Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Kama imemtokea Msuva vipi kwa vijana wengine?

Msuva Ml.jpeg Simon Msuva

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hii michuano ya juzi ya vijana walikuwepo kina Lionel Messi, N’Golo Kante, Gabriel Jesus, Cristiano Ronaldo na wengineo. Mtibwa waliibuka mabingwa.

Nilikuwa nafuatilia kwa karibu. Vipaji maridhawa. Vijana wakicheza kwa uhuru huwa wanaonyesha soka maridadi. Tatizo linakuja pale wakienda timu za Ligi Kuu. Sio kila mmoja anayeweza kuhimili presha. Wanajikuta wanacheza kwa hofu. Vipaji vinapotea. Lakini kwa sasa ukitaka kusikia raha basi tazama wakiwa vijana. Kila mmoja anataka kuonyesha ufundi.

Ulikuwa ukitazama michuano hii unaona vipaji maridhawa kweli kweli. Unajikuta unatabasamu. Yamefungwa mabao ya video. Zimepigwa penalti za video. Ni kama vile unawaangalia hao mastaa niliowataja hapo juu.

Unajua nini kinahitajika? Kwa kule Afrika Magharibi ikifikia hatua hii unakuta kila mtu ana wakala wake. Unakuta kila mtu yupo katika menejimenti fulani. Hauwezi kukuta kijana ana kipaji maridadi halafu hasimamiwi na mtu au watu.

Achilia mbali malezi kutoka kwa klabu lakini kijana anahitajika kuwa na malezi binafsi kutoka kwa mtu binafsi ambaye anaweza kuwa wakala wake, meneja wake au taasisi fulani ambayo itajulikana kama menejimenti yake.

Huku kwetu hawa vijana tunawapoteza. Hakuna ambaye atawapeleka mbali zaidi. Wenyewe wanakisia tu kwamba wanaweza kwenda timu za Ligi Kuu halafu wakabahatika kutakiwa na Simba, Yanga au Azam. Hawaoni mbali zaidi ya hapo.

Lakini ebu subiri kwanza. Kuna kaka zao ambao waliona mbali zaidi. Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Simon Msuva na wengineo waliona mbali zaidi. Lakini hapo hapo subiri kwanza. Majuzi nikasikia taarifa ambayo iliniangusha sana na kunifikirisha. Ilimhusu Msuva. Mmoja kati ya watu waliojitokeza kumsimamia katika skendo yake na klabu yake ya zamani ya Wydad Casablanca, Jasmine alikuwa kando ya Msuva wiki iliyopita katika mkutano wa waandishi wa habari akielezea madhila ambayo Msuva alipitia mpaka akashindwa kucheza soka katika miezi ya karibuni.

Msuva aliifungulia kesi Wydad kwa kumsainisha nyaraka ambazo zilisababisha asilipwe baadhi ya haki zake. Dada Jasmine ambaye wakati huo hakuwa na Msuva anadai kwamba Wydad walikuwa wamempoteza Msuva kwa kumlazimisha asaini mkataba au nyaraka ambazo alikuwa hazielewi. Ziliandikwa kwa lugha ya Kifaransa.

Hapa kidogo unarudi nyuma na kujiuliza. Kwanini Msuva alisaini? Na hapo hapo kidogo unarudi nyuma na kujiuliza kama Msuva alifanya kosa lile, vipi kwa makinda waliokuwa wanashiriki michuano ya vijana iliyomalizika majuzi pale Chamazi?

Kama mchezaji mkubwa ambaye amecheza nje ya Tanzania kwa muda mrefu kama Msuva anafanya kosa lile vipi kwa vijana hawa ambao wanahitaji ushauri mkubwa kutoka kwa Msuva? Msuva amecheza kwa muda mrefu katika klabu ya Difaa el Jadida, lakini bado aliingizwa chaka na Wydad. Vipi kwa kijana wa kawaida wa Tanzania ambaye hana uzoefu na soka la nje?

Hapa ndipo tunaporudi katika suala la menejimenti. Suala la watu ambao wanakuacha wewe ucheze soka uwanjani huku wao wakiwa bize kushughulikia masuala yako. Suala la watu ambao watausoma mkataba wako kwa usahihi na kutafsiri kwa umakini kila kilichoandikwa huku wewe ukiwa bize na kazi yako uwanjani.

Ni wazi kwamba wachezaji wetu wanahitaji msaada mkubwa. Kuanzia hawa tunaowapika sasa hivi hadi hawa ambao ni wakubwa na majina makubwa. Kuna mahali, kuna kitu hakipo sawa. Inawezekana ndio maana wachezaji wetu hawasongi mbele.

Naambiwa kwamba wachezaji wetu wenyewe huwa wanaona tatizo kuwa na meneja, wakala au menejimenti. Wanaamini kwamba hawa ni watu ambao wanachukua pesa nyingi bila ya kuzifanyia kazi. Kosa lao ni kwamba hawajui kwamba watu hawa wana msaada mkubwa kwao.

Watu hawa ndio wana uwezo mkubwa wa kupenya na kumtafutia mchezaji timu. Lakini pia ndio wana uelewa na masuala ya kimkataba. Kuna wachezaji wengi wakubwa nchini ambao nafahamu kwamba wanapata msaada mkubwa kutoka kwa watu hawa. Kama wangekuwa wanajisimamia wenyewe hali ingekuwa mbaya.

Viongozi wetu hupenda kuwalalia wachezaji na kisha kuwageuza mashabiki wa hizi timu. Nadhani wachezaji wa kigeni ndio ambao wamekuja kuwapa maarifa wachezaji wetu wazawa kiasi kwamba kwa sasa wameamka. Vinginevyo kabla ya hapo hali ilikuwa mbaya zaidi.

Wachezaji wetu wengi wametokea katika umaskini. Wachezaji wetu wengi pia kama ilivyo kwa mastaa wengi wa Ulaya huwa hawana muda wa kwenda shule. Kipindi ambacho wanatakiwa kuwa shule ndicho hicho hicho ambacho wanahitajika kuwa uwanjani.

Kuanzia hapo ndipo wanakosa elimu ya msingi ya ufahamu wa mambo mengi. Hii sio dhambi kwa sababu hata kina Lionel Messi hawakusoma. Kinachowasaidia ni kuzungukwa na watu mbalimbali wenye elimu ambao wanawasaidia katika mambo yao. Bahati nzuri huwa wanawasaidia kwa mkataba maalumu.

Wale vijana ambao walikuwa wanacheza michuano ya vijana wanahitaji watu wa namna hii. Walau kwa sasa kuna mwamko wa vijana kuhitaji kusimamiwa. Unahitaji mtu ambaye ni mjanja kukusaidia kukutafutia timu, kuingia mkataba, kusimamia maslahi yako na mambo mengineyo.

Unaweza kuwa kinda mahiri wa Mtibwa Sugar lakini ukaomba kusimamiwa na Taasisi ya Cambiasso. Kucheza mpira bila ya kuwa na watu imara nyuma yako ni mwanzo wa kupoteza kipaji. Hata hivyo, sio kila taasisi au kila meneja anaweza kukupeleka kuzuri. Wakati fulani kina Mike Tyson na Toni Braxtoni waliwahi kufilisika kwa kukosa usimamizi madhubuti. Hata hivyo ni muhimu kuwa na wasimamizi.

Columnist: Mwanaspoti