Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Inonga hatakuwa wa mwisho kufanya alichofanya

Inonga Baka Ttt Inonga hatakuwa wa mwisho kufanya alichofanya

Wed, 17 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Dada yangu Jonesia Rukyaa aliwahi kumtoa kwa kadi nyekundu mlinzi wa Simba, Abdi Banda katika pambano la Simba na Yanga miaka michache iliyopita. Ilikuwa ni kipindi cha kwanza cha pambano hilo. Kilichofuata kilichekesha kidogo.

Mashabiki wa Simba walikuwa wanalalamika kwa Jonesia kumpa kadi ya pili ya njano Abdi. Kwanini? Eti kwa sababu ilikuwa ni mechi ya watani wa jadi na alikuwa ameondoa ladha ya pambano. Kwamba pambano la Simba na Yanga hauwezi kutoa kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza.

Wakati mwingine kuna soka letu na kuna soka la wenzetu ambapo unaweza kumtoa staa katika dakika ya kwanza ya soka. Iwe Kombe la Dunia, iwe mechi ya Manchester City dhidi ya Manchester United. Iwe pambano la El Clasico. Iwe mechi yoyote ya soka. Sheria lazima zifuatwe.

Huku kwetu tunajaribu kutengeneza kanuni zetu kama hiyo hapo tulikuwa tunamwambia Jonesia. Matokeo yake mdogo wangu, Eli Sasi aliyechezesha pambano la Jumamosi usiku kati ya Simba na Yanga naye aliamua kuifuata kanuni hiyo.

Henock Inonga, mlinzi wa Simba alipaswa kupewa kadi nyekundu baada ya kucheza mchezo wa hatari dhidi ya Sure Boy. Ni mchezo huo wa hatari ambao ulizua vurugu kubwa katika pambano la Simba na Yanga. Sasi aliona kilichotokea.

Alimpa Sure Boy kadi ya njano kwa kujibu mapigo. Sawa. Alimpa Inonga kadi ya njano kwa rafu aliyofanya. Hapa kulikuwa na mambo mawili. Ni afadhali Sasi asingempa kadi nyekundu wala ya njano Inonga tungesema kwamba hakuona tukio zima.

Kama aliona, basi Inonga alistahili kupewa kadi nyekundu. Sasi sio kwamba hafahamu kuwa Inonga alistahili kadi nyekundu, hapana. Anafahamu. Tatizo ni kwamba alitumia sheria za mashabiki wetu. Kwamba hauwezi kumpa kadi ya mapema mchezaji wa Simba au Yanga katika pambano lao la watani.

Ilikuwa ni dakika za mwisho za kipindi cha kwanza. Kwa hiyo Sasi alijua kwamba Simba wangecheza pungufu kwa kipindi chote cha pili. Naamini Sasi angechukua uamuzi huu huu hata kama rafu ingechezwa na mchezaji wa Yanga.

Hii ni kwa sababu alikuwa na mechi nzuri kwa dakika zote isipokuwa lilipokuja tukio hili. Hakuonyesha upendeleo wowote kabla ya tukio hilo. Inonga alimuweka matatani Sasi na ikamlazimisha atumie sheria za mashabiki na sio sheria za soka.

Ni katika kutumia sheria hizi hizi za mashabiki, Sasi pia alikataa penalti ambayo Bernard Morrison alichezewa madhambi na kipa wa Simba, Beno Kakolanya. Sababu ilikuwa rahisi tu kwa mujibu wa sheria za mashabiki. Kwamba Yanga walikuwa wanaongoza mabao 2-1 na wasingelalamika sana kama wangeondoka na ushindi huo bila ya kujali kwamba walinyimwa penalti.

Na katika kutumia kanuni hiyo hiyo ya sheria za mashabiki kwa kuwaridhisha mashabiki wa Yanga kwa kumaliza mechi baada ya dakika nne za nyongeza licha ya Morrison kupoteza muda kijinga ndani ya dakika hizo.

Kwa mujibu wa kanuni za soka, endapo mpira utasimama muda mrefu katika dakika za nyongeza bado dakika hizo zitafidiwa. Ni tofauti na mashabiki wengi wa soka nchini wanavyodanganyana. Kwa mfano, mpira umeongezwa kwa dakika tatu halafu kuna mchezaji akaumia kwa dakika tatu basi mechi itamalizika na dakika 96 na sio dakika 93.

Hata hivyo Eli Sasi hili alilijua vyema. Alijua kwamba

angeongeza muda halafu Simba ikasawazisha basi Yanga wangekuwa wakali kuhusu penalti yao. Kwa sasa Yanga wala hawakumbuki sana penalti yao halali waliyonyimwa kwa sababu wameshinda. Wanaimba wimbo wa Fiston Mayele na Azizi Ki, basi.

Tukirudi kwa Inonga ukweli ni kwamba kuna wachezaji wengi wa Simba na Yanga huwa wanatumia sheria hii ya mashabiki kuendeleza ubabe. Kina Kelvin Yondani na Juma Nyosso mara nyingi walikuwa wakicheza ubabe na bado walisalimika.

Wakati mwingine sio tu katika pambano la Simba na Yanga, lakini hawa walipokuwa wakicheza dhidi ya timu nyingine. Ni nadra sana kwa mchezaji wa Simba na Yanga kupewa kadi nyekundu. Muulize John Bocco alivyokuwa anapigwa mateke kila mahala wakati akiwa Azam FC.

Mpaka sasa naamini kwamba Mukoko Tonombe asingepewa kadi nyekundu katika pambano la Simba na Yanga pale Kigoma kama angekuwa amecheza rafu mbaya. Alipewa kadi nyekundu kwa sababu tu tukio lilikuwa nje ya mpira.

Kama ingekuwa rafu ya kindava kama hii ya Inonga basi asingepewa kadi nyekundu. Hivi ndivyo ambavyo tumewalemaza wachezaji wa Simba na Yanga hapa nchini. Kinachonishangaza ni kwamba wachezaji hawa hawa huwa hawachezi hivi katika mechi za kimataifa.

Tumemtazama Inonga katika mechi nyingi za kimataifa alizocheza msimu uliopita akiwa na jezi ya Simba na hakuwahi kucheza mchezo wa hatari. Mechi zenyewe zilikuwa ngumu kama hii ya juzi, lakini alijua kwamba mwamuzi sio Mtanzania.

Hata kina Yondani walikuwa wanacheza kibabe katika mechi za ndani tu, lakini katika mechi za kimataifa walikuwa na adabu. Mara nyingi huwa wanawahofia waamuzi wa CAF kwa sababu wanajua kwamba hawajali mambo ya Simba na Yanga na watachezesha mechi kwa sheria za mpira zilivyo.

Na kwa sababu hii basi tegemea kwamba alichofanya Inonga hakitakuwa kitu cha mwisho kutoka kwa mchezaji wa Simba au Yanga pindi mwamuzi anapokuwa Mtanzania. Labda mwamuzi angetoka Morocco au Algeria angeweza kumuonyesha kadi nyekundu Inonga lakini sio kwa Sasa, Ahmed Aragija wala Ramadhan Kayoko.

Columnist: Mwanaspoti