Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Chama na Tuisila wamechagua kuishi katika dunia tofauti

Chama X Com Clatous Chama

Wed, 30 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Huwa namtazama Tuisila Kisinda. Pasipoti yake inaonyesha ana umri wa miaka 22 tu. sina uhakika kama anasema kweli au vinginevyo. Vyovyote ilivyo, kwa kasi yake hakupaswa kuwa Tanzania. Alipaswa kuwa kwingineko.

Wachezaji kama yeye ni adimu. Ile kasi yake sio ya kawaida. Majuzi alijipatia assistí yake kwanza tangu alipofika nchini. Alifanya kitu kimoja rahisi na kumpasia mpira Fiston Mayele aliyefunga kwa urahisi. Kila kitu kilionekana rahisi.

Subiri kwanza, hafanyi vile kila siku. Mechi inayofuata atajaribu kufanya kitu kigumu. Atakimbia na mpira kwa kasi na kujaribu kupiga shuti kali akiwa upande wa kulia. Anataka kufunga au kufanya nini? Hauwezi kuelewa.

Katika soka la kisasa ule upande anaokaa yeye siku hizi wanacheza wachezaji wanaotumia mguu wa kushoto. Kwa nini? Wanatakiwa waweze kugeuka na kuingia ndani. Mawinga wa siku hizi hawachezi kama mawinga wa zamani.

Anayetumia mguu wa kulia anakaa kushoto, anayetumia mguu wa kushoto anakaa kulia. Lengo ni rahisi tu, kwamba yule anayekaa kule kulia aweze kugeuka na kuingia ndani ya uwanjani huku akiangalia uwezekano wa kupiga krosi nzuri au kufunga.

Akina Bukayo Saka na miguu yao ya kushoto siku hizi ndio huwa wanakaa kule. Akina Lionel Messi wanakaa kule. Akina Mason Greenwood huwa wanakaa kule ili waingie ndani. Haishangazi kuona wanafunga mabao mengi kwa sababu wanapoingia ndani mguu wa kushoto unakuwa katika nafasi nzuri ya kufunga.

Tuisila bado anakaa kulekule kulia angali anatumia mguu wa kulia. Sio kitu kibaya sana lakini kwa staili hii anayoendelea kutumia ya mawinga wa kizamani basi kitu cha kwanza anachopaswa kufikiria ni kutoa pasi watu wafunge. Yeye hawi katika nafasi nzuri ya kufunga zaidi ya kutoa pasi ya mwisho. Inaweza kuwa krosi ndefu au krosi fupi.

Pale Yanga miaka ya karibuni walipita mawinga wawili ambao walikuwa na kasi kubwa ambayo iliwanufaisha washambuliaji wa kati. Mrisho Ngassa na Simon Msuva nao walikuwa mawinga wa kizamani ambao walitumia miguu ya kulia na kukaa upande wa kulia.

Waliibeba Yanga kwa kufanikiwa kupika mabao mengi kwa washambuliaji wa kati. Akina Boniface Ambani na Amiss Tambwe walifunga zaidi kwa kutumia mbio za Ngassa na Msuva katika nyakati tofauti.

Lakini pia tunaishi katika dunia ya kisasa ambayo mashabiki wameanza kuzinduka kuhusu umuhimu wa mchezaji katika kikosi. Kama kuna mchezaji ambaye angeweza kuiweka Yanga katika mfuko wake kwa urahisi zaidi basi angekuwa Tuisila.

Kama angeamua tu asiwe mchoyo na akili yake aielekeze katika kupiga pasi ya mwisho basi Tuisila angeweza kuwa mchezaji muhimu zaidi katika kikosi cha sasa cha Yanga kuliko hawa wengine ambao wanaimbwa. Bahati mbaya hajataka kuielekeza akili yake katika eneo hilo.

Yeye ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ina maana kwamba yeye huwa anawahi zaidi kufika katika lango la wapinzani kupitia ule upande wake. Ingekuwa rahisi zaidi kwake kupika mabao kwa wenzake lakini ukiangalia mbio zake halafu ukiangalia takwimu zake unakutana na kichekesho.

Wakati akiwa katika ubora wake, Thierry Henry alikuwa na kasi sana. Yeye tofauti na Tuisila ni kwamba alikuwa mchezaji wa kisasa zaidi kwa sababu alikuwa anatumia mguu wa kulia lakini anacheza upande wa kushoto. Lengo lilikuwa kuhakikisha anaweza kuingia kwa ndani kulitafuta boksi na kufunga.

Kwa sababu alikuwa ni mchezaji mwenye matumizi mazuri ya akili Henry alikuwa ana uwezo wa kufanya vyote huku akinufaika na kasi yake. Alikuwa na uwezo wa kufunga lakini pia alikuwa ana uwezo wa kupika mabao kwa wenzake. Henry angeweza kumaliza msimu akiwa na mabao 25 huku akiwa na assisti 15.

Lakini katika dunia hii ya kisasa Tuisila alipaswa kujifunza kitu kwa Clatous Chotta Chama wa Simba. Huwa tunasema Chama ndiye Simba na Simba ndiye Chama. Akili yake ameiwekeza katika jambo moja tu, kuwasaidia wenzake kufunga kwa urahisi.

Bahati nzuri zaidi kwa Chama ni kwamba anakaa katika maeneo ya katikati ambayo yangemuwezesha kufunga zaidi lakini hata hivyo akili yake ameiwekeza katika kusaidia wenzake kufunga. Matokeo yake Chama amejichukulia ufalme wake pale Simba. Hata asipofunga watu wa Simba wanafahamu kwamba timu yao haiendi bila ya yeye.

Matokeo yake ni kwamba Chama amekuwa mchezaji muhimu kuliko wachezaji wanaofunga. Mashabiki wa siku hizi sio wajinga. Wanajua kazi ya mchezaji na umuhimu wa mchezaji. Zamani ndipo mashabiki hawakujua umuhimu wa wachezaji wanaopiga pasi ya mwisho.

Aliwahi kunishtua staa wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ambaye katika sherehe fulani ya waandishi wa habari pale Hoteli ya Serena aliulizwa siri ya mafanikio yake katika ufungaji mabao hapo zamani akamtaja, Charles Boniface Mkwassa ambaye alikuwa amekaa kando yake. Wakati Abeid akiwa anatamba pale Yanga sisi wengine tulikuwa wadogo. Lakini hata watu wazima walikuwa hawajui umuhimu wa mchezaji kama Mkwassa kwa Mziba. Mara zote tulikuwa tunawaimba watu waliofunga zaidi bila ya kujali ni nani alikuwa amepiga pasi ya mwisho.

Dunia ya leo imebadilika na kuna hadi wataalamu wa kutunza takwimu ambao wamejitokeza. Hawa wanatukumbusha zaidi umuhimu wa kila mchezaji katika nafasi yake. Chama ameamua kuishi katika dunia mpya wakati Tuisila anaishi katika dunia ya zamani ambayo anaamini kwamba mchezaji muhimu zaidi klabuni ni yule ambaye anafunga mabao.

Kwa kasi yake ilivyo angekuwa ameiweka Yanga mkononi kwa muda mrefu. Lakini kama sio kuiweka Yanga mkononi basi si ajabu angekuwa Ulaya akitamba katika Ligi za Ufaransa au Ubelgiji ambao waliwahi kuitawala Congo nchi yake.

Hata Ulaya wachezaji wenye kasi kama yeye hawapo. Tatizo lake ni lilelile la kujiweka mbele yeye kuliko timu. Kwa kasi yake, Tuisila angeweza kuwa na assisti 10 karibu kila msimu, hasa unapokuwa na wachezaji wenye uwezo wa kufunga kama Mayele.

Columnist: Mwanaspoti