Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Ally Mayay ni zaidi ya mchezaji wa zamani

Ally Mayay Ttt Ally Mayay "Tembele"

Wed, 28 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Jinsi gani Garry Neville na Jamie Carragher walichukuliwa na Kituo cha Sky Sport kufanya kazi ya uchambuzi? Sifa kubwa ya kawaida ni kwamba walikuwa wachezaji wa zamani. Halafu kuna sifa nyingine ambayo inasimama nyuma yao.

Hii sifa nyingine ni uwezo wao wa kuchambua mambo wakiwa kama wachezaji. wakati fulani Carragher alikuwa nahodha msaidizi wa Liverpool wakati nahodha mkuu akiwa Steven Gerrard. Tatizo Gerrard alikuwa anaumia mara kwa mara.

Carragher ndiye ambaye alikuwa anaendesha mahojiano na Kituo cha Sky Sports au waandishi wa habari. Hapo ndipo ungeweza kuona upeo wake wa kufafanua mambo. Ni kama ilivyokuwa kwa Neville ambaye naye kuna wakati alikuwa nahodha wa Manchester United.

Hawakuwa wachezaji wazuri lakini walikuwa na upeo mkubwa wa kuelezea mambo ikiwemo dakika 90 ambazo wametoka kucheza. Walipomaliza tu soka wakawa wachambuzi. Sio kila mchezaji wa zamani anaweza kuwa mchambuzi. Kuna baadhi ya wachezaji wa zamani ukiwasiliza unaishia kushangaa. Hauelewi wanachozungumza.

Majuzi Ally Mayay alipochaguliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Michezo nchini nilikumbuka hadithi hii. Mayay alikuwa katika uchambuzi wa soka Kituo cha Azam. kando hapo alikuwa na nafasi yake serikalini katika eneo la viwanja vya ndege.

Kuna baadhi ya watu wanaojidanganya Ally amechaguliwa kwa sababu ni mchezaji wa zamani. Hapana. Kama amechaguliwa basi ni kwa sababu ya elimu yake na wasifu wake zaidi ya kuwa mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.

Hata kazi yake ya uchambuzi hapa nchini inafanywa na watu wengi ambao hawakucheza soka katika kiwango cha juu kama yeye. Wapo wanaotamani kuona kazi hii inafanywa na wachezaji wa zamani lakini ukweli ni kwamba kuwa mchezaji wa zamani sio kigezo cha kuwa mchambuzi au kocha.

Uchambuzi ni kazi ya maarifa mengine. Ukocha ni kazi ya maarifa mengine. Hata kutawala katika klabu au shirikisho ni kazi ya maarifa mengine. Wachezaji wa zamani mara tu wanapostaafu soka inabidi waongeze maarifa kwa ajili ya kuchukua nafasi nyingine kama uchambuzi, ukocha au utawala katika soka.

Wachezaji wetu wa zamani wamekuwa wakilalamika kuhusu kutopata fursa kama za kufanya kazi ya uchambuzi lakini wasiochelewa wana maarifa machache kuweza kuwepo katika kazi hii. Mara kadhaa nimekuwa nikiwatazama wachezaji wa zamani wanaopewa nafasi ya kufanya uchambuzi katika vituo kadhaa vya redio na televisheni lakini hawaonyeshi maarifa yoyote.

Kikubwa ambacho huwa wanakizungumzia ni namna ambavyo walikuwa hodari wakati wanacheza soka. Wengi utawasikia ‘Enzi zangu hili bao alilokosa Bocco mimi siwezi kukosa”. Anasema hivi bila ya kuzungumzia ambacho kimemtokea Bocco katika wakati husika.

Hata Ulaya na kwingineko kuna wanasoka wengi mahiri wa zamani wameshindwa kazi ya ukocha au uchambuzi. Mmoja wapo ni Pele. Hafahamu lolote la maana kuhusu soka ingawa alikuwa mchezaji mahiri. Wakati mwingine alikuwa akitoa utabiri wa kijinga kuhusu mechi za soka.

Kuna mchezaji kama Jay Jay Okocha. Huwa anaitwa katika Kituo cha Supersport kuchambua mechi lakini simuelewi vema. Nadhani wanalitumia zaidi jina lake kwa ajili ya mvuto lakini sio mtalaamu kama ilivyo kwa Neville na Carragher ambao hawakuwa wachezaji wenye vipawa kama yeye.

Ukiwatazama hata wachezaji wetu wa sasa ni vigumu kuona nani anaweza kuja kuwa mchambuzi wa soka. Mara nyingi nimekuwa nikiwasikiliza wakihojiwa baada ya mechi za Ligi Kuu na wote wanaonekana hawana ufahamu mkubwa na mchezo wenyewe licha ya kwamba wana vipaji vya kuucheza.

Manahodha wa timu zote za Ligi Kuu ni kama wamekariri mahojiano yao. Utawasikia wanasema: “Tunamshukuru Mungu tumemaliza salama. Mpira una matokeo matatu kufungwa kushinda na kutoka sare.” Hapo anakuwa amemaliza.

Mwingine atasema: “Kama kuna mapungufu yoyote basi kocha atakuwa ameyaona na tutayafanyia kazi kwa ajili ya mechi ijayo.” Hivi ndio namna ambavyo wanamaliza mahojiano yao na kisha kuondoka zao.

Kuna kitu zaidi ambacho wachezaji wenzetu wangeweza kusema kufuatana na matukio ya mchezo huo wanaocheza.

Unaweza kumsikia Bruno Fernandes anasema “Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwetu kwa sababu Liverpool waliongeza kasi katika maeneo ya pembeni na hatukuweza kuwadhibiti vema.” Huyu ndiye mchezaji ambaye alikuwa anausoma mchezo huku akiendelea kuucheza. Miaka kadhaa baadaye anaibukia katika kazi ya uchambuzi.

Wachezaji wa sasa na wa zamani kuna umuhimu mkubwa wakafuata nyayo za Ally Mayay. Kitu cha muhimu ni kwenda shule. Lakini pia kujiongezea maarifa katika mchezo wenyewe ni kitu bora zaidi. wachambuzi mahiri ni wale wanaojisomea na kubadilika kutokana na nyakati.

Kwa mfano, kuna wachezaji wengi wa zamani hawaelewi namna mifumo inavyotawala mchezo wenyewe kwa sasa. Wengi wameachwa nyuma kwa kuangalia zaidi mifumo ya zamani katika soka.

Kwa mfano, zamani mfumo maarufu wa soka ulikuwa 4-4-2. Duniani kote kila mahala huo ndio ulikuwa mfumo unaotawala. Lakini sasa kuna mifumo mingi tofauti. Ili usiachwe nyuma inabidi usome haya mambo na kuelewa na hauwezi kujivunia kuwa mchezaji wa zamani katika kuchambua.

Katika utawala kuna watu kama kina Leodeger Tenga. Huyu alikuwa Rais wa TFF. Unaweza kuamua kumkumbuka kama mchezaji wa zamani wa Yanga, Pan Afrika na Taifa Stars lakini kwa kazi yake aliyoifanya TFF aliifanya zaidi kama mtu msomi. Uchezaji wake wa zamani ulikuwa chachu tu lakini kama angekuwa hajaenda shule sidhani kama angeibadili TFF na kuwa bora.

Ulaya wachezaji wengi wa zamani ni wapo katika nafasi za utawala kama vile wakurugenzi wa ufundi, wakurugenzi wa michezo, na vyeo vinginevyo. Hawajavipata kwa sababu ni wachezaji wa zamani. Hapana. Walikwenda shule pia baada ya kustaafu soka.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz