya kipo juu kuliko Yanga. Au labda Ligi Kuu ya Guinea ina ushindani kuliko yetu.

Lakini wapo wachezaji walioonekana wamefeli sehemu moja halafu wakaibuka vinara katika upande mwingine na kurudisha heshima. Hili ndilo pekee ambalo nalitegemea kutoka kwa Makambo kwa sasa. Vinginevyo atawapa kauli wale ambao wamebeza uhamisho wake.

Vyovyote ilivyo ni kamari ambayo Yanga wanaweza kuichukua kwa sababu pia wamemsajili Mayele na wanataka kumchukua mshambuliaji mwingine huku pia Yacouba Sogne akiwa amemaliza msimu katika kiwango kizuri tofauti na alivyokuja.

Nasikia wanaweza kumchukua Jean Makusu. Kama wakiwa na Makambo, Mayele, Makusu na Yacouba siamini kama wote wanaweza kufeli tena kwa pamoja. Kama angekuwa amekuja Makambo pekee au Mayele pekee ingekuwa bahati nasibu.

Kwa sasa ni suala la kusubiri na kuona kama Makambo anaweza kuwa yuleyule. Vyovyote ilivyo nahisi Yanga wanaweza kuimarika zaidi tofauti na walivyokuwa. Achilia mbali suala la usajili ni kwamba Yanga wana kocha mzuri, Mohamed Nabi.

Amewaimarisha katika uchezaji wao. Namna wanavyojihami, namna wanavyopitisha mashambulizi kwenda mbele na namna pia wanavyoshambulia kwa wingi. Nabi ni kocha hasa. Labda kina Makambo wanaweza kufunga zaidi kama wakiwa makini kwa sababu msimu huu moja kati ya matatizo ya Yanga ilikuwa ni umaliziaji zaidi.

Katika eneo la mbele ni aibu kuona mfungaji bora wa Yanga alikuwa na mabao nane tu katika Ligi Kuu huku ‘utatu mtakatifu’ wa Simba wenye Meddie Kagere, John Bocco na Chris Mugalu kila mmoja akiwa na mabao zaidi ya 13.

Nikimalizia kwa utani tu. Nawakumbusha Yanga kwamba ghafla timu yao imekuwa ya Wakongo. Kumbuka kwamba wameshainasa saini ya mlinzi wa kulia wa kupanda na kushuka wa AS Vita na timu ya taifa ya DR Congo, Djuma Shabani.

Ina maana kutakuwa na Wakongo wangapi pale rafiki zangu? Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Djuma Shabani, Fiston Mayele na Herritier Makambo. Nasikia wanasaka kiungo mchezeshaji kutoka katika taifa hilo. Sijui inatokea kwa bahati mbaya au kuna kitu wamekiona kutoka kwa wachezaji wa DR Congo? Sina uhakika.

Inakumbusha jinsi ambavyo wakati fulani Barcelona ilikuwa inataliwa na wachezaji kutoka Uholanzi. Pale Catalunya wachezaji wa Uholanzi ni nyumbani kwao. Wamepita zaidi ya 30 na mpaka sasa kina Memphis Depay, Frenkie de Jong wameendelea kutawala katika viunga vya Catalunya.

Columnist: Mwanaspoti