Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Dilunga ameivusha Simba katika mdomo mwingine wa mauti

G3 Data Hassan Dilunga akifunga bao dhidi ya Red Arrows

Wed, 8 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Hassan Dilunga hakuwepo wakati babu yake, Maulid Dilunga pamoja na staa mwingine wa Tanzania, Omar Mahadhi walipochaguliwa katika kikosi cha kombaini cha Afrika mwaka 1974. Yaani Afrika nzima ilichagua kikosi chake halafu Watanzania wakawemo.

Juzi Hassan alikuwa katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa wa Zambia walau kuendelea kuliingiza jina la Dilunga katika ramani ya Afrika. Bao lake pekee lilitosha kuwatoa wapinzani wao wagumu Red Arrows - Wazambia ambao wiki moja iliyopita walichapwa mabao 3-0 katika uwanja uliojaa maji wa Mkapa pale Temeke.

Dilunga ndiye ambaye aliiokoa Simba. Alipenda mambo yatokee uwanjani. Ni mmoja kati ya wachezaji wa wazawa ambao wamepambana katika nyakati zote tangu Simba ikiwa bora zaidi kwa ajili ya kulinda nafasi zao uwanjani. Wengine huwa tunawaona zaidi katika akaunti zao za Instagram.

Kipindi cha kwanza Dilunga alikimbia vyema hadi ndani ya boksi na kupiga krosi nzuri kwa wenzake wakazubaa ikaoshwa. Alipenda mambo yatokee pengine kuliko wachezaji wengine wa Simba eneo la mbele. Bernard Morrison hakuwa yule wa wiki iliyopita.

Baadaye Simba ikafungwa mabao mawili. Bao la dakika za mwisho za kipindi cha kwanza. Na bao la dakika za mwanzo za kipindi cha pili. Kwanini walifungwa? Walilegeza nati za akili. Takwimu za soka duniani kote zinadai kwamba mabao mengi huwa yanafungwa kuanzia dakika ya 40 na pale timu zinapotoka mapumziko.

Timu zikitoka mapumzikoni wachezaji wanakuwa wamepoa. Haishangazi kuona makocha wa viungo huwa wanapanga koni na kuwafanyisha mazoezi wachezaji pindi wanapotoka katika vyumba vya kubadilishia nguo sekunde chache kabla ya kipindi cha pili kuanza.

Kwanini Simba waliruhusu mabao hayo? Achilia mbali kupoa kwa miili lakini ukweli ni kwamba Simba waliruhusu mashambulizi mengi langoni mwao. Hata katika hesabu za kawaida, ukikaribisha sana mashambulizi lazima kuna wakati utapoteza umakini. Hauwezi kushambuliwa mashambulizi 20 halafu walinzi au kipa wasikosee walau mara moja.

Kulikuwa na mambo mawili. Ama Simba wacheze kwa kujilinda katika kiwango ambacho kocha, Jose Mourinho amewahi kutufundisha katika soka, au wajaribu kuuchukua mpira na kwenda kucheza katika lango la Arrows.

Walianza kwa kujitahidi kufuata mbinu za Mourinho. Arrows walikuwa wanapiga mipira mirefu pembeni, hasa katika upande wa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’. Baada ya hapo wanapiga krosi. Henock Inonga na Sergi Wawa pamoja na kipa wao, Aishi Manula walikuwa wanafanya kazi nzuri.

Isingedumu kwa muda mrefu kama Simba wangeamua kupambana kujaribu kuuchukua mpira na kuliweka lango la Arrows shakani. Badala yake hawakufanya hivyo na mvua ilikuwa inaelekea kwao kwa muda mrefu. Tutake tusitake kuna mambo mawili yamepungua Simba.

Kwanza mkandamizo wao katika mechi (intensity) umepungua. Pili, makali yao katika eneo la mbele yamepungua tangu kuondoka kwa Luis Miquissone na Clatous Chama. Kama Morrison hana wakati mzuri mambo yanakuwa magumu zaidi.

Kama Simba wangeuchukua mchezo na kuupeleka katika lango la Arrows mara kwa mara si ajabu kasi ya mashambulizi ya Arrows ingepungua. Wakati mwingine njia sahihi zaidi ya kujihami ni kushambulia au kumiliki mpira kwa muda mwingi. Simba hawakufanya vyote.

Hii ilikuwa mechi ya wanarobo fainali wa msimu uliopita dhidi ya timu iliyoshika nafasi ya tatu katika Ligi ya Zambia msimu uliopita. Simba wanapaswa kuonyesha ukubwa katika timu kama hizi kama wanataka kutawala soka la Afrika. Wasichague uwanja. Wanawaweka mashabiki wao roho juu.

Kabla hata Dilunga kufunga tayari kuna mashabiki wa Simba walianza kuiota mechi ya Jwaneng Galaxy ya Bostwana ambayo ilirudisha mabao mawili waliyofungwa Gaborone pindi walipocheza katika Uwanja wa Mkapa. Na kisha wakapata bao la tatu ambalo liliitupa Simba nje zaidi katika michuano mikubwa zaidi ya hii. Hatimaye Dilunga akafunga bao muhimu ambalo halikutarajiwa.

Mlinzi mmoja wa Arrows alifanya makosa ya kitoto akaudharau mwili wa Dilunga kwa sababu yeye ana mwili mkubwa. Dilunga alikuwa na akili ya miguuni zaidi, yeye alikuwa na akili ya kupimana ubavu. Dilunga akauchukua mpira na kumfunga kirahisi kipa wa Arrows.

Kuanzia pale mechi ilikuwa imekufa. Arrows walihitajika kufunga mabao mengine matatu kuweza kupita. Wasingeweza. Kama kosa lile lingefanywa na mlinzi wa Simba katika hatua kama hii, tena Uwanja wa Mkapa, leo mitandao yote ingekuwa mgongoni mwake.

Bila ya bao hili la Dilunga, Arrows wangepandisha morali zaidi kwa sababu wangejua kwamba wanahitaji bao moja tu kwenda hatika hatua inayofuata. Ni kama ilivyotokea kwa wale Makhirikhiri. Kila bao moja liliwafanya waamini kwamba jingine linaweza kuja.

Hatimaye Simba wamepita. Nini kinahitajika? Simba wanahitaji kuongeza ubora. Kasi na maelewano ni jambo muhimu. Bahati nzuri kwao ni kwamba sasa wanakwenda katika hatua nyingine ambayo unaweza kufanya kosa na kujisahihisha.

Wanakwenda katika hatua ya makundi ambapo mshindi atapatikana kwa wingi wa pointi au wakati mwingine tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Walau wamevuka katika hatua hii ya hatari ambayo walikuwa wanachezea shilingi mkononi.

Katika hii hatua pia kuna timu nyingi ngumu kama tulivyowaona Arrows, lakini pia kuna wakubwa ambao wameshushwa katika michuano hii kama tunavyowaona Simba. Haitakuwa rahisi kwa Simba lakini hakuna kisichowezekana kama wataamua kufanya kweli.

Kwa sasa kabla hatujafika mbele tusubiri kwanza kuona nini kitatokea wikiendi hii wakati watakapocheza na mkubwa mwenzao pale katika Uwanja wa Mkapa. Wataendelea kujipima kama wana ubavu wa kucheza katika presha kubwa.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz