Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Inonga, mtoaji na mpokeaji wa rafu za kisela zisizofaa

Inonga Rafu Inonga, mtoaji na mpokeaji wa rafu za kisela zisizofaa

Wed, 4 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Rafu za kisela zimeendelea mapema wikiendi hii baada ya mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Samson Mbangula kumchezea rafu mbaya beki wa Simba, Enock Inonga katika pambano la Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ijumaa jioni.

Mbangula angeweza kumvunja mguu Inonga ambaye sijui hali yake inaendeleaje. Alimrukia kwa miguu miwili akiifuata miguu ya staa huyo wa DR Congo. Bahati nzuri hakumpata vizuri. Kama angempata kisawasawa nadhani angemvunja mguu.

Wachezaji wetu wanacheza rafu mbaya halafu unajiuliza sababu za msingi. Hauzioni. Hapa ndipo ambapo wananishangaza. Kule Ligi Kuu ya England huwa nachunguza sababu za rafu mbaya halafu huwa naziona. Mara nyingi inakuwa mchezaji amechanganyikiwa na hali ya mchezo. Labda timu yake imefungwa au imetawaliwa zaidi.

Wakati mwingine rafu inakuwa mbaya baada ya mchezaji kukosea ‘timing’ ya kuucheza mpira. Haiwi makusudi lakini rafu inaonekana mbaya kwa namna ambavyo mchezaji ameukosa mpira halafu akauvaa mwili wa mtu.

Hapa ni tofauti. Sasa hivi katika ligi yetu zimerudi rafu za kisela ambazo wakati mwingine inakupa mawazo kwamba huenda tunahitaji kuwapima wachezaji wetu akili kila msimu unapoanza. Tuanze na rafu ya Mbagula.

Simba ilikuwa inaongoza kwa bao moja na mechi ilionekana kwenda sawa kwa pande zote mbili. Baada ya Mbangula kutoka Prisons ikapata bao la kusawazisha kuthibitisha kwamba haikuwa mechi ya upande mmoja kwa Prisons. Kwanini alicheza rafu ile? Ni yeye tu ndiye anayejua. Vipi angekuwepo uwanjani wakati Simba ikiongoza kwa mabao saba? Si angeua mtu kwa hasira.

Watu huwa wanadai rafu hizi zinachezwa kwa sababu timu ndogo zinakuwa zimepewa ahadi. Sio kweli. Huyu huyu ambaye alikuwa mhanga wa mechi ya Ijumaa jioni naye amewahi kucheza rafu mbaya msimu huu.

Inonga aliwahi kumchezea rafu mbaya Salum Abuubakary ‘Sure Boy’ katika pambano la Simba dhidi ya Yanga. Hakukuwa na haja yoyote. Mechi ilikuwa nzuri tu kwa pande zote. Alikuwa ameuhamisha mpira vizuri tu lakini akaamua mguu wake utue kwa Sure Boy. Inashangaza alipewa kadi ya njano.

Pambano dhidi ya Ihefu, beki mwingine wa Simba, Joash Onyango alicheza rafu mbaya kwa Papy Shishimbi. Ilinishangaza mwamuzi hakumpa kadi. Lakini ilinishangaza pia Simba ilikuwa imemiliki mpira wake kama kawaida na ilikuwa inaongoza mechi. Sijui kwanini Onyango alikuwa anataka kumvunja mguu.

Pambano la Azam dhidi ya Yanga kiungo wa Azam anayeitwa Sospeter Banyana alicheza rafu mbili mbaya. Moja dhidi ya Dickson Job. Aliishia kupewa kadi ya njano. Kipindi cha pili akacheza rafu nyingine ya kumkwatua mchezaji mwingine wa Yanga kutoka nyuma. Kama haikuwa kadi nyekundu ya moja kwa moja basi alistahili kupewa kadi ya pili ya njano. Hakupewa.

Baadaye kocha wake akamtoa nje kwa kuhofia kwamba huenda angepewa kadi nyingine ya pili. Akaishia kulalamika kama vile hajui alichokifanya.

Pambano jingine nilicheka kidogo. Kipa wa Singida Big Stars, Metacha Mnata aliudaka mpira vema kisha akampiga kiwiko Charles Ilamfya wa KMC aliyekuwa kando yake. Hakukuwa na sababu yoyote ya msingi kwa sababu Singida ilikuwa inaongoza mechi. Aliamua tu. Basi.

Baadaye akakimbilia katika mtandao wa Instagram kuomba radhi. Ilinikumbusha namna ambavyo kiungo wa Coastal Union, Albano Mtenje alimchezea rafu mbaya, Yannick Bangala wa Yanga katika pambano la fainali za Shirikisho la Azam pale Arusha. Hakukuwa na sababu yoyote msingi kwa sababu timu zote mbili zilikuwa zinacheza vizuri tu. Rafu yake ilikuwa ile ya kisela zaidi ambapo aliunyanyua mguu kwa hatua tatu kwa ajili ya kwenda kutua katika mguu wa Bangala.

Baadaye na yeye akakimbilia Instagram kuomba radhi huku akitangaza urafiki na Bangala. Ujinga ulioje? Lakini tusiondoke kwanza kwa Ilamfya. Na yeye katika pambano moja la Ligi Kuu hivi karibuni alimpiga kiwiko mchezaji mwenzake katika staili ile ile ambayo yeye alipigwa na Metacha.

Ilamfya aligoma kutoka uwanjani kama vile hakuwa amefanya kosa lolote.

Ikanikumbusha namna ambavyo Abdulaziz Makame alimchezea rafu mbaya Shomari Kapombe kwa kumrukia kwa miguu miwili. Alipopewa kadi nyekundu akagoma kutoka nje kwa dakika mbili.

Unajiuliza, wachezaji wetu wana akili timamu? Unajiuliza, wanaweza kuwa wachambuzi? Wanaweza kujua aina gani ya rafu inaweza kukupatia kadi nyekundu?

Djuma Shaaban naye katika pambano la msimu uliopita dhidi ya Polisi Tanzania pale Arusha alimpiga mtu kiwiko bila ya sababu ya msingi.

Yanga ilikuwa imetawala mechi vizuri tu. Mpira mmoja uliokuwa unaelekea nje akaamua kumpiga mtu kiwiko bila ya sababu za msingi. Kisa alikuwa ameghasiwa.

Kwa nini rafu hizi zinarudi kwa kasi? Ni kwa sababu wachezaji wengi wanasalimika pindi wakicheza rafu hizi na hasa ni wachezaji wa hizi timu hizi kubwa. Waamuzi wetu sio wakali katika rafu mbaya za makusudi. Wakiona mchezaji husika ana dalili za kuendelea na mchezo wanadhani rafu haikuwa kubwa. Wanatoa kadi ya njano.

Na hata malalamiko haya ya kina Makame na Ilamfya kukaa muda mrefu uwanjani yanatokana na ukweli kwamba hawajazoea kuona kadi nyekundu zikitolewa uwanjani. Wamezoea kucheza kisela halafu maisha yanaendelea kama kawaida.

Imefikia wakati sasa Bodi ya Ligi ikajitengenezea kanuni ambayo hata rafu isipoonwa na mwamuzi bado wanaweza kutoa maamuzi. Lakini pia hata kama mwamuzi ametoa kadi ya njano kwa kadi inayostahili kadi nyekundu bado wawe na uwezo wa kuitengeneza kadi nyekundu kupitia mezani. Vinginevyo rafu za kisela hazitaisha.

Columnist: Mwanaspoti